Hadithi ya Uongofu (48)
Ni matumaini yangu kuwa hamjambo wapenzi wasikilizaji popote pale yanapokufikieni matangazo haya ya Idhaa ya Kiswahili ya Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Tunakutana tena katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu. Katika kipindi kilichopita tulizungumzia athari za utunzaji amana kimaanawi na kimaada pamoja na faida anazopata mtunzaji wa amana hapa duniani na kesho akhera. Tulisema katika kipindi hicho kwamba, utunzaji amana ni miongoni mwa sifa njema za kiakhlaqi na kimaadili ambazo zina faida na athari nyingi ambazo zimetajwa katika hadithi na mafundisho matukufu ya Kiislamu. Kipindi chetu cha wiki hii ambacho ni sehemu ya 48 ya mfululizo huu kitazungumzia uadilifu na kukunukulieni hadithi zinazozungumzia maudhui hii. Ni matumaini yangu kuwa mtakuwa name hadi mwisho wa kipindi.
Uadilifu ni jambo la kifitra na kimaumbile ambalo liko katika ujudi wa wanadamu wote. Dini Tukufu ya Kiislamu ikiwa ndio dini ya mwisho ya Mwenyezi Mungu na njia ya wokozi wa mwanadamu imetilia mkazo mno suala la kufanya uadilifu na ikalibainisha na kulieleza hilo katika engo tofauti.
Al-adl yaani uadilifu katika maana na fasili ya kilugha kama inavyoelezwa katika kamusi ya Kiarabu ya Mu'jam al-Wasit ni insafu na kumpatia kila mtu kile anachostahiki na kuchukua kila ambacho ni lazima kuchukua kutoka kwake.
Imam Ali bin Abi Twalib AS ambaye yeye mwenyewe ni shahidi katika njia ya uadilifu yaani aliuawa shahidi katika njia ya kutekeleza uadilifu anasema kuwa, uadilifu maana yake ni kuweka kila kitu mahala pake na kuwa na insafu na kuwa na hali ya katikati na kujiepusha na Ifrati na Tafriti. Imam Ali AS anasema katika hekima ya 437 kwenye Kitabu cha Nahaj al-Balagha kwamba:
"Uadilifu unaweka kila kitu katika mkondo wake wa kawaida." Kwa mujibu wa aya za Qur'ani Tukufu ni kwamba, fitra na maumbile ya wanadamu wote yamejengeka katika msingi wa uadilifu. Katika kivuli cha uadilifu kila mtu huweza kupata haki, na dhulma na ukandamizaji huondoka na natija yake ni kupatikana amani na utulivu kwa watu wote. Ni kwa kuzingatia ukweli huo ndio maana watu wanakataa na kulaumu dhulma na ukandamizaji na badala yake wanasifia uadilifu na insafu. Ni kwa muktadha huo ndio maana madhalimu na wakandamizaji wanafanya hili na lile kuhalalisha dhulma zao na kufanya bidii ya kuonesha kwamba, wana uadifu. Hili ni jambo linaloweka wazi kwamba, dhulma ni jambo lisilopendwa na mtu yeyote na wakati huo huo uadilifu unapendwa; na haya ni mambo ambayo yako katika fitra na maumbile ya mwanadamu. Kwa maana kwamba, pindi mtu anapokudhulumu utachukia na kukasirika na anapokufanyia uadilifu unafurahi na kumpenda.
Imam Ja'far Swadiq AS anabainisha kwamba, dhulma ni jambo baya na lisilipendeza na ilihali uadilifu ni jambo linalopendwa na kufurahiwa na wote. Imam huyo wa sita katika mlolongo wa Maimamu 12 kutoka katika kizazi cha Mtukufu Mtume SAW anasema: Uadilifu ni mtamu kuliko asali, ni mlaini kuliko ardhi na ni wenye harufu nzuri kuliko miski na manukato.
Kwa msingi huo basi kama ambavyo asali ni tamu mno kwa watu wote na harufu ya miski na manukato inavutia na kuwapendeza watu wote, vivyo hivyo uadilifu nao kwa mujibu wa maumbile na fitra ya mwanadamu ni jambo linalopendwa na wanadamu wote.
Uadilifu ni moja ya mafundisho muhimu mno ya Kiislamu ambayo mbali na kuleta hali ya uwiano katika jamii, huifanya jamii husika ifikie katika usalama na utulivu. Ukamilifu wote na mambo mazuri yawe ni ya kimaada au kimaanawi ni natija ya uadilifu ambao nao ni matokeo ya kuweko uwiano na ufanyaji mambo wa kati na kati. Mambo yote mabaya na mapungufu ni sababu ya kutokuweko uwiano na mlingano na badala yake kutawala hali ya ifrati na tafriti katika mambo baina ya wanajamii.
Imam Ali bin Abi Twalib AS anasema kuwa: Mwenyezi Mungu ameujaalia uadilifu kuwa wenzo mwepesi na ufunguzi kwa ajili ya watu. Aidha imenukuliwa hadithi kutoka kwa Bwana Mtume SAW ya kwamba amesema:
Mbingu na ardhi zinasimama na kuweko kutokana na uadilifu.
Ukweli wa mambo ni kuwa, kuweko na kubakia kwa ulimwengu wote na vilivyomo ambayo vinafungamana na uwepo wa uwiano na mlingano baina ya vitu vinavyounda hivyo, ni vitu hivyo kuwa katika mahala pake maalumu. Yaani kila kitu kuweko mahala pake.
Moja ya yaliyokuwa malengo muhimu ya kutumwa na kubaathiwa Mitume wa Mwenyezi Mungu ni kutekelezwa uadilifu baina ya watu. Katika aya na hadithi nyingi nukta hii imeashiria na kubainishwa. Miongoni mwa aya zilizoashiria hilo ni ile ya 25 ya Surat al-Hadid inayosema:
Kwa hakika tuliwatuma Mitume wetu kwa dalili waziwazi, na tukateremsha Kitabu pamoja nao na Mizani, ili watu wasimamie uadilifu…
Katika aya hiyo lengo la kutumwa Mitume limebainishwa ambalo ni kuhakikisha kwamba, watu wanasimamia uadilifu yaani uadilifu unakuweko katika jamii ambapo jambo hili hutumia kwa kuundwa serikali na kutekelezwa sheria za dini.
Imam Ali bin Abi Twalib AS aliasisi na kuunda utawala wake kwa misingi ya kusimamia uadilifu na usawa na kuchungwa mipaka ya Mwenyezi Mungu. Ni kwa kuzingatia ukweli huo ndio maana wakati Imam Ali bin Abi Twalib AS aliposhika hatamu za utawala na kutekeleza uadilifdu na kisha watu kuanza kumuandama kwamba, kwa nini hawapatii zaidi na kuliko watu wengine kutoka katika hazina ya dola watu ambao ni wa mwanzo zaidi katika Uislamu, walioshiriki zaidi katika vita au watu ambao nasaba zao ni mashuhuri, Imam Ali bin Abi Twalib AS alisema: Hapana, ninaapa kwa Mola, madhali dahari na dunia ipo siwezi kukaribia kufanya kitendo kama hicho. Hata kama mali hii ingekuwa yangu basi ningeigawa kwa uadilifu na usawa baina ya watu, seuze mali hii ni ya Mwenyezi Mungu.
Neno na lafudhi uadilifu ni neno zuri zaidi, lenye kupendwa zaidi na lenye thamani zaidi kutamkwa na ndimi za watu. Hii ni kutokana na kuwa, hakuna mafuhumu kubwa zaidi na yenye umuhimu zaidi ya maana na mafuhumu ya uadilifu.
Mtume SAW anasema kuhusiana umuhimu wa uadilifu kwamba:
Saa moja ya uadilifu ni bora kuliko miaka sabini ya ibada ambapo nyakati za mchana mtu anafunga Saumu na usiku anakesha akifanya ibada.
Kwa msingi huo uadilifu na kuchunga mipaka ya uwiano na mlingano katika mambo yote ni jambo ambalo linapaswa kuzingatiwa. Imepokewa hadithi kuhusiana na sira na mwenendo wa Mtume SAW ambaye yeye mwenyewe alikuwa dhihirisho la uadilifu na kiigezo chema kwa Waislamu wote kuhusiana na kutekeleza uadilifu kwamba, mbora huyo wa viumbe hata alipokuwa akizungumza na watu basi alikuwa akilizingatia suala la uadilifu hata katika kuwaangalia. Yaani alikuwa akiwatazama kwa usawa.
Wapenzi wasikilizaji muda wa kipindi chetu kwa juma hili umefikia tamati, tukutane tena wiki ijayo katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu.
Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh…