Jumatano, Januari 07, 2026
Leo ni Jumatano tarehe 17 Rajab 1447 Hijria sawa na Januari 7 mwaka 2026 Milaadia.
Miaka 90 iliyopita katika siku kama hii ya leo, wanawake wa Kiirani walipigwa marufuku kuvaa vazi la Kiislamu la aina yoyote kufuatia amri ya Rezakhan Pahlavi.
Rezakhan alitoa amri hiyo baada ya kutekelezwa mpango wa kubadili mavazi ya wanaume nchini Iran. Mpango huo ulitekelezwa kwa lengo la kufuta thamani za Kiislamu na badala yake kuiga utamaduni wa Kimagharibi.
Rezakhan alitekeleza mpango huo wa kupiga marufuku vazi la hijabu kwa wanawake wa Kiislamu nchini Iran baada ya safari yake nchini Uturuki na kufuata nyayo za Kemal Atatürk Rais wa wakati huo wa Uturuki aliyekuwa na mielekeo ya Kimagharibi ambaye aliwapiga marufuku wanawake wa nchi hiyo kuvaa mavazi ya Kiislamu. ***
Miaka 83 iliyopita yaani mnamo tarehe 7 mwezi Januari mwaka 1943 aliaga dunia Nikola Tesla mwanafikia mzaliwa waYugoslavia.
Nikola alizaliwa mwaka 1857 na alikuwa na shauku kubwa ya kujifunza masomo ya fizikia wakati akiwa shuleni. Msomi huyo wa Kiyugoslavia alifanya tafiti na uvumbuzi wake mwingi katika uwanja wa nishati ya umeme na kupata mafanikio makubwa.
Umeme mbadala au Altenative electricity unahesabiwa kuwa miongoni mwa uvumbuzi wa Nikola Tesla. Mwanafikizia huyo alikipa jina lake la Tesla, kifaa kinachotumika kupimia kiwango na mtiririko wa sumaku yaani (magnetic flux).
Katika siku kama ya leo miaka 58 iliyopita, Gholamreza Takhti mchezaji na bingwa wa mchezo wa mieleka wa Kiirani aliuawa kwa njama zilizopangwa na utawala wa wakati huo wa Shah.
Takhti alizaliwa Tehran katika familia iliyokuwa na maisha ya kati na kati. Gholamreza Takhti alijulikana mno kwa tabia yake ya huruma, ukweli na kuwapenda watu. Katika kipindi cha uhai wake na wakati wa kushiriki mashindano mbalimbali ya kimataifa, Gholamreza Takhti alifanikiwa kuipatia Iran medali 9 za dhahabu na fedha katika mashindano ya Olimpiki.
Takhti ni miongoni mwa wachezaji wa mieleka wa Irani waliotwaa medali nyingi za dhahabu na fedha katika mashindano muhimu ya kimataifa.
Miaka 49 iliyopita kwa mujibu wa kalenda ya Hijria Shamsia, wananchi Waislamu wa Iran walifanya maandamano makubwa kote nchini wakilalamikia kuchapishwa makala iliyomvunjia heshima mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Imam Ruhullah Khomeini, Mwenyezi Mungu amrehemu. Maandamano hayo yalizidisha vuguvugu na kasi za Mapinduzi ya Kiislamu kuelekea katika ushindi.
Utawala wa Shah ambao ulikuwa ukifahamu vyema ushawishi na uungaji mkono mkubwa wa Imam Khomeini miongoni mwa wananchi, ulikuwa ukidhani kwamba kumvunjia heshima Imam Khomeini kungeweza kupunguza kiwango cha mapenzi na uungaji mkono mkubwa wa wananchi wa shakhsia huyo.
Katika kufanikisha lengo hilo, gazeti la Ittilaat lililokuwa likitolewa mjini Tehran liliandika makala ya kumvunjia heshima Imam Khomeini katika toleo lake la mwezi Dei mwaka 1356 Hijria Shamsiya. Hata hivyo makala hiyo ilikuwa kama cheche ya moto iliyochochea zaidi harakati za mapinduzi na hatimaye tarehe 22 mwezi Bahman mwaka 1357, utawala kibaraka wa Shah ukang'olewa madarakani kwa mapambano ya wananchi wa Iran. ****
Siku kama ya leo miaka 47 iliyopita, majeshi ya Vietnam yaliishambulia Cambodia na kupelekea dikteta wa nchi hiyo Pol Pot kuikimbia nchi hiyo na hatamu za uongozi kuchukuliwa na Heng Samrin.
Pol Pot alikuwa kiongozi wa kundi la Khmer Rouge la Cambodia lililokuwa likifuata fikra za Kimao. Katika kipindi cha chini ya miaka mitatu cha uongozi wake nchini Cambodia, Pol Pot akishirikiana na kundi la Khmer Rouge aliwauwa watu kati ya milioni 1.5 na milioni 2.
Katika siku kama ya leo miaka 40 iliyopita, Suleiman Khater mmoja wa polisi wa mpakani katika jangwa la Sinai, alikufa shahidi akiwa jela.
Akionyesha upinzani wake dhidi ya mkataba wa Camp David, Oktoba mwaka 1985 aliwaangamiza Wazayuni kadhaa katika jangwa la Sinai. Serikali ya Misri baada ya kumtia mbaroni askari huyo, ilimhukumu kifungo cha maisha jela.
Hata hivyo baada ya muda kiwiliwili cha Suleiman Khater kilipatikana katika kituo cha matibabu cha magereza kikiwa kimening'inia na serikali ya Misri ilidai kwamba, mfungwa huyo alijiuwa.
Katika siku kama ya leo miaka 32 iliyopita alifariki dunia mtaalamu wa masuala ya Kiislamu na mtarjumi wa Qur'ani Tukufu kwa lugha ya Kijapani Toshihiko Izutsu.
Alizaliwa tarehe 4 Mei 1914 katika mji wa Tokyo na mwaka 1960 alipata shahada ya uzamivu katika taaluma ya lugha na kuanza kufunza lugha na falsafa yake. Toshihiko Izutsu alitunukiwa nishani ya juu kabisa ya elimu kutoka kwa mfalme wa Japan na ameandika vitabu vingi. Miongoni mwa vitabu vya msomi huyo ni "Historia ya Fikra za Kiislamu", tarjumu ya kitabu cha "al Mashair" cha Mulla Sadra na vilevile tarjumu ya kitabu cha "Fihi Maa Fiih" cha Maulavi kwa lugha ya Kijapani.