Alkhamisi, Machi 13, 2025
Leo ni Alkhamisi tarehe 12 Ramadhani mwaka 1446 Hijria inayosadifiana na tarehe 13 Machi 2025.
Siku kama ya leo miaka 1445 iliyopita yaani tarehe 12 Ramadhani mwaka wa Kwanza Hijria, muda mfupi baada ya Mtume Mtukufu Muhammad (SAW) kuhamia Madina akitokea Makka, aliunga udugu baina ya Muhajirina na Ansar.
Muhajirina ni watu ambao walihama na Mtume (SAW) kutoka Makka kwenda Madina na Ansar ni Waislamu wa mjini Madina waliowakaribisha na kuwanusuru Muhajirina katika mji huo.
Kwenye sherehe hiyo ya kuunga udugu wa Waislamu, Mtume (SAW) alimtangaza Ali bin Abi Talib (AS) kuwa ndugu yake hapa duniani na Akhera.

Katika siku kama ya leo yaani mwezi 12 Ramadhani kwa mujibu wa baadhi ya nukuu za historia, ni siku ambayo Nabii Issa Ibn Maryam AS aliteremshiwa kitabu kitukufu cha Injili.
Neno Injili ni la Kigiriki na lina maana ya bishara. Jina hilo limetajwa mara 12 katika Qur’ani Tukufu na kitabu hicho kinaitambua Injili kuwa ni kitabu cha Mwenyezi Mungu SW chenye sheria na kanuni za mbinginu.
Hata hivyo kitabu kinachojulikana hivi sasa kwa jina la Injili si kile kilichoteremshwa kwa Nabii Issa Masih bali ni riwaya na kumbukumbu zilizokusanywa na wanafunzi wake baada ya Yeye kupaa mbinguni.

Tarehe 12 Ramadhani miaka 849 iliyopita, alifariki dunia Ibn Jawzi, faqihi na mtaalamu mkubwa wa hadithi katika karne ya 6 Hijria.
Ibn Jawzi alizaliwa mwaka 510 Hijria na kufanya safari nyingi kwa ajili ya masomo. Mbali na kubobea katika masuala ya elimu ya fiq'hi na hadithi, alikuwa mtaalamu katika uwanja wa kutoa mawaidha na hata akaweza kuaminiwa na maulamaa wakubwa wa zama zake.
Mwanazuoni huyo ameandika vitabu vingi na mashuhuri zaidi ni Al Muntadhim na Mawaidhul Muluk.

Siku kama ya leo miaka 292 iliyopita, yaani 13 Machi, 1733 alizaliwa Joseph Priestley, mkemia na mwanafizikia wa Uingereza. Msomi huyo aliishi katika kipindi kilichokuwa maarufu kama zama za dhahabu za kemia na elimu hiyo ilikuwa imepiga hatua.
Katika uchunguzi na utafiti wake, Priestley alivumbua uvutaji pumzi katika mimea na gesi za oksijeni na haidrojeni. Joseph Priestley alifariki dunia mwaka 1804.

Miaka 77 iliyopita sawa na tarahe 13 Machi 1948, Wazayuni waliokuwa na mfungamano na kundi la kigaidi la Haganah walishambulia kitongoji cha Wapalestina cha Husseiniyah katika eneo la kaskazini mwa Jalilah.
Wazayuni hao licha ya kuwaua shahidi zaidi ya Wapalestina 60, waliharibu nyumba zao kadhaa. Hali kadhalika katika siku hiyo hiyo, wanajeshi wa Israel walizilipua kwa mabomu nyumba za Wapalestina katika eneo la 'Qatmun' lililoko Baitul Muqaddas.
Mauaji ya Waislamu wa Palestina yaliyofanywa na makundi ya kigaidi ya Israel yalitekelezwa kwa lengo la kutaka kutangaza uwepo wa utawala huo bandia kwenye ardhi zinazokaliwa kwa mabavu za Palestina baada ya kuondoka vikosi vya majeshi ya Uingereza katika eneo hilo.
