Alkhamisi 04 Agosti, 2016
Leo ni Alkhamisi tarehe Mosi Dhulqaada 1437 Hijria sawa na Agosti 4, 2016.
Siku kama ya leo miaka 1264 iliyopita, kwa mujibu wa baadhi ya mapokezi, alizaliwa Bibi Fatima Maasuma, binti yake Imam Musa al-Kadhim (as) ambaye ni miongoni mwa wajukuu watukufu wa Bwana Mtume (SAW). Fatima Maasuma (as) alikuwa hatibu hodari, mwalimu mahiri, zahidi na mcha-Mungu mkubwa. Alipatwa na maradhi alipokuwa njiani kuelekea Khorasan huko kaskazini mashariki mwa Iran kwa ajili ya kumtembelea kaka yake yaani Imam Ali bin Musa al Ridha (as) na akafariki dunia katika mji mtakatifu wa Qum baada ya kukaa hapo kwa siku 17. Leo hii ziara la mtukufu huyo linatembelewa na mamilioni ya waumini kila mwaka kutoka pembe mbalimbali za dunia.
Katika siku kama ya leo miaka 141 iliyopita, alifariki dunia, Hans Christian Andersen malenga, mwandishi na msimulizi wa visa maarufu vya watoto. Andersen ambaye alikuwa mtoto wa bwana mmoja maskini na fundi viatu, alihamia Copenhagen mji mkuu wa Denmark na kuanza kucheza michezo ya kuigiza. Baada ya muda, Hans Andersen alianza kutunga visa na kuwa mashuhuri baada ya kuandika kitabu chake cha kwanza cha hadithi alichokipa jina la "Fairy Tales, Told for Children" mnamo mwaka 1838 Miladia.
Siku kama ya leo miaka 52 iliyopita Marekani ilishindwa katika vita vya baharini vilivyozishirikisha meli za kivita za Marekani na Vietnam ya Kaskazini katika Ghuba ya Tonkin inayopatikana kwenye bahari ya China ya Kusini. Mivutano hiyo ya kijeshi iliipa Marekani kisingizio cha kuingia vitani moja kwa moja na Vietnam ya Kaskazini. Wakati huo Washington ilikuwa ikiiunga mkono kwa pande zote Vietnam ya Kusini dhidi ya ile ya Kaskazini. Baada ya kushindwa katika vita hivyo, serikali ya wakati huo ya Washington iliongeza idadi ya askari wake huko Vietnam ya Kusini na kisha kufanya mashambulio makubwa ya anga na ardhini dhidi ya wananchi wa Vietnam ya Kaskazini. Hata hivyo mashambulio hayo yalikabiliwa na upinzani mkubwa wa wananchi wa nchi hiyo.
Siku kama ya leo miaka 28 iliyopita inayosadifiana na tarehe 24 Mordad 1367 Hijria Shamsia, aliuawa shahidi Allamah Sayyid A'ref Hussein Husseini, mwanachuo mashuhuri na mwanamapambano wa Pakistan katika mji wa Peshawar, kaskazini mwa nchi hiyo. Sayyid A'ref Husseini licha ya kupata elimu ya kidini nchini Pakistan, alifunga safari na kuelekea katika nchi za Iraq na Iran kwa shabaha ya kuongeza maarifa ya kidini. Wakati wa kutokea harakati za mapinduzi ya Kiislamu dhidi ya utawala wa Shah, Allamah A'ref Husseini alikuwa hapa nchini na kuwa bega kwa bega na wananchi wa Iran dhidi ya utawala wa Shah, jambo ambalo liliukasirisha utawala wa Shah na kuamua kumfukuza nchini.
Miaka 224 iliyopita alizaliwa Percy Bysshe Shelley malenga wa Uingereza. Percy alianza kuvutiwa na fasihi tangu utotoni na kuonyesha kipawa kikubwa katika uwanja huo. Aidha Percy Bysshe alikuwa mfuasi na muungaji mkono wa thamani za upendo, urafiki na uhuru suala lililomfanya avutiwe na mapinduzi ya Ufaransa ambayo ndio kwanza yalikuwa yametokea.
Percy Bysshe Shelley aliaga dunia mwaka 1822 akiwa na umri wa miaka 30 baada ya boti yake kuzama katika Bahari ya Mediterrania. Percy ameacha vitabu kadhaa hasa katika uwanja wa mashairi.