Leo ni Jumatano Julai 30, 2025
Leo ni Jumatano tarehe 5 Safar 1447 Hijria sawa na Julai 30 mwaka 2025.
Tarehe 8 mwezi Mordad kwa mwaka wa Kiirani wa Hijria Shamsia ni siku ya kumuenzi mwanafalsafa, arifu na msomi mkubwa wa Kiislamu Shahabuddin Sohravardi aliyepewa lakabu ya Sheikhul Ishraq.
Sheikhul Ishraq alizaliwa mwaka 549 Hijria karibu na mji wa Zanjan kaskazini magharibi mwa Iran. Alibobea haraka katika taaluma nyingi za Kiislamu za wakati huo hususan falsafa.
Sheikh Sohravardi alifanya safari katika miji mbalimbali ya nchi za Kiislamu kwa ajili ya kutafuta elimu. Aliasisi mfumo mpya wa falsafa uliopewa jina la Ishraq. Sheikhul Ishraq ameandika vitabu vingi kama vile "Hikmatul Ishraq", al Mabda wal Maad", na "Talwihat".

Siku kama ya leo miaka 127 iliyopita, alifariki dunia Otto von Bismarck, Kansela wa kwanza na mwanasiasa mkongwe wa Ujerumani.
Bismarck aliongoza vita vitatu ambavyo viliainisha mustakbali wa Ujerumani kama nchi huku akikabiliana pia na madola ya Ulaya wakati huo.
Bismarck alikuwa rais wa Prussia akiwa na umri wa miaka 28 na kwa mara ya kwanza akawa pia Kansela wa Ujerumani. Mwaka 1862 aliteuliwa kuwa waziri mkuu wa Prussia na kuanzisha mpango wa Ujerumani moja.
Ili kufikia lengo hilo hakuwa na njia nyingine ghairi ya kuiondoa Austria katika shirikisho la majimbo ya Ujerumani ya Kikatoliki sambamba na kulikomboa jimbo la Schleswig-Holstein kutoka udhibiti wa Denmark na kuhitimisha upenyaji wa Ufaransa katika majimbo ya kusini mwa Ujerumani.
Baada ya kujiimarisha kijeshi alipigana vita vitatu na kufikia malengo yake katika vita vyote hivyo. Kwa mujibu wa historia, Otto von Bismarck alizishinda nchi za Denmark, Austria na Ufaransa, kulikoenda sambamba na kuteuliwa kuwa kansela wa Ujerumani mwaka 1890.

Tarehe 30 Julai miaka 78 iliyopita alifariki dunia Henry Ford, mvumbuzi wa Kimarekani anayejulikana kama baba wa sekta ya utengenezaji magari wa nchi hiyo.
Alizaliwa tarehe 30 Julai 1863 katika familia ya kimaskini na tangu utotoni alikuwa na hamu kubwa ya masuala ya mekaniki. Siku moja Ford aliona gari likitembea barabarani bila ya kuvutwa na farisi na akaamua kutengeneza gari lake mwenyewe.
Henry Ford alifanyia majaribio mkokoteni wa kwanza usiotumia farasi akiwa na umri wa miaka 12 tu. Mvumbuzi huyo aliboresha zaidi mkokoteni huo na mwaka 1896 alifanikiwa kutengeneza gari lake la kwanza. Mwaka 1895 alipewa haki ya kutengeneza magari licha ya kwamba watu wengine pia walikuwa wanatengeneza chombo hicho na mwaka 1903 aliasisi kampuni ya magari ya Ford Motor.
Ford aliwapiku watengeneza magari wengine kwa kutengeneza magari mengi ya bei rahisi.

Na siku kama ya leo miaka 17 iliyopita, alifariki dunia Ayatullah Ali Akbar Faydh mashuhuri kwa jina la Ayatullah Mishkini.
Ayatullah Mishkini alisoma kwa wanazuoni wakubwa wa zama hizo kama Ayatullah Burujerdi na Imam Khomeini. Alikuwa miongoni mwa watu wa mwanzo kujiunga na harakati ya mapambano ya Imam Khomeini dhidi ya utawala wa Shah.
Alitiwa nguvuni na kufungwa jela mara kadhaa sambamba na kubaidishwa. Baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Mishkini alishika nyadhifa mbalimbali na muhimu zaidi ni ile ya Mwenyekiti wa Baraza la Wanazuoni wanaomchagua Kiongozi Muadhamu na Kusimamia Kazi Zake. Mwanazuoni huyu ameandika vitabu vingi ikiwa ni pamoja na Islahul Usul, Ndoa Katika Uislamu, al Mawaidhul Adadiyyah na Ukamilifu katika Uislamu.
