Jumatano, 17 Agosti, 2016
Leo ni Jumatano tarehe 14 Dhilqaada 1437 Hijria sawa na 17 Agosti 2016.
Siku kama ya leo miaka 28 iliyopita, baada ya vita vya miaka minane vya kulazimishwa vilivyoanzishwa na Iraq dhidi ya Iran, hatimaye Umoja wa Mataifa ulitangaza rasmi kusimamishwa vita hivyo kwa mujibu wa moja ya vipengee vya azimio nambari 598 la Baraza la Usalama la umoja huo. Baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran, madola yanayopenda kujitanua ambayo yaliona maslahi yao yamo hatarini hapa nchini na katika Mashariki ya Kati yalianza kufanya njama mbalimbali ili kuuangusha mfumo wa Kiislamu wa Iran. Saddam Hussein kibaraka wa madola ya Magharibi na hasa Marekani, wakati huo akiwa Rais wa Iraq alitumiwa na Washington na kuanzisha vita vya miaka minane dhidi ya taifa la Iran akitumia visingizo visivyo na msingi wowote. Mwanzoni mwa vita hivyo, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilipasisha azimio la kutaka kusimamishwa vita hivyo, ingawa cha kusikitisha katika azimio hilo ni kwamba Baraza la Usalama halikuashiria hata kidogo uchokozi wa majeshi vamizi ya Iraq dhidi ya taifa la Iran.
Miaka 29 iliyopita katika siku kama ya leo, Rudolf Hess makamu wa dikteta wa zamani wa Ujerumani Adolf Hitler alijiua akiwa jela nchini Uingereza. Hess ambaye alizaliwa mwaka 1894, alikuwa mmoja wa waasisi wa chama cha Kinazi na miongoni mwa viongozi wakuu wa serikali ya Hitler. Rudolf Hess alihukumiwa kifungo cha maisha jela na mahakama ya jinai za kivita ya Nuremberg nchini Ujerumani baada ya nchi hiyo kushindwa katika Vita vya Pili vya Dunia. Hess alijiua akiwa jela mwaka 1987.
Siku kama ya leo miaka 56 iliyopita, nchi ya Kiafrika ya Gabon iliyoko magharibi mwa Afrika na katika pwani ya bahari ya Atlantiki, ilipata uhuru wake. Wareno walifika huko Gabon kwa mara ya kwanza mwishoni mwa karne ya 15 Miladia. Hata hivyo nafasi ya kijiografia ya Gabon ilizuia kugunduliwa nchi hiyo hadi karne ya 19. Katikati ya karne ya 19 Wafaransa waliwasili Gabon na kuidhinishwa kuitawala nchi hiyo katika mkutano uliofanyika huko Berlin Ujerumani. Hatimaye mwaka 1960 Gabon ilipata uhuru. Kijiografia nchi ya Gabon inapakana na Jamhuri ya Afrika ya Kati, Kongo, Cameroon na Equatorial Guinea.
Siku kama ya leo miaka 71 iliyopita, wananchi wa Indonesia walianzisha mapambano ya kujikomboa kutoka katika makucha ya mkoloni Mholanzi. Mapambano hayo yaliyoongozwa na Ahmad Sukarno yaliendelea kwa miaka minne huko Indonesia. Baada ya kushadidi mapambano hayo ya ukombozi ya wananchi Waislamu wa Indonesia, Umoja wa Mataifa uliiamuru serikali ya Uholanzi kuuasisi utawala kwa jina la " Umoja wa Indonesia na Uholanzi". Jamhuri ya Indonesia ilivunja umoja huo mwaka 1956 na kutangaza uhuru wa nchi hiyo na Sukarno akawa Rais wa kwanza wa taifa hilo.