Alkhamisi, tarehe 23 Januari, 2025
Leo ni Alkhamisi tarehe 22 Rajab 1446 Hijria sawa na 23 Januari mwaka 2025.
Siku kama ya leo miaka 218 iliyopita, inayosadifiana na 22 Rajab 1228 Hijria, alifariki dunia Allamah Sheikh Jaafar Kashiful Ghitwa, mwanachuoni mashuhuri wa Kiislamu mjini Najaf, Iraq.
Allamah Kashiful Ghitwa alikuwa mwanachuoni aliyebobea kwenye taaluma mbalimbali za kielimu kama fiqhi, usulul fiqh, tafsiir ya Qur'ani na Hadith. Mwanachuoni huyo ameandika vitabu vingi vikiwemo, Kashful Ghitwaa na al Al A'qaaidul Jaafariyyah.

Miaka 193 iliyopita katika siku kama ya leo Edouard Manet mchoraji mahiri wa Kifaransa alizaliwa. Awali Edouard alikuwa na mapenzi makubwa na ubaharia.
Hata hivyo baadaye alianza kujihusisha na uchoraji na kuonyesha kipaji kikubwa katika sanaa hiyo. Kazi zake ziliwavutia wengi. Edouard Manet aliaga dunia 1883.

Katika siku kama ya leo miaka 127 iliyopita alizaliwa Sergei Mikhailovich Eisenstein mwananadharia na muongozaji wa filamu wa nchini Russia.
Aliongoza na kutengeneza filamu yake ya kwanza mwaka 1925 iliyojulikana kwa jina la Strike yaani mgomo. Filamu ya pili ya Sergei Mikhailovich Eisenstein iliyojulikana kwa jina la Battleship Potemkin ilileta mageuzi makubwa katika Sanaa ya filamu na sinema ulimwenguni.
Miongoni mwa athari nyingine za Mikhailovich ni Seed of Freedom, Ten Days that Shook the World na Time in the sun. Mwongozaji filamu huyo aliaga dunia 1948.

Katika siku kama ya leo miaka 106 iliyopita yaani tarehe 23 Januari 1919, Chama cha Kifashisti cha Italia kiliasisiwa na Benito Mussolini. Wanachama wa chama hicho walikuwa wakivaa mashati meusi kama sare zao.
Sare hiyo ilipelekea wafuasi wa chama hicho kujulikana kwa jina la watu wa " Mashati Meusi'.'' Fikra za Kifashisti zilikuwa zimejengeka juu ya misingi ya kuunda dola moja kubwa la kidikteta na fikra hizo zilikuwa zikipingana na aina yoyote ya uhuru. Oktoba mwaka 1922, Benito Mussolini na wafuasi wake waliuteka mji wa Roma na yeye mwenyewe akashika hatamu za uongozi akiwa Waziri Mkuu. Kuanzia hapo kiongozi huyo alianza kutekeleza malengo na sera za Chama cha Kifashisti.
Hata hivyo mwaka 1945, mwishoni mwa Vita vya Pili vya Dunia Benito Mussolini alitiwa mbaroni na wazalendo na kisha akanyongwa.

Miaka 75 iliyopita katika siku kama ya leo, Bunge la utawala haramu wa Israel (Knesset) liliutangaza mji wa Baitul Muqaddas ambao ni kibla cha kwanza cha Waislamu, kuwa mji mkuu wa utawala huo badala ya Tel Aviv.
Uamuzi huo uliofikiwa na Bunge hilo miaka miwili tu baada ya kuasisiwa utawala ghasibu wa Israel katika ardhi za Wapalestina, uliwakasirisha mno Waarabu na Waislamu.
Njama hiyo ya Israel iliyolenga kupata ridhaa ya nchi nyingine ili ziutambue rasmi mji huo kama mji mkuu wake na hivyo zihamishie balozi zao katika mji huo, haikuwa na natija, kwani hadi leo mji wa Tel Aviv ungali unatambuliwa kama mji mkuu wa utawala huo vamizi unaozikalia kwa mabavu ardhi za Palestina.

Tarehe 5 Bahman miaka 46 iliyopita matabaka mbalimbali ya wananchi wa Iran waliendeleza maandamano makubwa katika miji mbalimbali dhidi ya utawala kibaraka wa Shah licha ya mamluki wa mfalme huyo kutumia mbinu zote za ukatili na ukandamizaji.
Siku hiyo wananchi Waislamu wa Iran walipuuza marufuku iliyokuwa imetangazwa ya kuzuia mikusanyiko ya zaidi ya watu mawili katika miji mbalimbali ya Iran.
Ukandamizaji mkubwa wa maajenti wa utawala wa Shah ulipelekea kuuawa shahidi idadi kubwa ya raia. Siku hiyo hiyo idadi kubwa ya maafisa wa Jeshi la Anga la Iran ilijiunga na harakati ya mapambano ya wananchi katika mitaa ya jiji la Tehran na kufanya maandamano dhidi ya utawala wa Shah.
Askari hao walitangaza utiifu wao kwa Imam Ruhullah Khomeini na harakati ya Mapinduzi ya Kiislamu.
