Oct 04, 2024 02:20 UTC
  • Ijumaa, tarehe 4 Oktoba, 2024

Leo ni Ijumaa tarehe 30 Mfunguo Sita Rabiul Awwal 1446 Hjria sawa na Oktoba 4 mwaka 2024.

Siku kama ya leo miaka 194 iliyopita, Ubelgiji ilijitangazia uhuru.

Mwanzoni mwa karne ya 18 Ubelgiji ilikuwa chini ya udhibiti wa Austria, huku ikidhibitiwa na Ufaransa mwishoni mwa karne hiyo hiyo. Hata hivyo baada ya Napoleon Bonaparte kushindwa na madola ya Ulaya, mwaka 1815 Ubelgiji na Uholanzi ziliunda muungano.

Hata hivyo muungano huo haukudumu kwa muda mrefu kufuatia Wabelgiji wa Kikatoliki kuanzisha uasi dhidi ya Waholanzi wa Kiprotestanti na hivyo kuamua kujitangazia uhuru wao katika siku kama ya leo.

Katika siku kama ya leo miaka 96 iliyopita tabibu Alexander Fleming alivumbua dawa ya penicillin.

Fleming ambaye alikuwa daktari maarufu nchini Uingereza, alizaliwa tarehe Sita Agosti mwaka 1881 katika familia ya wakulima mjini Lochfield farm, magharibi mwa Scotland. Fleming alivumbua dawa hiyo baada ya kuona kuwa askari wengi walikuwa wakipoteza maisha kutokana na kukumbwa na bakteria wa maambukizi kwenye majeraha, suala ambalo lilimtia wasi wasi mkubwa.

Miaka 10 baada ya kumalizika vita, sawa na tarehe Nne Oktoba mwaka 1928 Miladia, Fleming alifanikiwa kuvumbua dawa ya penicillin, ambayo huua vijidudu vya maambukizi kwenye kidonda.

Siku kama ya leo miaka 67 iliyopita satalaiti ya kwanza ilirushwa angani na msomi wa Urusi ya zamani na kwa utaratibu huo zama za udhibiti wa anga zikawa zimeanza.

Satalaiti hiyo iliyopewa jina la Sputniki 1 ilizunguka dunia mara 1400 kwa siku 92 na kwa mara ya kwanza ikafikisha ujumbe wa radio kutoka angani kuelekea ardhini. 

Miaka 46 iliyopita katika siku kama ya leo  Imam Khomeini (MA) mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran aliondoka Iraq na kuhamia Paris, Ufaransa.

Imam Khomeini aliamua kufanya hijra hiyo ya kihistoria wakati utawala wa zamani wa Iraq ulipoanza kumzuia kufanya harakati za mapambano dhidi ya utawala wa Shah. Serikali ya wakati huo ya Iraq ambayo ilikuwa ikilinda uhusiano wake na utawala wa Shah nchini Iran, ilimtaka Imam Khomeini ajiepushe na harakati zozote za kisiasa na za kimapinduzi dhidi ya utawala huo wa Shah.

Hata hivyo Imam aliiambia serikali hiyo kuwa hilo lilikuwa jukumu lake la kisheria ambalo aliwajibika kulitekeleza na kusisitiza juu ya kuendelezwa mapambano kwa kutoa hotuba na kutuma kanda za kimapinduzi nchini Iran. 

 

Tags