Jumamosi, 08 Machi, 2025
Leo ni Jumamosi 7 ya mwezi mtukufu wa Ramadhani 1446 Hijria mwafaka na 8 Machi 2025 Miladia.
Siku kama ya leo miaka 1436 iliyopita, yaani tarehe 7 Ramadhani mwaka wa 10 baada ya kubaathiwa Mtume, kwa mujibu wa baadhi ya nukuu za historia, Abu Twalib ami ya Mtume Muhammad (SAW) na baba wa Imam Ali (A.S) alifariki dunia.
Abu Twalib alichukua jukumu la kumlea Mtume wetu Muhammad (SAW) akiwa na umri wa miaka minane, baada ya kuaga dunia babu yake, Abdul Muttalib.
Abu Twalib alikuwa mlinzi na msaidizi mkubwa wa Mtume (saw) baada ya mtukufu huyo kupewa Utume, na daima alisimama dhidi ya Washirikina wa Makka waliompiga vita Mtume wa Mwenyezi Mungu.
Kabla ya kuaga dunia, Abu Twalib aliwausia jamaa na marafiki zake kufuata Uislamu na kumtetea Mtume Muhammad (saw).

Siku kama ya leo miaka 128 iliyopita, aliuawa Sayyid Jamaluddin Asadabadi mwanazuoni na mmoja wa viongozi wa mapambano dhidi ya ukoloni wa kimaitaifa dhidi ya Waislamu.
Sayyid Jamaluddin mashuhuri kama Sayyid Jamaluddin al Afghani, alizaliwa huko Asadabad magharibi mwa Iran na kupata elimu katika taaluma za falsafa, nujumu na historia. Mbali na kufahamu lugha za Kiarabu, Kifarsi na Kituruki, Sayyid Jamaluddin Asadabad alikuwa mtaalamu pia katika lugha za Kiingereza, Kifaransa na Kirusi.
Sayyid Jamaluddin Assadabadi alikuwa mmoja wa waanzilishi wa fikra ya umoja wa Kiislamu na mmoja wa wapinzani wakubwa wa ushawishi wa kikoloni katika nchi za Kiislamu. Alifanya jitihada kubwa za kuyaamsha mataifa ya Kiislamu kwa kuchapisha magazeti ya Al Urwatul Wuthqa mjini Paris na Dhiyaul Khafiqin mjini London.
Vilevile alieneza mawazo za kupigania uhuru miongoni mwa watu kwa hotuba zake za hamasa, na kwa sababu hiyo alikabiliwa na uadui na wakoloni na tawala dhalimu.
Miaka 1245 iliyopita katika sioku kama ya leo, Maamun mtawala wa Kabbasi, alimtwisha Imam Ridha (as) urithi wa kiti cha uongozi. Uadui wa koo za Bani Umayya na Bani Abbas dhidi ya Ahlul-Bait ulikuweko tangu kale.
Familia hizi mbili za dhulma na katili lilizifanya suala la kuteswa Ahlul-Bayt wa Mtume kuwa jambo la kawaida, na hazikuepuka hata kumuua shahidi Imam maasumu. Wakati Mamun alipokaliia kiti cha uongozi, alifahamu ushawishi wa Imam Ridha na kukubalika kwake miongoni mwa watu, na kwa sababu alitaka kumuweka chini ya uangalizi Imamu na kujionyesha kuwa ni mtu anayewapenda Ahlul-Bayt ili kuvutia upendeleo wa umma, aliamuru Imam (a.s.) aletwe kutoka Madina hadi Khorasan, na akang'angania amkabidhi Imamu urithji wa kiti cha uongozi.
Kutokana na mazingira yaliyovyokuwa, Imam Ridha aliilazimika kukubali hilo bila ya ridhaa.
Katika siku kama ya leo miaka 935 iliyopita, Ibn Zuhrah, mmoja wa mafakihi watajika na wanateolojia mashuhuri wa karne ya 6 Hijria alizaliwa.
Ibn Zuhrah alikuwa mmoja wa wanazuoni mashuhuri wa Kiislamu wa Halab moja ya miji ya Syria ya leo. Baada ya kukamilisha masomo yake ya msingi katika miji ya Halab na Syria, alifanikiwa kukwea daraja za juu za kielimu.
Mwanazuoni huyu alikuuwa amebobea katika elimu za Fiqh, Usul, teolojiia na fasihi ya lugha ya Kiarabu. Ibn Zuhrah aliaga dunia mwaka 585 Hijria.

Siku kama ya leo miaka 57 iliyopita, inayosadifiana na 8 Machi 1968 ilianza Harakati ya Ukombozi ya Moro dhidi ya utawala wa dikteta Ferdinand Marcos nchini Ufilipino.
Dikteta Marcos alikuwa mshirika na muitifaki mkubwa wa Marekani na katika utawala wake wa kidikteta, maelfu ya Waislamu wa Ufilipino waliuawa au kufungwa jela. Harakati ya Ukombozi ya Moro ilipambana kwa ajili ya kupigania haki za Waislamu, na ilihesabiwa kuwa harakati kubwa zaidi iliyopinga utawala wa Marcos nchini Ufilipino.
Baada ya Marcos kuondoka madarakani mwaka 1986, harakati ya Moro ilikubali kutia saini makubaliano ya amani na serikali ya Manila.

Leo tarehe 8 Machi inatambuliwa kuwa Siku ya Kimataifa ya Mwanamke.
Awali siku hii ilianzishwa kama tukio la kisiasa la kisoshalisti lakini baadaye liliingia katika utamaduni wa nchi nyingi duniani.
Siku ya Kimataifa ya Mwanamke inayoadhimishwa katika nchi nyingi duniani imepoteza sura yake ya kisiasa na sasa limekuwa tukio linalotumiwa na wanaume kudhihirisha upendo wao kwa wanawake. Mwaka 1977 Umoja wa Mataifa iliitangaza rasmi siku hiyo kama Siku ya Haki za Wanawake na Amani ya Kimataifa.
