Jumatatu, 05 Januari, 2026
Leo ni Jumatatu 15 Rajab 1447 Hijria mwafaka na 5 Januari 2026.
Tarehe 15 Rajab miaka 1452 iliyopita kundi la kwanza la Waislamu lilianza safari ya kuondoka Makka na kuhamia Uhabeshi barani Afrika.
Hijra hiyo iliyokuwa na taathira kubwa katika harakati za Uislamu ilifanyika miaka 8 kabla ya Mtume (saw) kuhamia Madina.
Baada ya kushadidi mashaka ya Waislamu waliokuwa wakiteswa na kusumbuliwa na washirikina wa Makka, Mtume Muhammad (saw) aliwaamuru baadhi ya maswahaba zake waelekee katika ardhi ya Uhabeshi barani Afrika kwa ajili ya kujilinda na adha na mateso ya washirikina.
Kundi hilo la Waislamu lililojumuisha wanaume 11 na wanawake 4 likiongozwa na Uthman bin Madh'un, lilihamia Uhabeshi na kutayarisha uwanja na mazingira mazuri ya Hijra ya Pili ya Waislamu kuelekea katika ardhi hiyo ya Afrika. Kundi hilo la pili liliongozwa na binamu wa Mtume wetu Muhammad (saw), Ja'far bin Abi Twalib.
Hijra hizo mbili zilikuwa na mchango mkubwa wa kueneza zaidi dini ya Uislamu barani Afrika. ****
Miaka 1445 iliyopita katika siku kama ya leo, mnamo tarehe 15 Rajab mwaka wa Pili Hijria, Kibla cha Waislamu kilibadilishwa kutoka Baitul Muqaddas na kuelekea Makka kwa amri ya Mwenyezi Mungu. Mayahudi daima walikuwa wakiwakebehi Waislamu kwa vile walikuwa nao wakielekea kwenye kibla hicho hicho cha Baitul Muqaddas.
Hali hiyo iliwatia unyonge Waislamu na hasa Mtume Mtukufu SAW, na kwa minajili hiyo, katika siku kama ya leo Mwenyezi Mungu aliteremsha wahyi kwa Mtume SAW kupitia Malaika Jibrail AS akimtaka aelekee Makka wakati wa ibada ya Swala, badala ya Baitul Muqaddas. ***
Siku kama ya leo miaka 1423 iliyopita vilianza vita vya miaka 24 kati ya falme za Iran na Roma.
Vita hivyo viliibuka kufuatia kuuawa Maurice, aliyekuwa mfalme wa Romaambaye pia alikuwa muungaji mkono na rafiki wa karibu wa Mfalme Khosrow Parviz wa Iran. Kufuatia mauaji hayo ya Maurice, mtoto wake alikwenda Iran na kumuomba msaada Mfalme Khosrow. Mfalme huyo wa Iran na kwa lengo la kulipiza kisasi cha damu ya Maurince, alituma jeshi lililojizatiti kwa silaha kwenda kuishambulia Roma ambapo kwa kipindi kifupi liliweza kuteka miji mingi.
Baada ya ushindi huo, mfalme mpya wa Roma alimtuma mjumbe wake Iran kwa ajili ya kufanya mazungumzo ya amani na mfalme wa Iran, hata hivyo Mfalme Khosrow Parviz ambaye alikuwa tayari ameingiwa na kiburi cha kupata ushindi mkubwa katika vita hivyo, alikataa mpango wa amani na akaendeleza vita hivyo. Vita hivyo ambapo pande mbili zilipata ushindi katika vipindi tofauti, viliendelea kwa muda wa miaka 24. ****
Tarehe 15 Rajab mwakak 62 Hijria yaani katika siku kama hii ya leo miaka 1385 iliyopita, alifariki dunia Bibi Zaynab binti Ali bin Abi Twalib (AS) mjukuu wa Mtume Mtukufu SAW baada ya kuvumilia mateso na machungu mengi.
Bibi Zaynab AS alizaliwa mwaka wa 6 Hijiria na alipata malezi bora kutoka kwa baba yake Imam Ali AS na mama yake Bibi Fatimat Zahra AS. Mwaka 61 Hijria, Bibi Zaynab AS alishiriki katika tukio la Karbala pamoja na kaka yake Imam Hussein AS na watu wengine wa familia ya Mtume SAW.
Baada ya kuuawa shahidi Imam Hussein (AS) na wafuasi wake, Bibi Zaynab alikuwa mfikisha ujumbe wa hamasa ya kudumu ya Imam Hussein na wafuasi wake. ****
Siku kama ya leo miaka 335 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 5 Januari 1691, ilichapishwa na kusambazwa noti ya kwanza huko Ulaya.
Noti hiyo ilichapishwa na Benki ya Stockholm na kutumiwa kama fedha. Kabla ya kuchapishwa noti hiyo nchini Sweden, miamala ya kibiashara ilikuwa ikifanyika kwa kutumia sarafu za dhahabu zenye pembe nne.
Moja kati ya noti za awali kabisa kuchapishwa nchini Sweden, inahifadhiwa kwenye makumbusho ya Benki ya Stockholm. ***
Siku kama ya leo miaka 217 iliyopita, ulitiwa saini mkataba wa Dardanelles (Treaty of the Dardanelles) baina ya utawala wa Othmania na Uingereza.
Kwa mujibu wa mkataba huo, Uingereza iliahidi kuondoka katika ardhi zote zilizokuwa chini ya utawala wa Othmania ikiwemo Misri na kuhitimisha ukaliaji mabavu wa ardhi hizo. Mkabala wake, utawala wa Othmania uliahidi kutambua rasmi haki za kibalozi za Uingereza katika ardhi za utawala wa Othmania. ****
Tarehe 15 Dei miaka 47 iliyopita wanafunzi wa vyuo vikuu nchini Iran waligoma kwenda madarasani na kufunga masomo wakitangaza upinzani wao dhidi ya safari ya rais wa wakati huo wa Marekani, Jimmy Carter hapa nchini na uungaji mkono wake kwa utawala wa Shah.
Wakati huo Carter alikuwa akidai kuwa ni mtetezi wa haki za binadamu na mpinzani wa suala la kuziuzia silaha tawala za kidikteta. Hata hivyo serikali ya Washington ilichukua uamuzi wa kufunga mikataba ya kuuzia silaha nzito utawala wa kidikteta wa Shah na kupuuza ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu uliokuwa ukifanywa nchini Iran.
Jimmy Cater alifikia kiwango cha kumwita Shah kuwa ni kiongozi anayependwa na wananchi na kwamba Iran ni kisiwa cha amani. Hata hivyo muda mfupi baadaye wananchi walianza harakati za kudai uhuru na kujitawala na miezi 13 baada ya safari ya Carter mjini Tehran Shah aliondolewa madarakani na ikaanzishwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. ***
Miaka 41 iliyopita katika siku kama ya leo, inayosadifiana na tarehe 5 Januari 1985, utawala wa Kizayuni wa Israel uliwachukua maelfu ya Mayahudi wa Ethiopia, "Mafalasha', kupitia ardhi ya Sudan na kuwapeleka Palestina inayokaliwa kwa mabavu.
Mafalasha hao ambao idadi yao ilikuwa watu 8,000 walipelekwa huko katika ardhi inayokaliwa kwa mabavu ya Palestina. Nchi za Kiarabu ziliikasirikia Sudan kwa kushirikiana na Israel katika kuwahamisha Mayahudi wa Kiethiopia na kuwapeleka Palestina inayokaliwa kwa mabavu. ******
Na siku kama hii leo miaka 11 iliyopita aliaga dunia mkongwe wa soka nchini Ureno, Eusebio da Silva Ferreira. Eusebio alifariki dunia kutokana na mshituko wa moyo akiwa na umri wa miaka 71. Eusebio ambaye ni mzaliwa wa Msumbiji, aliichezea timu ya taifa ya Ureno mechi 64 na kupachika mabao 41, huku akiipachikia klabu yake ya Benfica mabao 585 katika mechi 571 alichoichezea.
Anatambuliwa kuwa mmoja kati ya wafungaji bora zaidi katika historia ya mpira wa miguu duniani. Nyota huyo, alisifika kwa kuwa na tabia na maadili bora wakati wa alipokuwa akisakata kandanda na hata baada ya kustaafu mchezo huo, na kwa sababu hiyo ametambuliwa kuwa gwiji mkubwa wa nyakati zote nchini Ureno.
Inafaa kuashiria hapa kuwa katika michuano ya Kombe la Dunia iliyofanyika 1966, Eusebio aliibuka mfungaji bora kwenye michuano hiyo kwa kupachika mabao 9 na Ureno ilishika nafasi ya tatu. Mwaka 1965, Eusebio alifanikiwa kuchaguliwa kuwa mchezaji bora duniani na kupewa tuzo ya Mpira wa Dhahabu, na mara mbili alichaguliwa kuwa mfungaji bora wa Ulaya. ****