Jumatatu, 26 Agosti, 2024
Leo ni Jumatatu tarehe 21 Mfunguo Tano Safar 1446 Hijria mwafaka na tarehe 26 Agosti 2024.
Katika siku kama ya leo miaka 678 iliyopita mzinga mkubwa ulitumika kwa mara ya kwanza katika historia.
Siku hiyo jeshi la Uingereza lilitumia silaha ya mzinga dhidi ya askari wa Ufaransa.
Katika vita hivyo Mfalme Philip wa Sita wa Ufaransa alishindwa vibaya na jeshi la Uingereza licha ya kwamba jeshi la Ufaransa lililokuwa limekaribia kupata ushindi, lilikuwa na idadi kubwa ya askari na wapiganaji. Ushindi wa jeshi la Uingereza katika vita hivyo ulitokana na utumiaji wa silaha ya mzinga. *

Miaka 281 iliyopita katika siku kama ya leo, alizaliwa mjini Paris Ufaransa Antoine Laurent Lavoisiere, mtaalamu wa kemia wa Kifaransa.
Baada ya kumaliza masomo yake alianza kufanya utafiti katika elimu ya kemia. Miongoni mwa uvumbuzi wa msomi huyo ni kwamba, maji yanaundwa na vitu viwili yaani gesi za oksijeni na haidrojeni na mchango wa hewa ya oksijeni katika kuchomeka vitu mbalimbali.
Mwaka 1794 Antoine Laurent Lavoisiere alituhumiwa kuwa anapinga mapinduzi na kunyongwa hapo baadaye.

Siku kama ya leo miaka 128 iliyopita askari wa utawala wa Kiothmani walianza kufanya mauaji ya umati dhidi ya Waarmenia.
Waturuki wa Kiothmani walifanya mauaji hayo kwa kisingizio kwamba Waarmenia waliwasaidia Wagiriki katika ghasia zilizofanyika dhidi ya utawala wa Kiothamani. Maelfu ya wanawake, wanaume na watoto wadogo wa Kiarmeni waliuawa kwa umati katika mauaji hayo yaliyoendelea kwa kipindi cha siku tano. **

Tarehe tano Shahrivar miaka 46 iliyopita kwa mujibu wa kalenda ya Kiirani, mwanzo wa kalenda ya Iran ulirejeshwa tena katika mwaka wa Hijria Shamsia kutoka mwanzo wa tarehe wa Kifalme.
Katika miaka ya kabla ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu utawala wa kidikteta wa Pahlavi ambao ulitambua mafundisho ya Uislamu kuwa ni kinyume na maslahi yake, ulikuwa ukifanya njama za kukabiliana na Uislamu kwa kutumia utajiri na turathi ya kihistoria ya Iran.
Katika mkondo huo bunge la kimaonyesho la utawala wa Kipahlavi lilipasisha sheria iliyobadilisha mwanzo wa kalenda ya Iran kutoka mwaka wa Hijra ya Mtume (saw) na kuifanya kuwa tarehe ya kuvikwa taji la Mfalme Kurosh wa silsila ya Khahamaneshi. Hatua hiyo ilikabiliwa na hasira na malalamiko makubwa ya Imam Ruhullah Khomeini na wananchi Waislamu wa Iran.
Kubadilishwa huko kwa mwaka wa Hijria na kufuata mwaka wa Kifalme nchini hakukudumu kwa zaidi ya kipindi cha miaka miwili na nusu na utawala wa Shah uliokuwa ukikabiliwa na harakati za Mapinduzi ya Kiislamu ulilazimika kutambua tena mwaka wa Hijra ya Mtume (saw) kutoka Makka kwenda Madina kuwa ndiyo mwanzo wa kalenda nchini Iran.

Miaka 34 iliyopita mwafaka na siku hii ya leo alifariki dunia Ali Akbar Kaveh, mwalimu mkubwa wa sanaa ya kaligrafia ya hati za Kifarsi.
Mtaalamu huyu alizaliwa mwaka 1271 Hijria mjini Shiraz, moja ya miji ya kusini mwa Iran na kuanza kujihusisha na masuala ya karigrafia. Baada ya hapo Ali Akbar Kaveh alipata kusoma kwa walimu wakubwa wa zama hizo kama vile Mirza Twahir Katib, Homayun Hamedani na Imad Al Katib Seifi Qazwini na hatimaye akawa hodari mkubwa katika sanaa ya kaligrafia.

Siku kama ya leo tarehe 5 Shahrivar nchini Iran ni siku ya kumkumbuka Muhammad bin Zakaria Razi, msomi mtajika wa Kiislamu.
Muhammad bin Zakaria Razi alizaliwa mwaka 251 hijria katika mji wa Rei nchini Iran na alianza kujifunza kemia na fizikia akiwa bado kijana. Tabibu na mkemia Muhammad bin Zakaria Razi alijifunza pia elimu nyingine kama vile tiba, mantiki na falsafa. Baadaye Razi alifanikiwa kutengeneza asidi ya sulfuriki kwa kustafidi na mada asilia.
Msomi huyo wa Kiislamu Muirani alikuwa shakhsia wa kwanza kuvumbua alkoholi. Muhammad bin Zakaria Razi ameandika vitabu 56 vya tiba, 33 vya sayansi ya asili, 17 vya falsafa, 14 vya teolojia, 22 vya kemia na makumi ya vita katika nyanja mbalimbali.
Msomi huyo wa Kiislamu alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 60 na alizikwa katika mji wa Rei ambao hii leo uko kusini mwa Tehran.
