Mar 28, 2025 02:24 UTC
  • Ijumaa, tarehe 28 Machi, 2025

Leo ni Ijumaa tarehe 27 Ramadhani 1446 Hijria inayosadifiana na tarehe 28 Machi mwaka 2025.

 Miaka 886 iliyopita katika siku sawa na ya leo Abubakar Muhyiddin Muhammad mashuhuri kwa jina la Ibn al Arabi, arif na msomi mkubwa wa Kiislamu alizaliwa huko Andalusia, Uhispania ya leo.

Ibn al Arabi alifanya safari nyingi katika baadhi ya nchi na miji ikiwemo Tunisia, Makka na Baghdad na kila alipofika aliheshimiwa na kukirimiwa. Alikuwa msomi hodari na baadhi ya duru zinasema kuwa ameandika vitabu na risala zaidi ya 500.

Miongoni mwa kazi zake kubwa ni vitabu vya "Tafsir Kabir", "al Futuhatul Makkiyyah" na "Fususul Hikam". 

Siku kama ya leo miaka 336 iliyopita aliaga dunia Allamah Muhammad Baqir Majlisi, mmoja kati ya maulamaa wakubwa wa Kiislamu.

Allamah Majlisi aliandika vitabu vingi wakati wa uhai wake ambavyo hii leo ni marejeo ya Waislamu.

Katika kipindi cha uhai wake Allamah Muhammad Baqir Majlisi alifanya hima kubwa kuhakikisha kuwa Swala za Ijumaa na jamaa zinatekelezwa. Vilevile alifanya juhudi za kuasisi shule za masomo ya kidini na kueneza Hadithi za Mtume wa Uislamu na Ahlul Bait zake watoharifu.

Idadi ya vitabu vilivyoandika na Allamah Muhammad Baqir Majlisi imetajwa kuwa zaidi ya 600 na mashuhuri zaidi ni kile kinachojulikana kwa jina la Biharul Anwar. Vitabu vingine mashuhuri vya msomi huyo ni Hayatul Quluub, Ainul Hayat na Zadul Maad.

Siku kama ya leo miaka 157 iliyopita, alizaliwa mwandishi mashuhuri wa Russia Alexei Maximovich Peshkov aliyekuwa mashuhuri kwa jina la Maksim Gorky.

Gorky alilazimika kusoma na wakati huo huo akifanya kazi ili kuweza kukidhi mahitaji yake ya maisha kutokana na umaskini mkubwa uliokuwa ukimkabili.

Alianza kuandika riwaya haraka sana na kufanikiwa kuchapisha riwaya yake ya kwanza katika gazeti la Tbilisi wakati alipokuwa akifanya kazi katika sekta ya reli.

Miaka miwili baadaye mwandishi Gorky alipata mafanikio makubwa ambapo alichapisha riwaya yake katika kitabu na taratibu akaanza kuingia katika safu ya waandishi wakubwa na mashuhuri duniani. 

Maksim Gorky

Katika siku kama leo miaka 86 iliyopita, baada ya kupita karibu miaka miwili na nusu ya vita vya ndani huko Uhispania, wapigania usultani chini ya uongozi wa Jenerali Francisco Franco waliwashinda wapigania jamhuri na kudhibiti Madrid, mji mkuu wa nchi hiyo.

Machafuko yalianza huko Uhispania wakati Alphonso wa 13 mfalme dikteta wa nchi hiyo alipolazimika kujiuzulu kufuatia mashinikizo ya wapigania jamhuri na baadaye mfumo wa jamhuri ukaasisiwa huko Uhispania. 

Jenerali Francisco Franco

Siku kama ya leo miaka 84 iliyopita mwandishi wa Kiingereza, Bi Virginia Woolf aliaga dunia kwa kujiua.

Woolf alizaliwa mwaka 1882 na alianza kufaidika na maktaba binafsi ya baba yake ambaye alikuwa mwandishi na mkosoaji wa fasihi, akiwa bado mtoto.

Virginia Woolf alianza kuandika vitabu mapema na miongoni mwa vitabu hivyo ni Mrs. Dalloway, The Waves na To the Lighthouse. Hata hivyo maradhi ya kiakili na kinafsi yaliyompata akiwa bado kijana yaliendelea kumuandama na hatimaye mwandishi huyo wa Uingereza aliamua kujiua katika siku kama hii ya leo.

Virginia Woolf