Jumapili, tarehe 6 Aprili, 2025
Leo ni Jumapili tarehe 7 Shawwal 1446 Hijria inayosadifiana na tarehe 6 Aprili 2025.
Siku kama hii ya leo miaka 1443 iliyopita kulipiganwa Vita vya Uhud kando kando ya mlima wenye jina hilo kaskazini mwa mji wa Madina, kati ya Waislamu na Washirikina.
Baada ya washirikina wa Kiquraishi kushindwa vibaya na Waislamu katika Vita vya Badr walianzisha vita hivi vya Uhud kwa kuandaa jeshi la watu 3,000 waliokuwa na zana kamili kwa ajili ya vita hivyo, huku wapiganaji wa Kiislamu wakiwa 700 tu.
Kabla ya kuanza kwa vita hivyo, Mtume Muhammad (s.a.w) aliwashauri masahaba zake juu ya namna atakavyopambana na Maquraishi, na iliamuliwa kuwa vita hivyo vipiganwe nje ya mji wa Madina. Mwanzoni mwa vita hivyo, Waislamu walionekana kushinda, hata hivyo kufuatia kughafilika na baadhi yao kuasi amri ya Mtume (saw) aliyewataka kuendelea kubakia mlimani, Waislamu hao walishuka mlimani kwa tamaa za kupata ngawira, hali iliyowafanya washirikina kuwashambulia Waislamu na kudhoofika nguvu na uwezo wao. Waislamu 70 waliuawa shahidi katika vita hivyo akiwemo Hamza, ami yake Mtume (s.a.w). Hata hivyo washirikina hawakuweza kupata ushindi wa moja kwa moja na hivyo walilazimika kurejea Makka. **
Siku kama ya leo miaka 445 iliyopita, ardhi ya Ureno, moja kati ya nchi zilizokuwa na nguvu barani Ulaya katika karne za 15 na 16, iliunganishwa na Uhispania.
Ureno ilikuwa mpinzani wa kisiasa na kikoloni wa Uhispania huko Asia, Afrika na Marekani. Hata hivyo kutokana na raia wa nchi hiyo kuhamia kwa wingi katika nchi makoloni ya Ureno na vile vile hali mbaya ya kiuchumi taratibu Ureno ilianza kupoteza satwa na nguvu yake ya kisasa.
Udhaifu na kutokuwa na nguvu Ureno uliipelekea Uhispania kuivamia nchi hiyo. Pamoja na hayo yote hatimaye mapambano ya ukombozi ya wananchi wa Ureno ya mwaka 1640 yalipelekea kukombolewa tena nchi hiyo. ****
Miaka 108 iliyopita katika siku kama ya leo, serikali ya Marekani ilitangaza vita dhidi ya Ujerumani na ikaingia katika Vita vya Kwanza vya Dunia kwa maslahi ya Waitifaki. Tab'an kabla ya hatua hiyo, Marekani ilikuwa imekata uhusiano wake wa kisiasa na Ujerumani na ilikuwa ikizisaidia nchi Waitifaki. ****
Miaka 40 iliyopita katika siku kama hii ya leo Ja'far Nimeiry, Rais wa zamani wa Sudan alipinduliwa na Jenerali Abdulrahman Swarul Dhahab aliyekuwa Waziri wa Ulinzi ambaye alichukua madaraka ya kuiongoza Sudan.
Ni vyema kuashiria hapa kuwa Nimeiry pia aliingia madarakani kufuatia mapinduzi ya kijeshi yaliyotokea Sudan mwaka 1969.
Nimeiry aliongoza Sudan kimabavu kwa miaka 16 na kuanzisha uhusiano mkubwa kati ya nchi hiyo na Marekani. ***
Na katika siku kama ya leo miaka 31 liyopita, Wahutu wenye misimamo mikali wa Rwanda walianzisha mauaji makubwa dhidi ya Watutsi.
Katika mauaji hayo Wahutu wenye misimamo mikali waliwauwa raia wa Kitutsi na Wahutu wenye misimamo ya wastani karibu milioni moja na kuwafanya mamilioni ya wengine kuwa wakimbizi. Wahutu wanaunda asilimia 84 ya jamii ya Rwanda na kabila hilo lilikuwa madarakani hadi mwaka 1994. ***