Jumatano, tarehe Pili Julai, 2025
Leo ni Jumatano tarehe 6 Muharram 1447 Hijria sawa na Julai Pili mwaka 2025.
Tarehe sita Muharram mwaka 61 Hijria yaani miaka 1384 iliyopita katika siku kama hii ya leo mjukuu wa Mtume Muhammad (saw), Imam Hussein bin Ali bin Abi Twalib (as) aliyekuwa Karbala alimwandikia barua fupi lakini muhimu sana ndugu yake, Muhammad bin Hanafiyya na wafuasi wake kadhaa waliokuwa Madina.
Barua hiyo ilisema: "Kwa jina la Allah, Mwingi wa rehma Mwenye kurehemu. Hakika anayejiunga nami atapata daraja ya kuuawa shahidi, na ambaye hatajiunga nami hatapata ushindi."
Barua hii ilikuwa na ujumbe kadhaa, miongoni mwa ujumbe hizo ni kwamba, Imam Hussein alikuwa akijua kuwa, atauawa shahidi yeye na masahaba wake katika mapambano yake na mtawala dhalimu, Yazid bin Muawiya. Pili ni kwamba aliweka wazi hatima ya wale wote watakaofuatana naye katika mapambano ya Karbala na kwamba wote watauawa, na hivyo mtu yeyote mwenye malengo tofauti bora arejee Madina.

Siku kama ya leo miaka 1386 iliyopita, Habib Bin Madhahir, mmoja wa masahaba wa Mtume Muhammad (saw) na mfuasi wa kweli wa Imam Hussein (as), aliwalingania watu wa kabila la Bani Asad kwa ajili ya kwenda kumsaidia mjukuu huyo wa Nabii wa Allah.
Katika siku hiyo, sahaba huyo wa Mtume aliomba idhini kwa Imam Hussein (as) kwa kusema: “Ewe mjukuu wa Mtume, katika maeneo haya jirani wanaishi watu wa kabila la Bani Asad, ikiwa utaniruhusu nitaenda kwao nikawalinganie, huenda Mwenyezi Mungu akakuokoa kutokana na shari ya watu hawa makatili kupitia uwepo wa watu wa kabila la Bani Asad.”
Imam Hussein alimruhusu Habib Bin Madhahir ambaye alitoka majira ya usiku kwenda kwa watu wa kabila hilo akiwataka wamsaidie mjukuu huyo wa Mtume. Akiwa katika linganio hilo, sahaba huyo wa Mtume alisema: “Kwa kuwa nyinyi ni watu wa ukoo na kabila langu, ninakulinganieni kufuata njia hii, leo ninakuombeni msikie usia wangu na mfanye haraka kwenda kumsaidia Imam Hussein (as) ili mpate utukufu wa dunia na Akhera.”
Kutokana na wito huo, watu wachache kutoka kabila hilo wanaokadiriwa kufikia 90 walisimama na kwenda kumsaidia mjukuu huyo wa Nabii wa Allah. Hata hivyo baadaye walitoroka na kurejea makwao baada ya kufahamu kwamba jeshi la Omar Bin Sa’ad lilifahamu nia yao, hivyo walihofia kuuawa na jeshi hilo. Baada ya Imam Hussein kusikia habari hiyo, alisema: “Laa haula walaa quwwatan illa Billah.”

Siku kama ya leo miaka 1041 iliyopita inayosadifiana na tarehe 6 Muharram mwaka 406 Hijria, alifariki dunia Sayyid Muhammad Hussein Musawi Baghdadi, msomi mashuhuri, mwanafikra na mshairi wa Kiislamu.
Aalim huyo pia alijulikana kwa jina la Sayyid Radhi. Alipata elimu za wakati huo katika kipindi cha ujana wake akiwa pamoja na ndugu yake, Sayyid Murtadha, ambaye pia alikuwa msomi mtajika. Sayyid Radhi aliinukia kuwa msomi mkubwa katika taaluma za fiqhi, tafsiri ya Qur'ani Tukufu na elimu nyingine za Kiislamu.
Msomi huyo alikuwa wa kwanza kuasisi chuo kikuu kwa mtindo wa kisasa na ameandika zaidi ya vitabu 20 katika taaluma za fiqhi, tafsiri ya Qur'ani, historia na fasihi ya Kiarabu. Kitabu mashuhuri zaidi cha mwanazuoni huyo ni Nahjul Balagha ambacho kinakusanya semi, hotuba, amri, barua na mawaidha ya Amirul Muuminin Ali bin Abi Twalib (as).

Siku kama ya leo miaka 136 iliyopita mfumo wa kisultani ulifutwa huko Brazil katika mapinduzi ambayo hayakuwa na umwagaji wa damu na badala yake ukaasisiwa mfumo wa jamhuri.
Mfalme wa mwisho wa Brazil alikuwa Pedro II ambaye alifanya jitihada za kufanya mabadiliko nchini humo. Hatua za mfalme huyo hususan ile ya kuondoa biashara ya utumwa mwaka 1888, iliwakasirisha wamiliki wa ardhi waliokuwa wakiunga mkono mfumo wake wa kisultani.
Pedro II alienguliwa madarakani bila ya mapambano yoyote na mfumo wa jamhuri ukaasisiwa nchini Brazil. ***
Miaka 100 iliyopita katika siku kama hii ya leo alizaliwa Patrice Lumumba mhandisi wa uhuru wa Kongo.
Lumumba alitoa mchango mkubwa katika juhudi za kukombolewa Kongo wakati wa harakati za ukombozi wa nchi za Kiafrika. Lumumba aliteuliwa kuwa Waziri Mkuu na Waziri wa Ulinzi baada ya kuundwa Jamhuri ya Kongo mwaka 1960. Patrice Lumumba aliuawa mwaka 1961 na vibaraka wa Marekani na Ubelgiji baada ya kuvumilia mateso na unyama mkubwa.
Lumumba aliandika vitabu kadhaa wakati wa uhai wake na mashuhuri zaidi ni kile alichokita "Kongo, Nchi Yangu."

Tarehe Pili Julai miaka 64 iliyopita aliaga dunia mwandishi mtajika wa Kimarekani kwa jina la Ernest Hemingway.
Alizaliwa mwaka 1899 na kwa muda fulani alijishughulisha na uandishi huko Uingereza na Ufaransa. Hemingway alianzisha mbinu ya kuandika riwaya na tungo fupi fupi na alikuwa akitumia lugha nyepesi na inayoeleweka. Mwaka 1954 mwandishi Ernest Hemingway alitunukukiwa tuzo ya Nobel katika medani ya fasihi.
Miongoni mwa vitabu maarufu vya Hemingway ni "The Old Man and The Sea", "A Farewell to Arms" na For Whom The Bell Tolls". ***