Jun 22, 2026 17:31 UTC
  • Jumatatu, tarehe 22 Juni, mwaka 2026

Leo ni Jumatatu tarehe 7 Muharram 1448 Hijria sawa na Juni 22 mwaka 2026.

Siku kama ya leo miaka 1387 iliyopita, Omar Bin Saad, alitoa amri ya kuuzuia msafara wa Imam Hussein (as), mjukuu wa Bwana Mtume Muhammad (saw) kutumia kwa aina yoyote maji ya mto wa Furati (Euphrates.)

Baada ya Ubaidullah Bin Ziyad, kutuma jeshi kubwa kwa ajili ya kupambana na mjukuu huyo wa Mtume, alituma barua kwa Ibn Saad ili kumzingira Imam Hussein na masahaba zake. Katika ujumbe huo, Bin Ziyad alimtaka Omar Bin Saad kumwamuru Al-Imamul-Hussein kumbai Yazid mwana wa Muawiya. Aidha sehemu nyingine ya barua hiyo ilimtaka kamanda huyo wa jeshi katili kumtenga mjukuu huyo wa Nabii wa Allah na maji ya Mto Furati na asimruhusu kamwe kuweza kuyanywa yeye au vamilia yake.

Bila kuchelewa Ibn Saad aliwaamuru askari 500 wapanda farasi kumzuia Imam Hussein na maji ya mto huo. Kitendo hicho cha kikatili, kilijiri ikiwa ni siku tatu kabla ya kuuawa shahidi Imam Huusein (as). Hata hivyo Abul-fadhlil-Abbas alifanya juhudi kubwa kwa ajili ya kuwaletea maji watu wa msafara huo ingawa hata hivyo askari wale katili walimzuia na kumuua kinyama mtukufu huyo.

Hadi asubuhi ya siku ya tisa ya mwezi huu wa Muharram, hakukuwa na tone la maji lililokuwa limesalia kwa wafuasi wa mjukuu huyo wa Mtume (Imam Hussein) suala ambalo liliwafanya watukufu hao kuvumilia tabu ya kiu kali kutokana na joto kali lililokuwepo eneo hilo. ***

Miaka 393 iliyopita mnajimu, mtaalamu wa hisabati na mwanafizikia wa Italia Galileo Galilei alilazimika kukana itikadi zake za kisayansi na kielimu mbele ya viongozi wa Kanisa.

Mwaka 1632 Galilei aliandika kitabu akijibu na kukosoa mitazamo ya Betlemosi kuhusu sayari ya jua na kutangaza kuwa dunia inazunguma jua. Mwaka mmoja baadaye Papa wa Kanisa Katoliki alimwita Galileo mjini Roma na kuitaja mitazamo hiyo ya kisayansi kuwa ukafiri. Kwa msingi huo, kanisa lilimlazimisha Galileo akane itikadi zake za kielimu la sivyo akabiliwe na adhabu ya kifo.

Japokuwa msomi huyo alikana mitazamo yake hiyo ya kielimu kidhahiri tu lakini wakati alipotoka nje ya mahakama alipiga chini mguu wake na kuiambia ardhi: "Licha ya haya yote lakini wewe unazunguka."      ***

Siku kama ya leo miaka 135 iliyopita, alizaliwa Sayyid Mohammad Hadi Milani, marjaa mkubwa wa Waislamu wa Shia.

Ayatullahil-Udhma Sayyid Mohammad Hadi Milani alizaliwa tarehe saba mwezi Muharram mwaka 1313 Hijiria Qamaria huko mjini Najaf, Iraq. Alianza kusoma elimu ya dini akiwa na umri mdogo ikiwa ni pamoja na kujifunza Qur'ani Tukufu mjini hapo. Baada ya hapo alijifunza fasihi ya lugha ya Kifarsi na Kiarabu huku akiandika pia vitabu vingi. Aidha kando na shughuli hiyo alikuwa akifundisha idadi kubwa ya wanafunzi elimu ya hawza ya kidini na kufikia daraja ya umarjaa.

Msomi huyo alitambulika kwa uchaji-Mungu, taqwa, na tabia njema ya hali ya juu. Kitabu cha 'Muhaadharat fii Fiqhil-Imaamiyyah' ni miongoni mwa athari za msomi huyo.     ***

Siku kama ya leo miaka 85 iliyopita, katika Vita vya Pili vya Dunia, jeshi la Ujerumani ya Kinazi lilianza mashambulizi makubwa dhidi ya Urusi ya zamani kwa jina la Operesheni ya Barbarossa. Kwa utaratibu huo Adolph Hitler akaanzisha vita vingine katika upande wa mashariki mwa Ujerumani kwa shabaha ya kutimiza mipango yake ya kutaka kujitanua zaidi. Hadi wakati huo tayari dikteta huyo alikuwa ameteka nchi kadhaa za Ulaya.  

Katika operesheni hiyo, askari wa Ujerumani walisonga mbele na kufika katika viunga vya mji mkuu wa nchi hiyo, Moscow. Hata hivyo jeshi la Ujerumani lilipata matatizo makubwa kufuatia kuanza kipindi cha baridi kali na hivyo likashindwa kusonga mbele. Wananchi na jeshi la Urusi katika miji mbalimbali ya nchi hiyo hususan Moscow, Leningrad na Stalingrad walipambana vikali na jeshi hilo vamizi na kulilazimisha kurudi nyuma. Mwezi Agosti 1944 jeshi la Urusi lilifika katika mipaka ya Ujerumani.   ****

Katika siku kama ya leo miaka 51 iliyopita ilianzishwa Harakati ya Ukombozi wa Chad.

Tangu mwishoni mwa karne ya 19 nchi ya Chad iliyoko katikati mwa Afrika ilikuwa chini ya udhibiti wa Ufaransa na ilipata uhuru mwaka 1960 baada ya kukoloniwa kwa kipindi cha karibu miaka 80. Hata hiyo iligawanyika katika sehemu mbili tofauti. Sehemu ya kaskazini iliyokuwa nyuma kimaendeleo na kiuchumi, na ya kusini iliyokuwa na suhula nyingi na makau makuu ya nchi ambayo ilidhibitiwa na Wakristo.

Tarehe 22 Juni mwaka 1960 kuliundwa Chama cha Maendeleo ya Chad kwa lengo la kuunganisha tena nchi hiyo na kuimarisha umoja wa kitaifa na ustawi wa kiuchumi. Chama hicho kilivunjwa mwaka 1973 na nafasi yake ikachukliwa na Harakati ya Kitaifa ya Mapinduzi ya Kiutamaduni na Kijamii.   ******

Na miaka 45 iliyopita sawa na tarehe Mosi Tir mwaka 1360 kwa mujibu wa Kalenda ya Kiirani, hayati Imam Ruhullah Khomeini alipasisha uamuzi wa Bunge la Jamhuri ya Kiislamu wa kutokuwa na imani na rais wa wakati huo, Abul Hassan Bani Sadr, na kwa utaratibu huo kiongozi huyo akalazimika kung'atuka madarakani.

Bani Sadr ni miongoni mwa watu waliojidhihirisha kuwa wapenzi na watetezi wa harakati za Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran baada ya Imam Khomeini kuhamia Paris, Ufaransa na alifanikiwa kushika madaraka ya nchi na kuwa rais katika uchaguzi wa kwanza wa baada ya Mapinduzi ya Kiislamu nchini kwa kutumia ujanja wa kipropaganda.

Muda mfupi baadaye Imam Khomeini alimkabidhi ukamanda wa majeshi ya Jamhuri ya Kiislamu. Hata hivyo Bani Sadr aliyekuwa mtu mwenye uchu wa madaraka, mwenye kiburi na msaliti alianza mara moja kushirikiana na makundi yaliyokuwa yakipinga Mapinduzi ya Kiislamu kwa lengo la kuangusha utawala wa Kiislamu nchini Iran.  ***