Nov 03, 2024 02:28 UTC
  • Jumapili, 03 Novemba, 2024

Leo ni Jumapili tarehe Mosi Mfunguo Nane Jamadul-Awwal 1446 Hijria mwafaka na 3 Novemba 2024 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 235 iliyopita, yaani mwaka 1211 Hijiria, alifariki dunia mshairi mkubwa wa Kiislamu, Sheikh Muhammad Kadhim Tamimi Baghdadi, maarufu kwa jina la Uzri akiwa na umri wa miaka 80. Alikuwa msomi na mwanafasihi mkubwa na ameacha diwani ya mashairi. Miongoni mwa mashairi ya malenga huyu maarufu wa Kiislamu ni shairi maarufu la "Al Uzriya" ambalo linamsifu Mtukufu Mtume Muhammad (saw) na kizazi chake kitukufu na kubainisha misingi ya dini ya Uislamu. Shairi hilo lina zaidi ya beti 1000.

 

Miaka 137 iliyopita Ayatullah Mirza Muhammad Hassan Shirazi alitoa fatuwa maarufu ya kuharamisha tumbaku na sigara ili kuzuia uporaji uliokuwa ukifanywa na wakoloni wa Kiingereza katika nchi za Kiislamu. Fatuwa hiyo ilitolewa baada ya mfalme Nasiruddin Shah wa Iran kutia saini mkataba wa kuipa kampuni moja ya utawala wa kikoloni wa Uingereza mamlaka ya kuuza na kununua tumbaku ya Iran kwa kipindi cha miaka 50. Jina la Mirza Shirazi ni mashuhuri mno kutokana na fatuwa hiyo ya kuharamisha tumbaku. Fatuwa yake hiyo ya kuharamisha tumbaku na matumizi ya sigara, bidhaa ambayo ilikuwa imehodhiwa na Uingereza, ilitoa pigo kubwa kwa ukoloni wa Uingereza nchini Iran. Vilevile fatua hiyo ilitambuliwa kuwa mapambano ya moja kwa moja dhidi ya utawala wa Shah na ukoloni wa Uingreza nchini Iran na iliandaa uwanja wa mapambano ya baadaye ya wananchi wa Iran dhidi ya dhulma, ukandamizaji na ukoloni wa wageni.

Ayatullah Mirza Muhammad Hassan Shirazi

 

Siku kama ya leo miaka 121 iliyopita, nchi ya Panama ilifanikiwa kujipatia uhuru wake kutoka Colombia na siku hii huadhimishwa nchini humo kama siku ya taifa. Ardhi ya Panama iligunduliwa na kukaliwa kwa mabavu na Wahispania mnamo mwaka 1501 Miladia. Panama ilikaliwa kwa mabavu na Colombia mwaka 1821 Miladia na tangu wakati huo wananchi wa nchi hiyo walianzisha mapambano dhidi ya wavamizi wa Colombia. Mapambano hayo ya wananchi yalishadidi zaidi baada ya kuwasilishwa mpango wa mfereji wa Panama. Mwaka 1903, Panama ikafanikiwa kujitenga na Colombia na kujitawala. 

 

Miaka 68 iliyopita muwafaka na siku kama hii ya leo, wakati wa kujiri mashambulio ya askari wa utawala dhalimu wa Israel dhidi ya Misri, wanajeshi wa utawala huo waliuvamia mji wa Khan Yunis katika Ukanda wa Gaza huko Palestina na kuwaua kwa umati wakazi wa mji huo. Baada ya kuukalia kwa mabavu mji huo, askari hao waliwanyonga askari 25 wa Kimisri. Unyama wa askari hao haukuishia hapo, kwani waliishambulia hospitali ya mkoa mjini Khan Yunis na kuwaua kwa umati wauguzi, madaktari na wagonjwa wote waliokuwa wamelazwa katika hospitali hiyo. Watu wapatao 275 waliuawa katika mashambulio hayo.  

 

 

Siku kama ya leo miaka 60 iliyopita, askari vibaraka wa utawala wa Shah uliokuwa ukitawala Iran waliivamia nyumba ya kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Imam Ruhullah Khomeini mjini Qum na kumtia mbaroni. Baada ya kumhamishia mjini Tehran, utawala wa Shah ulimbaidishia Imam Khomeini nchini Uturuki. Utawala wa Shah uliamua kufanya hivyo kutokana na uungaji mkono wa Imam Khomeini kwa harakati za mapambano za wananchi Waislamu wa Iran za kutaka kujitawala, uhuru na kutetea thamani za Kidini. Lengo la kumpeleka uhamishoni Imam Khomeini lilikuwa kusimamisha mapambano yake na wananchi Waislamu wa Iran dhidi ya utawala huo kwani utawala wa Shah ulitambua kwamba kuwepo Imam nchini kunawaamsha wananchi dhidi ya utawala huo wa kidikteta. ***

Imamu Khomeini akiwa nchini Uturuki

 

Miaka 46 iliyopita na katika siku kama ya leo yaani tarehe 13 Aban mwaka 1357 Hijria Shamsia, kulifanyika maandamano makubwa ya wanafunzi na wanachuo mjini Tehran. Maandamano hayo ya yalikandamizwa vibaya na askari wa utawala wa Shah na kusababisha umwagaji damu mkubwa. Katika siku kama hii ambayo ilisadifiana na kumbukumbu ya kubaidishwa Imam Khomeini huko Uturuki, kundi kubwa la wanafunzi na wanachuo, wakiwa na lengo la kulaani kitendo hicho cha mfalme Shah walikusanyika katika Chuo Kikuu cha Tehran. Askari wa utawala wa Shah walishambulia kundi hilo la wanachuo na wanafunzi na kuwauwa shahidi wanafunzi na wanachuo wengi. Tarehe 13 Aban ina umuhimu mkubwa katika historia ya Mapinduzi ya Kiislamu, na ndio maana imepewa jina la "Siku ya Mwanafunzi." ***

Siku kama ya leo 45 iliyopita, wanafunzi na wanachuo wa Tehran walifanya maandamano makubwa katika mji huo kwa mnasaba wa kukumbuka tukio la kupelekwa uhamishoni nchini Uturuki Imam Khomeini MA na kwa mnasaba wa kutimia mwaka mmoja tangu kuuawa wanafunzi na wanachuo wa Iran. Mauaji hayo yalifanywa na vikosi vya usalama vya utawala wa Shah. Wanafunzi na wanachuo kadhaa wa Kiislamu walioshiriki kwenye maandamano hayo ambao walikuwa wakijulikana kama Wafuasi wa Sera za Imam, waliuvamia ubalozi wa Marekani mjini Tehran, ambao ulikuwa pango la ujasusi dhidi ya wananchi wa Iran. Siku hii inajulikana katika kalenda ya Iran kwa jina la  Siku ya Kupambana na Uistikbari wa Kimataifa.***

Tarehe 13 Aban, Siku ya Kupambana na Uistikbari wa Kimataifa