Jan 09, 2025 02:31 UTC
  • Alkhamisi, Januari 9, 2025

Leo ni Alkhamisi tarehe 8 Rajab 1446 Hijria sawa na Januari 9 mwaka 2025 Milaadia.

Siku kama ya leo mwezi 8 Rajab, yaani miaka 413 iliyopita kwa mujibu wa kalenda na Hijria, alizaliwa faqihi na mwanazuoni mashuhuri wa Kiislamu Sheikh Abu Jaafar Muhammad bin Hassan maarufu kwa jina la Sheikh Hurr al Aamili huko Jabal Amil nchini Lebanon.

Baada ya utafiti na uchunguzi wa muda mrefu Sheikh Aamili alitokea kuwa miongoni mwa maulama wakubwa wa zama hizo hususan katika elimu za fiqhi na Hadithi. 

Sheikh Hurr al Amili ameandika vitabu vingi katika taaluma hizo na miongoni mwake ni kile cha Wasailu Shia ambacho kina nafasi maalumu katika elimu ya fiqhi. Kitabu kingine muhimu cha mwanazuoni huyo ni Hidayatul Ummah. Mwanazuoni huyo aliaga dunia mwaka 1114 Hijria. ***

Sheikh Hurr al Aamili

Siku kama ya leo miaka 233 iliyopita, kulitiwa saini makubaliano ya amani baina ya wafalme wawili wa utawala wa Othmania na Urusi, makubaliano ambayo yalihitimisha vita vya Ulaya katika karne ya 18.

Vita hivyo vilianza mwezi Agosti mwaka 1787 wakati utawala wa Othmania ulipotangaza vita dhidi ya Russia na Austria. Hii ni kwa kuwa nchi hizo mbili zilikuwa na mpango wa kuigawa dola ya Othmania.   ***

Katika siku kama ya leo miaka 117 iliyopita, alizaliwa Simone De Beauvoir, mwandishi wa kike wa Ufaransa.

Beauvoir alisoma elimu ya hisabati na falsafa katika chuo kimoja kikuu cha nchi hiyo na baada ya kuhitimu masomo akaanza kufundisha elimu ya falsafa. Simone De Beauvoir alikuwa mfuasi wa mrengo wa kushoto wa ufeministi, ambapo alitaka kuondolewa ubaguzi ndani ya jamii ya wanawake.

Kitabu chake cha 'Jinsia ya Pili' ni moja ya athari zake mashuhuri katika uwanja huo. Hata hivyo mwanamke huyo alifuata njia ghalati zaidi, ambapo kupitia kampeni yake ya kile alichokiita kuwa ni kudai uhuru wa mwanamke, badala ya kusisitizia nafasi ya kimaumbile aliyonayo mwanamke, alihalalisha mwanamke kuavya mimba, kuishi bila ya kuolewa na kufanya usagaji, suala ambalo limekuwa na madhara makubwa kwa jamii ya wanawake.

Bi. Simone De Beauvoir mwenyewe alikuwa na mahusiano haramu na profesa Jean-Paul Sartre kuanzia mwaka 1929 hadi mwaka 1980 alipofariki dunia, suala ambalo linadhihirisha undumakuwili wa kampeni za ufeministi. ***

Simone De Beauvoir

Siku kama ya leo miaka 103 iliyopita alizaliwa Ahmed Sékou Touré, kiongozi wa mapinduzi ya Guinea.

Touré aliingia katika mapambano ya kupigania uhuru wa nchi yake kutoka mikononi mwa mkoloni Mfaransa akiwa bado kijana. Mwaka 1952 Ahmed Sékou Touré alichaguliwa kuwa mkuu wa chama cha Demokrasia nchini Guinea na kuendeleza mapambano ya amani dhidi ya mkoloni huyo.

Hatimaye mwaka 1958 nchi hiyo ilipata uhuru na mwaka mmoja baadaye Touré akateuliwa kuwa rais na kusalia madarakani hadi mwaka 1984 alipofariki dunia.   ****

Ahmed Sékou Touré

Tarehe 9 Januari miaka 65 iliyopita ilianza operesheni ya kujenga bwawa kubwa la Aswan huko katika mto Nile nchini Misri.

Ujenzi wa bwawa hilo ulikuwa miongoni mwa mipango muhimu ya kiuchumi ya Misri iliyotangazwa mwaka 1953 na rais wa wakati huo wa nchi hiyo, Gamal Abdulnasir.

Nchi za Magharibi pia zilitangaza kuwa zilikuwa tayari kusaidia na kushiriki kwenye ujenzi wa Bwawa la Aswan. Hata hivyo baada ya mfereji wa Suez kutaifishwa na Rais Gamal Abdulnasir mwaka 1956 na vikosi vya Ufaransa, Uingereza na utawala wa Kizayuni kuendesha mashambulio ya pamoja dhidi ya Misri, serikali hizo za Magharibi zilikataa kusaidia ujenzi wa bwawa hilo.

Bwawa la Aswan huzalisha megawati 2100 za umeme na kusaidia shughuli za kilimo cha umwagiliaji katika eneo la kusini mwa Misri. ***

Bwawa la Aswan

Januari 9 miaka 61 iliyopita ulitokea uasi mkubwa dhidi ya Marekani huko Panama kufuatia kupeperushwa bendera ya Marekani katika eneo la Mfereji wa Panama.

Wanajeshi wa Marekani waliwauwa na kuwajeruhi wananchi wengi wa Panama katika uasi huo. Marekani iliasisi vituo vya kijeshi katika maeneo 134 ya Panama wakati wa Vita vya Pili vya Dunia na kuikalia kwa mabavu kikamilifu nchi hiyo. ***