Jumatatu, Agosti 25, 2025
Leo Jumatatu tarehe Mosi Mfunguo Sita Rabiul Awwal mwaka 1447 Hijria, sawa na Agosti 25 mwaka 2025.
Siku kama ya leo miaka 1447 iliyopita, Mtume Muhammad SAW alianza Hijra yake ya kuhama Makka na kuelekea Madina, ikiwa imepita miaka 13 tokea alipobaathiwa na kupewa Utume.
Mtume wa Allah alihama Makka kutokana na kushadidi vitimbi vya washirikina wa mji huo ambao walikusudia kumdhuru na kumuua wakati wa usiku akiwa amelala nyumbani kwake. Imam Ali AS alijitolea mhanga, kwa kuamua kulala kwenye kitanda cha Mtume, ili maadui wasitambue kwamba Mtume wa Allah ameondoka mjini Makka.
Hijra ya Mtume SAW na matukio ya baada yake yalikuwa na umuhimu mkubwa katika ustawi na maendeleo ya Uislamu kiasi kwamba lilitambuliwa kuwa mwanzo wa kalenda ya Kiislamu.
Ni vyema kukumbusha hapa kuwa Mtume (saw) ndiye aliyekuwa wa kwanza kutumia hijra yake kama mwanzo wa kalenda ya Kiislamu kwani barua zote zilizoandikwa na mtukufu huyo kwa wakuu wa makabila na shakhsia maarufu alizisajili kwa kalenda hiyo.

Tarehe Mosi Rabiul Awwal miaka 1382 iliyopita, ilianza harakati ya Tawwabin kwa lengo la kulipiza kisasi cha kuuawa shahidi Imam Hussein AS pamoja na wafuasi wake watiifu.
Awali, watu wa Kufa walimuomba Imam Hussein AS aelekee mjini humo kwa lengo la kuongoza harakati dhidi ya utawala wa kidhalimu wa Yazid bin Muawiya lakini alizingirwa njiani na jeshi la mtawala dhalimu, Yazid bin Muawiya, na kuuawa shahidi. Tawwabin ni kundi la watu wa Kufa ambalo lilijuta kwa kushindwa kutekeleza ahadi yake na kumuacha Imam Hussein na wafuasi wake wachache peke yao wapambane na majeshi ya Yazid.
Kwa minajili hiyo watu hao walitubia makosa yao na kuamua kuanzisha harakati ya kulipiza kisasi wakiongozwa na Sulaiman bin Sorad dhidi ya jeshi la Yazid. Kundi hilo lilipigana kishujaa na jeshi la Yazid na wengi kati ya wapiganaji wake wakauawa shahidi.

Katika siku kama ya leo miaka 930 iliyopita sawa tarehe 25 Agosti mwaka 1095, vilianza Vita vya Msalaba kati ya Wakristo na Waislamu.
Watu wa msalaba walianzisha vita hivyo kidhahiri wakiwa na lengo la kuteka Baitul Muqaddas, ingawa shabaha halisi ya wapiganaji hao ilikuwa kudhibiti ardhi kubwa za Waislamu, kuwanyonya na kuwakoloni wafuasi wa dini hiyo.
Katika vita hivyo wafuasi wa kanisa walichora alama za msalaba kwenye mabega na mavazi yao, na kwa sababu hiyo vita hivyo vimekuwa maarufu kwa jina la Vita vya Msalaba. Baada ya vita vingi na Waislamu, wapiganaji wa msalaba hatimaye waliuteka na kuukalia kwa mabavu mji wa Baitul Muqaddas mnamo mwaka 1099, ambako waliua raia wengi na kupora mali zao. Mji huo ulikombolewa mwaka 1187 na wapiganaji wa Kiislamu waliokuwa wakiongozwa na Salahuddin Ayyubi.

Miaka 200 iliyopita mwafaka na siku hii ya leo, Uruguay ilipata uhuru. Tangu Uruguay ivumbuliwe na wagunduzi wa Kihispania mwaka 1516, ilitawaliwa na Wareno na Wahispania.
Baina ya mwaka 1810 na 1814 kulitokea uasi uliopelekea umwagaji damu mkubwa, ambapo baada ya matukio hayo, nchi hiyo ilipata huru wa kiasi fulani. Hata hivyo mwaka 1820 Brazil iliikalia tena kwa mabavu na miaka mitano baadaye Uruguay ikajikomboa na kujipatia uhuru kamili.

Katika siku kama hii ya leo miaka 158 iliyopita alifariki dunia msomi mashuhuri wa Uingereza, Michael Faraday.
Faraday alizaliwa mwaka 1791 mjini London na licha ya kuwa hakuwa na elimu ya juu lakini alifanikiwa kupata maendeleo muhimu katika fizikia na kemia kwa kutumia majaribio na tajiriba. Michael Faraday aligundua chombo cha mkondo wa umeme kinachojulikana kwa kitaamu kama ''Electric Current''.
Kwa ugunduzi huo Faraday akawa amefanikiwa kupiga hatua kubwa katika elimu ya fizikia. Miongoni mwa mafanikio mengine makubwa yaliyoletwa na mtaalamu huyo ni pale alipogundua mota ya umeme pamoja na kubadilisha nguvu za sumaku kuwa nguvu za umeme.