Jumanne 23 Agosti, 2016
Leo ni Jumanne tarehe 20 Dhilqaada 1437 Hijria sawa na tarehe 23 Agosti 2016.
Siku kama ya leo, miaka 72 iliyopia, mji wa Paris ulikombolewa kutoka kwa mikononi mwa wavamizi wa Ujerumani. Miezi 15 baada ya kushtadi moto wa Vita vya Pili vya Dunia na katika kuendeleza njama za kujitanua kwa dikteta Adolph Hitler, aliyaamuru majeshi ya nchi hiyo kuushambulia mji wa Paris kwa lengo la kutaka kuudhibiti mji huo. Hii ni katika hali ambayo tarehe tano Juni mwaka 1940, Hitler alitoa amri ya kuharibiwa kikamilifu muundo wa majeshi ya Ufaransa ambapo siku tatu baadaye yaani tarehe nane Juni mwaka 1940, vikosi vya Wanazi vilikishinda kikosi cha ulinzi cha Ufaransa huko katika eneo la kaskazini mashariki mwa taifa hilo, na hivyo kutoa mwanya kwa jeshi la Ujerumani kuingia nchini Ufaransa.
Na miaka 981 iliyopita katika siku kama ya leo sawa na tarehe 20 Dhulqaada mwaka 456 alifariki dunia Abu Ali Qirawani, mshairi, mwanafasihi na mkosoaji wa fasihi wa Morocco. Abu Ali alijifunza mashairi, fasihi na elimu nyingi za kipindi hicho akiwa bado mdogo na baada ya hapo alielekea katika mji wa Qirawan nchini Tunisia kwa shabaha ya kushiriki katika vikao na majlisi za wasomi wakubwa. Kipindi hicho mji wa Qirawan ulikuwa kituo kikuu cha ustaarabu wa Kiislamu huko kaskazini mwa Afrika na Andalusia na wasomi wa Kiislamu na wanazuoni wengi mashuhuri walikuwa wakiishi katika mji huo. Mashairi mengi ya malenga huyo yanaakisi vipindi mbalimbali vya naisha yake ya kijamii. Mshairi huyo aligundua mbinu mpya ya kukosoa kazi za fasihi na kuacha athari nyingi katika uwanja huo.
Miaka 38 iliyopita katika siku kama hii ya leo Hujjatul Islam Walmuslimin Sayyid Ali Andarzgu aliuawa shahidi na vibaraka wa utawala wa Shah. Shahidi Andarzgu alianza harakati za mapambano akiwa na umri wa miaka 19 na kufahamiana kwa karibu na shahidi Nawab Safawi, kiongozi wa kundi la Waislamu wanamapinduzi. Baada ya hapo Shahid Andarzgu alijiunga na harakati ya Muutalifeye Eslami na alikuwa miongoni mwa waliotekeleza mauaji ya kimapinduzi dhidi ya Waziri Mkuu wa wakati huo wa Shah, Hussein Ali Mansour. Shahid Andarzgu aliendesha mapambano ya siri dhidi ya utawala wa Shah kwa kipindi cha miaka 13 na hatimaye aliawa shahidi na vibaraka wa Shah katika siku kama hii ya leo katika mapambano ya silaha mjini Tehran.