Ijumaa, Mei 23, 2025
Leo ni Ijumaa tarehe 25 Mfunguo Pili Dhulqaada 1446 Hijria sawa na Mei 23 mwaka 2025 Milaadia.
Siku kama ya leo miaka 1436 iliyopita Nabii Muhammad (saw) aliondoka Madina akiwa na masahaba na Waislamu zaidi ya laki moja na kuelekea Makka kwa ajili ya kutufu nyumba tukufu ya Mwenyezi Mungu, al Kaaba.
Tangu alipohamia Madina Mtume (saw) alielekea Makka mara tatu kutufu al Kaaba lakini alifanikiwa mara mbili tu kutekeleza ibada ya Hija. Katika safari yake ya mwisho ya Hija, Mtukufu huyo aliwafunza Waislamu namna ya kutekeleza ibada ya Hija kwa njia sahihi.
Baada ya kukamilisha ibada hiyo, Mtume Muhammad (saw) alirejea Madina na alipofika katika eneo la Ghadir Khum aliwakusanya masahaba zake, na kwa amri ya Mola wake alimtangaza Imam Ali bin Abi Twalib kuwa Khalifa na Kiongozi wa Umma wa Kiislamu baada yake. Hiyo ilikuwa safari ya mwisho ya Hija ya Mtume ambayo ni maarufu kwa jina la Hajjatul Widaa. Miezi kadhaa baada ya safari hiyo Mtume Muhammad (saw) aliaga dunia na kurejea kwa Mola wake.

Katika siku kama ya leo miaka 407 iliyopita, sawa na 23 Mei 1618, kulianza vita vya kidini barani Ulaya vilivyoendelea kwa muda wa miaka 30. Katika vita hivyo, nchi za Ufaransa, Sweden na Denmark zilikuwa zikiwaunga mkono Waprotestanti, huku Uhispania na Ufalme wa Rome zikiwaunga mkono Wakatoliki. Vita hivyo vilifikia tamati mwaka 1648 baada ya kutiwa saini Mkataba wa Westaphalia. ****
Miaka 119 iliyopita katika siku kama ya leo, aliaga dunia Henrik Ibsen mwandishi wa tamthiliya wa nchini Norway. Alizaliwa mwaka 1828 na shauku na mapenzi ya Ibsen ya kuwa mwandishi wa tamthiliya ndiyo yaliyomsukuma kwenye taaluma hiyo. Mwandishi huyo wa Kinorway ameandika drama na tamthiliya nyingi. Moja kati ya tamthmliya zake mashuhuri ni ile iitwayo, An Enemy of the People yaani Adui wa Watu.

Miaka 110 iliyopita katika siku kama ya leo, Italia ilijiingiza katika Vita vya Kwanza vya Dunia.
Kuingia Italia katika Vita vya Kwanza vya Dunia kulianza wakati nchi hiyo ilipoivamia Austria bila ya sababu yoyote isipokuwa tu kwa tamaa ya kujinufaisha kisiasa na kupanua utawala wake. Muda mchache baadaye, serikali ya Italia ilitangaza vita dhidi ya ufalme wa Othmania na hivyo kuufanya moto wa vita uwake kwa ukali zaidi.
Hata hivyo, licha ya kupata ushindi kundi la nchi Waitifaki, Italia ikiwa moja yao, lakini nchi hiyo haikufaidika kivyovyote na vita hivyo. Matunda pekee iliyopata ni kuwaulisha raia wa Italia baada ya kuwaingia Waitaliano milioni tano na nusu katika vita hivyo. Kwa maneno mengine ni kuwa, maamuzi na siasa za Italia katika Vita vya Kwanza vya Dunia zilifeli, kwani haikupata matunda yoyote ya maana kwa kujiingiza kwake kwenye vita hivyo.

Siku ya leo miaka 35 iliyopita tarehe Pili Khordadi mwaka 1370 Hijria Shamsia Waislamu duniani walilalamikia vikali hatua ya utawala wa chama cha Baath cha Iraq ambao ulivunjia heshima maeneo matakatifu ya Kiislamu nchini humo.
Baada ya wananchi Waislamu wa Iraq kuanzisha harakati ya kupinga jinai nyingi za utawala wa Baath, Saddam Hussein dikteta wa wakati huo Iraq, alitoa amri ya kuuawa bila huruma wananchi na kuhujumiwa maeneo matakatifu ya Kiislamu nchini humo. Kitendo hicho cha utawala wa Baath kiliibua hasira za Waislamu hasa wa madhehebu ya Shia ambao walifanya maandamano kupinga jinai hizo.
Jinai hizo zilitendeka ukiwa umesalia muda mfupo kabla ya wananchi wa Iraq kupata ushindi dhidi ya Saddam. Katika kipindi hicho, Marekani na waitifaki wake walimsaidia Saddam kuua na kuwakandamiza wananchi. Hata baada ya wananchi kukimbilia hifadhi katika maeneo matakatifu, Jeshi la Saddam liliwahujumu wakiwa katika maeneo hayo.
Baada ya kupinduliwa utawala wa Saddam, kulipatikana makaburi mengi ya umati yaliyoweka wazi kiwango cha jinai zilizofanywa Saddam dhidi ya watu wa Iraq.
