Jul 02, 2026 02:52 UTC
  • Leo Katika Historia
    Leo Katika Historia

Leo ni Alkhamisi tarehe 17 Mfunguo Nne Muharram 1448 Hijria sawa na tarehe Pili Julai 2026.

Siku kama ya leo miaka 550 iliyopita kwa mujibu wa kalenda ya Hijria, aliaga dunia Nuruddin Abdul-Rahman Jami, mshairi na mwanafasihi mkubwa wa Kiirani wa karne ya 9 Hijria.

Alizaliwa katika mji wa Jam ulioko katika mkoa wa Khorasan kaskazini mashariki mwa Iran. Alianza kujifunza elimu mbalimbali akiwa katika rika la ujana. Aliwapenda sana Watu wa Nyumba ya Mtume Muhammad (SAW) na katu hakuwahi kuwasifu wafalme na watawala.

Silsilat al-Dhahab, Nafahatul Uns, Shawahidu Nubuwah na "Baharestan" ni baadhi ya athari za Nuruddin Abdul Rahaman Jami.    ***

Siku kama ya leo miaka 495 iliyopita alizaliwa Bahauddin al Amili maarufu kwa jina la Sheikh Bahai, faqihi na aalimu mkubwa wa Kiislamu huko katika mji wa Baalbek nchini Lebaon.

Baba yake Sheikh Bahai alikuwa mmoja wa maulamaa wakubwa wa Lebanon ambaye alisafiri naye nchini Iran akiwa mtoto. Sheikh Bahai alitumia kipaji chake kikubwa na kuweza kufikia daraja ya uanazuoni katika kipindi kifupi.

Mwanazuoni huyo alipewa jina la Sheikhul-Islam kutokana na kipawa cha kielimu cha hali ya juu alichokuwa nacho. Sheikh Bahai ameacha zaidi ya vitabu 88 alivyoviandika kwa lugha za Kifarsi na Kiarabu. Baadhi ya vitabu vyenye thamani vya msomi huyo wa Kiislamu ni Jami' Abbasi na Kashkool kilichojumuisha riwaya na Hadithi, Tashrihul Aflak na vingine vingi alivyoviandika kuhusu masuala ya hisabati na kemia.

Sheikh Bahai alifariki dunia mwaka 1030 Hijria huko Isfahan, Iran.  ****

Siku kama ya leo miaka 137 iliyopita mfumo wa kisultani ulifutwa huko Brazil katika mapinduzi ambayo hayakuwa na umwagaji wa damu na badala yake ukaasisiwa mfumo wa jamhuri.

Mfalme wa mwisho wa Brazil alikuwa Pedro II ambaye alifanya jitihada za kufanya mabadiliko nchini humo. Hatua za mfalme huyo hususan ile ya kuondoa biashara ya utumwa mwaka 1888, iliwakasirisha wamiliki wa ardhi waliokuwa wakiunga mkono mfumo wake wa kisultani.

Pedro II alienguliwa madarakani bila ya mapambano yoyote na mfumo wa jamhuri ukaasisiwa nchini Brazil. ***

Miaka 101 iliyopita katika siku kama hii ya leo alizaliwa Patrice Lumumba mhandisi wa uhuru wa Kongo.

Lumumba alitoa mchango mkubwa katika juhudi za kukombolewa Kongo wakati wa harakati za ukombozi wa nchi za Kiafrika. Lumumba aliteuliwa kuwa Waziri Mkuu na Waziri wa Ulinzi baada ya kuundwa Jamhuri ya Kongo mwaka 1960.

Patrice Lumumba aliuawa mwaka 1961 na vibaraka wa Marekani na Ubelgiji baada ya kuvumilia mateso na unyama mkubwa.

Lumumba aliandika vitabu kadhaa wakati wa uhai wake na mashuhuri zaidi ni kile alichokita "Kongo, Nchi Yangu."    *****

Tarehe Pili Julai miaka 65 iliyopita aliaga dunia mwandishi mtajika wa Kimarekani kwa jina la Ernest Hemingway.

Alizaliwa mwaka 1899 na kwa muda fulani alijishughulisha na uandishi huko Uingereza na Ufaransa. Hemingway alianzisha mbinu ya kuandika riwaya na tungo fupi fupi na alikuwa akitumia lugha nyepesi na inayoeleweka. Mwaka 1954 mwandishi Ernest Hemingway alitunukukiwa tuzo ya Nobel katika medani ya fasihi.

Miongoni mwa vitabu maarufu vya Hemingway ni "The Old Man and The Sea", "A Farewell to Arms" na For Whom The Bell Tolls".  ***

Na tarehe 11 Tir miaka 44 iliyopita Ayatullah Muhamad Saduqi alimu mkubwa, mwanamapambano na Imamu wa Ijumaa wa mji wa Yazd huko katikati mwa Iran, aliuawa shahidi na vibaraka wa kundi la kigaidi la MKO na kuwa shahidi wa nne aliyeuawa katika mihrabu ya Swala katika historia ya Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran.

Ayatullah Muhammad Saduqi alikamilisha masomo yake ya kidini katika Hauza ya mji mtakatifu wa Qum, Iran, na kustafidi na bahari kubwa ya elimu kutoka kwa walimu mashuhuri wa kituo hicho cha kielimu kama vile Ayatullah Burujerdi na Ayatullah Khansari.

Tangu mwanzo wa mapambano ya watu wa Iran dhidi ya utawala wa Shah, Saduqi alishiriki kikamilifu katika harakati za Mapinduzi na alitambuliwa kuwa rafiki wa karibu wa Imam Khomeini (Mwenyezi Mungu amrehemu). Baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu alikuwa mwanachama wa Baraza la Wataalamu wanaomchagua Kiongozi Mkuu wa Iran na alikuwa na nafasi muhimu katika kuandika Katiba ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Ayatullah Saduqi alikuwa mwakilishi wa Imam Khomeini (RA) na Imam wa Swala ya Ijumaa ya Yazd. Alitoa huduma nyingi kwa watu wa eneo hilo, na kwa sababu hiyo, alipendwa sana na wananchi.

Msomi na mwanamapinduzi huyo wa Kiislamu aliuawa shahidi na maadui wa Uislamu wakati wa Swala ya Ijumaa.