Jumatatu tarehe 7 Aprili 2025
Leo ni Ijumatatu 8 Shawwal mwaka 1446 Hijria inayosadifiana na tarehe 7 Aprili 2025.
Miaka 304 iliyopita, mnamo tarehe 7 Aprili 1721, Mfalme wa Urusi Peter the Great aliishambulia kijeshi Sweden.
Kuanzia mwaka 1700, Urusi na Sweden pamoja na Poland na Denmark, zilitumbukia kwenye vita vya kaskazini. Wakati jeshi la Urusi lilipoivamia Sweden, nchi hiyo ilikuwa imefanya suluhu na nchi zingine ilizokuwa ikipigana nazo na ikawa imepanga kufanya suluhu na Urusi pia; lakini Peter the Great, ambaye alitaka kujipanulia maeneo ya ardhi, alilishambulia na kulishinda jeshi la Sweden kwa jeshi lake lililojiandaa kwa vita na kujizatiti kwa silaha na kuilazimisha nchi hiyo kusaini mkataba wa suluhu ilioutaka.
Kwa mujibu wa mkataba huo, maeneo kadhaa ya ardhi ya Sweden pamoja na Finland, iliyokuwa inakaliwa na nchi hiyo, yakakabidhiwa kwa Urusi. Kwa njia hiyo, nguvu za Sweden zikapungua sana na mkabala wake, Urusi ikageuka kuwa dola lenye nguvu kubwa barani Ulaya. ****

Miaka 136 iliyopita mnamo Aprili 7, 1889, Bi Gabriela Mistral, mshairi na mwandishi mashuhuri wa Amerika ya Kusini, alizaliwa nchini Chile.
Katika athari zake, mshairi huyo wa Amerika ya Latini, ameienzi na kuitukuza hadhi ya mama pamoja na hisia zake za upendo. Gabriela Mistral alikuwa mshairi wa kwanza wa Amerika ya Kusini kutunukiwa Tuzo ya Nobel ya Fasihi mnamo mwaka 1945. Amechapisha kazi zake muhimu zaidi katika majimui yenye anuani ya Gabriela.
Mwandishi na mshairi huyo maarufu wa Chile aliaga dunia mwaka 1957. ****

Miaka 122 iliyopita katika siku kama ya leo ya tarehe 8 Shawwal mwaka 1324 Hijria toleo la kwanza la gazeti la 'Majlis' lilichapishwa nchini Iran. Gazeti hilo lilianzishwa na mtu aliyejulikana kwa jina la Mirza Sayyid Muhammad Sadiq Tabatabai.
Mbali na gazeti hilo kuandika habari za ndani na nje ya nchi, liliakisi pia mijadala yote ya Majlisi ya Ushauri ya Iran yaani Bunge. ***

Miaka 103 iliyopita, tarehe 7 Aprili 1922, alizaliwa Annemarie Schimmel, mtaalamu wa Kijerumani wa masuala ya Uislamu.
Alipenda sana kujifunza kuhusu Ustaarabu wa Kiislamu; na akiwa na umri wa miaka 19, Schimmel alipata shahada yake ya Uzamivu (Phd) ya Taaluma za Kiislamu katika Chuo Kikuu cha Berlin.
Kwa miaka mingi, Bi Schimmel alifundisha Historia ya Dini na I'rfani ya Kiislamu katika vyuo vikuu vya Ujerumani, Marekani na Uturuki. Mbali na Kijerumani na Kiingereza, alijifunza pia lugha za Kiarabu, Kifarsi, Kituruki, Kiurdu na Kibengali ili kuwa na uelewa mkubwa zaidi wa masuala ya Kiislamu.
Mtaalamu huyu wa Kijerumani wa masuala ya Uislamu alikuwa na shauku maalumu ya I'rfani ya Kiislamu na shakhsia wa elimu hiyo kama Hafez na Molavi, ambao ni miongoni mwa malenga na wanairfani wakubwa wa Kiirani.
Profesa Schimel ametunukiwa tuzo nyingi na shahada za heshima. Amealifu vitabu kadhaa vikiwemo Muhammad SAW Mtume wa Allah, Mwanamke Katika I'rfani na Tas'awuf ya Kiislamu (Women in Islamic Mysticism and Sufism), Jalaluddin Rumi na Ghazali za Ulimwengu wa Mashariki (Oriental Ghazliat). Bi Shimmel alifariki dunia mwaka 2003.

Siku kama ya leo miaka 102 iliyopita, Mawahabi wa Saudi Arabia walibomoa makaburi ya Ahlul Bait wa Mtume (s.a.w) ambayo yako Baqii, katika mji mtakatifu wa Madina.
Baada ya Muhammad Ibn Saud kutawala tena maeneo ya Hijaz, likiwemo eneo la Madina, sheikh Abdullah bin Bulaihad aliyekuwa mkuu wa makadhi wa Kiwahabi, alitoa fatwa ya kuhalalisha kuharibiwa makaburi matukufu na ya kihistoria ya mjini Madina.
Mawahabi walikusanya watu kwa nguvu na kuwalazimisha kwenda katika makaburi hayo ya Baqii na kuanza kubomoa na kuharibu kila kitu kilichokuwa juu ya makaburi ya mji wa Madina na nje ya mji huo.
Miongoni mwa makaburi yaliyobomolewa na kuharibiwa vibaya ni makaburi manne ya maimamu na wajukuu wa Mtume (s.a.w), kaburi la Abdullah, baba mzazi wa mtukufu Mtume (s.a.w), kaburi la Ibrahim mtoto wa kiume wa Mtume (s.a.w), makaburi ya wake wa Mtume na makaburi ya Ummul Banin mke mwema wa Imam Ali bin Abi Twalib na ya masahaba wa Mtume (saw).
Kaburi pekee lililobakishwa na Mawahabi hao wenye mioyo ya kikatili ni la Mtume Muhammad (s.a.w), kwani walijua kuwa kubomoa kaburi la mtukufu huyo kungezua hasira kali ya Waislamu duniani.

Na miaka 78 iliyopita katika siku kama ya leo, yaani Aprili 7, 1947, Henry Ford, mvumbuzi na mwanasayansi wa Marekani, alifariki akiwa na umri wa miaka 84.
Alizaliwa mwaka 1863 katika familia maskini huko Greenfield, Marekani. Ford alijishughulisha na utengenezaji wa saa akiwa mtoto na umekanika akiwa kijana, lakini kufikia wakati wa kifo chake, alikuwa ameunda himaya na mtandao mkubwa katika sekta ya uundaji magari.
Ford anahesabiwa pia kuwa mmoja wa wavumbuzi wa magari. ***
