Jumanne, 30 Juni, 2026
Leo ni Jumanne tarehe 15 Muharram 1448 Hijria sawa na tarehe 30 Juni 2026.
Siku kama ya leo miaka 1095 iliyopita, yaani tarehe 15 Muharram mwaka 353 Hijiria, alifariki dunia Ibn Sakan mwanazuoni na mpokezi mashuhuri wa hadithi wa karne ya nne Hijiria.
Ibn Sakan alizaliwa mwaka 294 Hijiria huko mjini Baghdad, Iraq ambapo alisafiri katika nchi mbalimbali kwa ajili ya kutafuta elimu. Ibn Sakan alikusanya hadithi nyingi katika miji ya nchi kama Uzbekistan, Tajikistan, Kazakhstan Kyrgyzstan (Transoxiana), Khorasan, Iraq, Sham na Misri na mwishowe akaweka makazi yake nchini Misri.
Mpokezi huyo wa hadithi ameacha athari nyingi na mojawapo ni kitabu cha historia kinachohusu maswahaba wa Mtume SAW, kinachoitwa Al Huruf fi Al -Swahaba. *****
Katika siku kama ya leo, miaka 859 iliyopita, sawa na tarehe 15 Muharram mwaka 589, alizaliwa Ali bin Mussa bin Ja'far maarufu kwa jina la Ibn Twaus, faqihi, mpokezi wa hadithi na mwanazuoni mashuhuri wa Kiislamu katika eneo la Hillah nchini Iraq.
Ibn Twaus alipitisha kipindi cha utotoni katika mji huo na baadaye alihamia mjini Baghdad ambako aliishi kwa kipindi cha karibu miaka 15. Ibn Twaus alipata umashuhuri mkubwa katika elimu na ucha-Mungu na ameandika vitabu vingi ambavyo ni marejeo ya taaluma za Kiislamu.
Kitabu mashuhuri zaidi cha msomi huyo ni "al Luhuuf" ambacho ndani yake alizungumzia kwa namna bora zaidi matukio ya Siku ya Ashura na harakati ya Imam Hussein bin Ali bin Abi Twalib (as) katika medani ya vita vya Karbala. Kitabu kingine mashuhuri cha mwanazuoni huyo ni "Al Iqbal". Ibni Twaus alifariki dunia mwaka 664 akiwa na umri wa miaka 75. ****
Katika siku kama ya leo miaka 66 iliyopita Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (Zaire ya zamani) ilijitangazia uhuru na Joseph Kasavubu akawa rais wa nchi hiyo, huku Patrice Lumumba akiwa Waziri Mkuu.
Kongo ilikoloniwa na Ubelgiji. Mapambano ya kudai uhuru yaliyoongozwa na Patrice Lumumba yalishika kasi katika miaka ya mwisho ya kumalizika kwa Vita vya Pili vya Dunia na kupelekea nchi hiyo kujipatia uhuru wake.
Hata hivyo baada ya Kongo kupata uhuru zilianza harakati nyingi za uasi zilizokuwa zikiungwa mkono na Ubelgiji. Katika upande mwingine kulishadidi mapigano kati ya Lumumba na Musa Chumbe kiongozi aliyekuwa akiungwa mkono na Ubelgiji.
Hatimaye mnamo mwaka 1965 Jenerali Mobutu Sese Seko aliyeungwa mkono na Marekani alifanya mapinduzi ya kijeshi na kutwaa madaraka ya nchi hiyo ambapo badaye alianza kuwakandamiza wananchi masikini wa Kongo. ***
Katika siku kama ya leo miaka 40 iliyopita, sawa na tarehe 9 Tir 1365 Hijria Shamsia, ilianza operesheni ya kijeshi ya Karbala -1 kwa ajili ya kukomboa mji wa Mehran huko magharibi mwa Iran uliokuwa umetwaliwa na jeshi vamizi la Saddam Hussein wa Iraq.
Mji huo ulikaliwa kwa mabavu muda mfupi baada ya jeshi la Baath la Iraq kuvamia ardhi ya Iran Septemba 1981 na ulikombolewa na wapiganaji shupavu wa Iran katika operesheni makini ya Karbala-1. ****
Miaka 37 iliyopita katika siku kama ya leo, Jenerali Omar Hassan Ahmad Al Bashir wa Sudan aliongoza mapinduzi ya kijeshi na kuuangusha utawala wa Swadiq Al Mahdi bila ya umwagaji damu. Utawala huo ulikuwa ukikabiliwa na matatizo mbalimbali ya ndani.
Baada ya mapinduzi hayo Omar Hassan Al Bashir kwa kushirikiana na Hassan Al Turabi alianzisha chama cha Kongress ya Kitaifa huku yeye akiwa mwenyekiti wa chama hicho na rais wa nchi. Baada ya Al Bashir kutwaa urais alijitahidi kujitenga na siasa za Marekani, hatua ambayo iliipelekea serikali ya Washington kuichukia Khartoum na kuchukuua hatua za kiaduai dhidi ya serikali ya Al Bashir.
Miongoni mwa hatua za kiadui zilizochukuliwa na Marekani dhidi ya Sudan ni kuwaunga mkono waasi wa Kusini mwa Sudan ambapo mwaka 2011 eneo hilo la kusini lilijitenga na Sudan na kujitangazia uhuru wake. Hata hivyo al Bashir alibadilisha mielekeo yake na kuwa tegemezi kwa utawala mwa kifalme wa Saudi Arabia. Utawala wa al Bashir ulitafunwa na ufisadi, utumiaji mbaya wa madaraka, hali mbaya ya uchumi na kufuata kibubusa sera za Saudi Arabia katika vita vya Yemen. Mambo haya yaliwakasirisha Wasudani walioanzisha harakati ya upinzani dhidi ya al Bashir na hatimaye tarehe 11 Aprili mwaka 2019 kiongozi huyo alilazimika kung'atuka madarakani na kutiwa nguvuni kwa tuhuma za ufisadi na utakatishaji wa fedha chafu. Omar al Bashir anatumikia adhabu ya kifungo. ***
Katika siku kama ya leo miaka 35 iliyopita, mfumo wa utawala wa ubaguzi wa rangi nchini Afrika Kusini ulihitimishwa.
Kuanzia mwaka 1948, wazungu walio wachache nchini Afrika Kusini walianza kutekeleza siasa za kibaguzi dhidi ya wazalendo weusi. Kwa mujibu wa siasa hizo, wazungu waliokuwa wakiunda asilimia 20 tu ya wananchi wa Afrika Kusini walihesabiwa kuwa jamii bora zaidi na iliyokuwa na nafasi muhimu katika uendeshaji wa masuala ya nchi hiyo.
heria za kibaguzi kama vile za kupiga marufuku watu weusi kuoana na watu weupe na vilevile kushiriki katika harakati za kisiasa ni baadhi tu ya sheria za kibaguzi zilizotekelezwa na makaburu nchini Afrika Kusini. Siasa hizo ziliwakasirisha mno walimwengu na nchi nyingi duniani kukata uhusiano na utawala huo. ***