Jumapili, 7 Septemba, 2025
Leo ni Jumapili 14 Mfunguo Sita Rabiul-Awwal 1447 Hijria mwafaka na 7 Septemba 2025 Miladia
Siku kama ya leo miaka 1383 iliyopita Yazid bin Muawiya aliangamia. Yazid alikuwa mtawala dhalimu na fasiki na alitawala kwa muda wa miaka mitatu na miezi tisa. Katika kipindi cha utawala wake Yazid mwana wa Muawiya alifanya kila aina ya jinai na alitambulikana kwa ufuska. Miongoni mwa jinai zake ni kumuua shahidi mjukuu wa Mtume Muhammad SAW yaani Imam Hussein bin Ali (AS) na masahaba zake katika ardhi ya Karbala huko Iraq mwaka 61 Hijria, kushambulia kinyama miji mitakatifu ya Makka na Madina na kubomoa nyumba ya Mwenyezi Mungu yaani Al-Kaaba.
Katika siku kama ya leo miaka 200 iliyopita, nchi ya Brazil ilipata uhuru kutoka kwa mkoloni Mreno. Ureno ilianza kuikoloni Brazil mwaka 1494, na mbali na kuwatumikisha watu wa jamii ya Wahindi Wekundu wa nchi hiyo, ilichukua mamilioni ya Waafrika kwa ajili ya kuwatumikisha kama watumwa katika shughuli za kilimo.

Siku kama ya leo miaka 126 iliyopita harakati ya kihistoria ya Wanamasumbwi nchini Uchina ilikandamizwa na kuzimwa. Wanamasumbwi lilikuwa jina walilopewa wanajeshi wa China waliosimama kupambana na ubeberu wa nchi za kigeni hususan za Magharibi ulioambatana na harakati za wamishonari wa Kikristo ndani ya China. Miongoni mwa hatua zilizochukuliwa na wanamasumbwi hao ni kuteka balozi za nchi za Magharibi katika mji wa Beijing na kupambana vikali na shughuli za wahubiri wa Kikristo kutoka Ulaya. Harakati ya Wanamasumbwi wa Kichina ilikandamizwa na majeshi ya Ulaya, Marekani na Japan na serikali ya China ikalazimika kulipa gharama kubwa kwa nchi hizo. ***

Katika siku kama ya leo miaka 81 iliyopita kwa mujibu wa kalenda ya Hijria, aliaga dunia Sayyid Hussein Tabatabai Qomi, fakihi na marjaa mahiri wa Kishia. Alizaliwa mwaka 1282 Hijria katika mji mtakatifu wa Qom ulioko yapata kilomita 125 kusini mwa mji mkuu wa Iran, Tehran. Alisoma masomo yake ya utangulizi na ya msingi ya dini katika mji huo. Baadaye Sayyid Tabatabai alielekea Tehran na kunufaika na drsa na masomo ya Maulamaa wa mji huo. Akiwa na lengo la kujiendeleza zaidi kielimu alifunga safari na kwenda katika Hawza ya Najaf nchini Iraq. Mwanazuoni huyu hakuwa nyuma pia katika uandindishi wa vitabu na baadhi ya vitabu vyake ni Manasik Haj, Dhakhirat al-Ibad na Tariq al-Najat.

Tarehe 16 Shahrivar miaka 41 iliyopita aliaga dunia Ayatullah Mirza Muhammad Baqir Ashtiyani, mmoja wa maulamaa wakubwa wa Iran. Alizaliwa mwaka 1284 Hijria Shamsiya mjini Tehran. Ayatullah Ashtiyani alielekea katika chuo cha kidini cha Najaf nchini Iraq kwa ajili ya kukamilisha masomo baada ya kuhitimu masomo yake ya awali. Ayatullah Mirza Muhammad Baqir Ashtiyani alirudi Tehran na kuanza kutoa elimu kwa wanafunzi wa masuala ya dini baada ya kupata daraja ya ijtihadi. Msomi huyo mkubwa ameandika vitabu vingi vya thamani kama "Uongozi kwa Mtazamo wa Uislamu" na kile cha "Umiliki katika Uislamu".

Siku kama ya leo miaka 28 iliyopita alifariki dunia dikteta wa zamani wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo au Zaire ya zamani, Jenerali Mobutu Sese Seko. Mobutu alizaliwa mwaka 1930 nchini Congo na mwaka 1950 alijiunga na harakati ya ukombozi ya Patrice Lumumba. Baada ya uhuru wa Congo, Jenerali Mobutu alishika uongozi wa jeshi la nchi hiyo na mwaka 1960 alikuwa waziri mkuu akiwa na umri wa miaka 30. Tarehe 25 Novemba mwaka 1965 Mobutu alipindua serikali na kushika hatamu za nchi hiyo aliyeitawala kidikteta. Tarehe 16 Mei 1997 Mobutu alilazimika kukimbia nchi hiyo na kwenda Morocco ambako alifia na kuacha nyuma faili jesi la ukatili na mauaji. ***
