Nov 28, 2024 02:50 UTC
  • Alkhamisi tarehe 28 Novemba 2024

Leo ni Alkhamisi tarehe 26 Jamadil Awwal 1443 Hijria sawa na Novemba 28 mwaka 2024.

Siku kama ya leo miaka 267 iliyopita, alizaliwa William Blake mshairi na mchoraji wa Kiingereza.

Blake alikuwa na mapenzi na sanaa tangu akiwa mdogo na alipofikisha rika la ubarobaro alijihusisha na kusoma vitabu vya falsafa na mashairi. Athari za mshairi huyo zilikuwa zikipingana wazi na kanisa, hali ambayo iliwakasirisha mno viongozi wa dini ya Kikristo na watawala wa Uingereza. Hadi anaaga dunia mwaka 1827, msomi huyo wa Uingereza alikuwa ameandika vitabu 13.

Miongoni mwa vitabu vyake mashuhuri ni The Marriage of Heaven and Hell, The Tiger, The Chimney Sweeper na The Lamb.   

William Blake

Tarehe 28 Novemba mwaka 1820 alizaliwa mwanafalsafa mashuhuri wa Ujerumani, Friedrich Engels.

Alikuwa rafiki na mshirika wa karibu wa mwanafalsafa mwingine wa Ujerumani kwa jina la Karl Marx. Engels alifuatiliwa na kusakwa na vyombo vya dola kutokana na harakati zake za kisiasa na mwaka 1850 alikimbilia nchini Uingereza. Engels na Karl Marx walitayarisha Manifesto ya Ukomunisti iliyotangazwa na vyama vya kikomunisti katika mkutano wao wa kwanza hapo mwaka 1848.

Baada ya  Karl Marx, Friedrich Engels alikuwa na nafasi muhimu katika kubuni nadharia za kikomunisti ambazo ziliugawa ulimwengu katika kambi mbili za kisoshalisti na kibepari.   

Friedrich Engels

Katika siku kama ya leo miaka 112 iliyopita, nchi ya Albania ilipata uhuru.

Nchi hiyo ilikuwa huru miaka mingi kabla ya kuzaliwa Nabii Issa Masih AS, lakini baada ya kuasisiwa ufalme wa Roma ilikaliwa kwa mabavu na utawala huo. Mwaka 1501 Albania ilidhibitiwa na utawala wa Othmaniya.

Mwanzoni mwa karne ya 19 utawala huo ulidhoofika na kupoteza nchi za Balkan ilizokuwa ikizitawala na kwa juhudi za wapigania uhuru, hatimaye mwaka 1912 Albania ikajipatia uhuru.   

Siku kama ya leo miaka 64 iliyopita Mauritania ilitangaza rasmi uhuru wa nchi hiyo. Mauritania ilikuwa ikikoloniwa na Ureno tangu karne ya 15 Miladia.

Baadaye Uholanzi na Uingereza ziliivamia nchi hiyo na mwaka 1903 Mauritania ikawa koloni la Ufaransa. Katika nusu ya pili ya karne ya ishirini wananchi wa Mauritania walipiga kura ya maoni wakitaka kuasisiwa utawala wa jamhuri ya mamlaka ya ndani.

Hatimaye mwaka 1960 Mauritania ilipata uhuru kamili baada ya kusainiwa makubaliano kati yake na serikali ya Ufaransa.   

Miaka 53 iliyopita katika siku kama ya leo Iran ilivirejesha kwenye mamlaka yake visiwa vitatu vya Tombu Kubwa, Tombu Ndogo na Bu Musa baada ya kuondoka vikosi vamizi vya Uingereza katika maeneo hayo.

Uingereza iliondoka katika visiwa hivyo vitatu vya Iran vilivyoko katika Ghuba ya Uajemi katika fremu ya mpango wa nchi hiyo wa kuondoa wanajeshi wake katika eneo la Bahari ya Mediterranean na Ghuba ya Uajemi kutokana na matatizo ya kisiasa na kiuchumi yaliyokuwa yakiisumbua nchi hiyo. 

 

 Miaka 30 iliyopita katika siku kama ya leo, inayosadifiana na tarehe 8 Azar mwaka 1373 alifariki dunia Ayatullah Muhammad Ali Araki, mmoja wa marjaa wakubwa wa taqlidi wa Waislamu akiwa na umri wa miaka 103.

Mwanzuoni huyo wa Kiislamu alizaliwa katika mji wa Arak katikati mwa Iran na tangu akiwa na umri mdogo alikuwa na shauku kubwa ya kujifunza elimu ya dini.

Ayatullah Muhammad Ali Araki kwa muda mrefu alifundisha katika chuo kikuu cha kidini cha Qum na miongoni mwa vitabu vyake ni risala ya Ijitihadi na Taqlidi pamoja na Sherhe ya Uruwatul Uthqaa.

Ayatullah Muhammad Ali Araki

Na miaka 14 iliopita sawa na tarehe 8 mwezi Azar mwaka 1389 Hijria Shamsia, Madakta Majid Shahriyari na Fereydun Abbasi waliokuwa Wahadhiri wa Fizikia ya Nyuklia wa Iran walilengwa katika mashambulio mawili tofauti ya kigaidi mjini Tehran.

Dakta Abbasi alijeruhiwa ambapo Dakta Majid Shahriyari Mhadhiri wa Chuo Kikuu, Mwanafizikia na Msomi wa Nyuklia wa Iran akauawa shahidi katika shambulio hilo. Magaidi waliofanya jinai hiyo walitiwa nguvuni na kukiri kwamba wanashirikiana na shirika la ujasusi la Israel MOSSAD.

Dakta Majid Shahriyari