Jumatano, Julai 27, 2016
Leo ni Jumatano tarehe 22 Shawwal 1437 Hijria sawa na Julai 27, 2016.
Miaka 27 iliyopita wananchi Waislamu wa Iran walishiriki kwenye kura ya maoni na kupasisha kwa kura nyingi mabadiliko yaliyofanywa katika Katiba ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Imam Khomeini Mwenyezi Mungu amrehemu muda mfupi kabla ya kufariki dunia yaani mwezi Khordad mwaka 1368 Hijria Shamsiya aliagiza kutekelezwa marekebisho hayo na kuasisiwa baraza maalumu kwa ajili ya lengo hilo.
Siku kama ya leo miaka 192 iliyopita, alizaliwa huko Paris nchini Ufaransa Alexandre Dumas, Fils (mtoto) mwandishi wa vitabu na wa michezo ya kuigiza. Fils alikuwa mwana wa Alexandre Duma, Jenerali wa jeshi na mwandishi wa Kifaransa. Kipindi cha utotoni cha Fils kilikuwa cha mashaka na taabu nyingi, masaibu ambayo ameyataja pia katika athari zake za uandishi.
Miaka 244 iliyopita, katika siku kama ya leo ulitiwa saini mkataba wa kwanza wa kuigawa Poland kati ya madola matatu makubwa ya Ulaya katika karne ya 18. Poland ambayo hii leo ni moja ya nchi zilizo huru za mashariki mwa Ulaya, iligawanywa baina ya nchi tatu za Urusi, Austria na Prussia kwa kutiwa saini makubaliano yaliyotajwa. Ni muhimu kuashiria hapa kwamba hadi sasa Poland imeshawahi kugawanywa mara nne kati ya nchi tofauti.
Na tarehe 6 Mordad mwaka 1388 Hijria aliaga dunia mtengeneza filamu mashuhuri wa Iran, Saifullah Dad. Alizaliwa Shirazi kusini mwa Iran na kupata shahada ya masuala ya jamii. Dad alishika nyadhifa mbalimbali rasmi kama mwanachama katika Baraza la Filamu na mjumbe wa Taasisi ya Filamu ya Farabi. Mwaka 1376 hadi 1379 Hijria Shamsia alikuwa Naibu Waziri wa Utamaduni Na Miongozi ya Kiislamu katika masuala ya filamu. Saifullah Dad ametengeneza filamu kadhaa au kushitiki katika uzalishaji wa filamu kama Kanimanga, Waliosalia, Chini ya Mvua, Iblisi, Watoto wa Talaka na Machinjio na Penzi. Alifariki dunia mwaka 1577 kutokana na maradhi ya saratani.