Jumatano, 29 Januari, 2025
Leo ni Jumatano tarehe 28 Rajab, 1446 Hijria sawa na tarehe 29 Januari, 2025.
Siku kama ya leo miaka 1386 iliyopita, ilianza safari ya msafara wa Imam Hussein (as) kutoka Madina kwenda mjini Makka.
Hatua hiyo ilijiri baada ya kufariki dunia Muawiyah Bin Abu Sufiyan tarehe 15 ya mwezi wa Rajab na kutwaa madaraka mwanaye, Yazid Bin Muawiyah.
Baada ya Yazid kutwaa madaraka, haraka sana alimtaka mtawala wa mji wa Madina amlazimishe Imamu Hussein (as) kutoa baia (kiapo cha utiifu) kwake na kwamba iwapo angekataa kufanya hivyo basi amuuwe. Kwa kuzingatia kwamba Yazid alikuwa mtu muovu na mtenda madhambi, Imamu Hussein alikataa kutoa kiapo hicho na kwa ajili hiyo akaamua kuondoka Madina yeye na watu wa familia ya Mtume Muhammad (saw) kuelekea mjini Makkah.
Kabla ya kuanza safari hiyo, Imamu Hussein (as) alimuusia kaka yake Muhammad Ibnil-Hanafiyyah akisema: "Ninatoka kwa ajili ya kurekebisha umma wa babu yangu, Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw); ninataka kuamrisha mema na kukataza maovu na kufuata njia ya babu yangu, Muhammad, na baba yangu, Ali Ibn Abi Twalib (as)…."
Baada ya kufika Makka na kufuatia kukithiri barua za watu wa mji wa Kufa Iraq, waliokuwa wamemtaka aelekee huko kwa ajili ya kuwaongoza, Imamu Hussein (as) aliamua kuelekea Kufa ambapo hata hivyo alizuiliwa na jeshi la Yazid eneo la Karbala na kuuawa shahidi yeye na watu wa familia ya Mtume (saw) katika eneo hilo.

Miaka 288 iliyopita, mnamo Januari 29, 1737 alizaliwa Thomas Paine, mwanasiasa na mwandishi mwanamapinduzi wa Uingereza.
Baada ya kumaliza masomo yake ya elimu ya kati Paine aliamua kujishughulisha na kazi mbalimbali lakini hakufanikiwa katika yoyote kati ya hizo.
Hatimaye mnamo mwaka 1774, yaani mwaka mmoja kabla ya kuanza vita vya uhuru wa Marekani aliwasili nchini humo na kuanza kazi ya uandishi. Tasnifu yake iliyoitwa "Akili Timamu" iliwaathiri mno wananchi na viongozi wa Marekani na kuimarisha azma yao ya kujikomboa kutoka kwenye makucha ya Uingereza. Baada ya uhuru wa Marekani, Thomas Paine alirejea kwao Uingereza ambako aliandika kitabu "Haki za Mtu" kutetea Mapinduzi ya Ufaransa.
Kwa sababu huko Uingereza alitambuliwa kama haini, Paine alilazimika kuelekea Ufaransa ambako alichaguliwa kuwa mjumbe wa Baraza la Taifa. Alifia Marekani mwaka 1809 katika hali ya simanzi na ufakiri.
Siku kama ya leo miaka 109 iliyopita alifariki dunia Ayatullahil-Udhma Sayyid Mohammed Kazem Tabatabai Yazdi maarufu kwa jina la Allamah Yazdi, msomi mashuhuri wa elimu ya fiqhi.
Baada ya kuhitimu masomo yake ya msingi alijiunga na hauza ya kielimu ya mjini Najaf, Iraq na kupata kusoma kwa maulama wakubwa wa zama hizo kama vile Ayatullah Mirza Shirazi ambapo alifikia daraja ya ijtihadi.
Baada ya hapo alijishughulisha na kazi ya ufundishaji huku akihusika pia na kuasisi vituo vya misaada, misikiti na shule za kidini. Ameacha taathira mbalimbali lakini maarufu ni kitabu cha 'Al Urwatul-Wuthqa' na 'Bustane Niyaz' ambacho kinahusiana na dua.
Miaka 99 iliyopita, mnamo tarehe 29 Januari 1926, alizaliwa Profesa Muhammad Abdussalam, mwanafizikia mbobezi wa Pakistan katika mji wa Punjab mashariki ya nchi hiyo.
Abdussalam, ambaye alizaliwa katika familia ya kidini alianza kudhihirisha mapema kipawa kikubwa alichokuwa nacho kwa kufanikiwa kuingia chuo kikuu cha Punjab akiwa na umri wa miaka 14. Na baada ya kuhitimu shahada ya pili ya Uzamili akiwa na umri wa miaka 20 alielekea chuo kikuu cha Cambridge nchini Uingereza. Baada ya kuhitimu shahada ya kwanza ya Hisabati na Fizikia, mwaka 1951, Abdussalam alihitimu shahada yake ya Uzamivu au PhD ya Fizikia na kutunukiwa tuzo ya Adams.
Mwaka 1979, Profesa Muhammad Abdussalam pamoja na watafiti wengine wawili, alitunikiwa tuzo ya amani ya Nobeli na kuwa mwanasayansi wa kwanza katika Ulimwengu wa Kiislamu kushinda tuzo hiyo. Mwanasayansi huyo aliteuliwa kuwa mshauri wa masuala ya sayansi na elimu wa rais wa Pakistan kuanzia mwaka 1961 hadi 1974. Katika uhai wake, Muhammad Abdussalam alivumbua vitu kadhaa wa kadhaa na aliaga dunia mwaka 1996.