Maswali Yetu na Majibu ya Thaqalain (139)
Assalaama Aleikum Warahmatullahi Wabarakatuh wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inayokutangazieni kutoka mjini Tehran. Karibuni kusikiliza kipindi kingine katika mfululizo wa vipindi vya kiitikadi vya Maswali Yetu na Majibu ya Thaqalain.
Ndugu wasikilizaji, je ni kwa nini Mtme Mtukufu (saw) alibana njia ya uongofu dhidi ya upotovu wa kila aina sio katika kushikamana kikamilivu na Qur’ani Tukufu tu bali na Ahlul Beit wake watoharifu kwa kusema katika hadithi ya Thaqalain: ‘Vitu viwili ambavyo iwapo mtashikamana navyo ipaswavyo, kamwe hamtapotea baada yangu?’
Hili ndilo swali ambalo tumekuwa tukilijadili katika vipindi kadhaa vilivyopita kwa kutegemea Qur’ani Tukufu yenyewe ambapo tumeona kwamba hadithi ya Thaqalain na kubanwa kwenye hadithi hiyo uongofu katika kushikamana kikamilifu na kitabu hiki kitakatifu pamoja na Watu wa Nyumba ya Mtume (saw) ni ufafanuzi na tafsi ya Mtume Mtukufu kuhusiana na aya kadhaa za kitabu hiki cha mbinguni. Aya hizo ni pamoja na aya za 43 na 44 za Surat an-Nahl, aya ya 7 ya Surat Aal Imran aya za 75 hadi 80 za Surat al-Waqiah na aya ya 49 ya Surat ak-Ankabut ambapo tutaendelea kunufaika na nuru ya aya hizi katika kipindi chetu cha leo, karibuni.
Ndugu wasikilizaji, katika aya hii ya 49 ya Surat al-Ankabut, Mwenyezi Mungu amekisifu kitabu chake kwa njia ya kuvutia sana na inayopaswa kuzingatiwa na kila mmoja wetu. Anasema katika aya hii na katika aya nyingine mbili za kabla yake: Na namna hivi tumekuteremshia Kitabu (cha Qur'ani). Basi wale tuliowapa Kitabu (cha Biblia) wanakiamini (Qur'ani), na miongoni mwa hawa (washirikina) wapo wanaokiamini. Na hawazikatai Ishara zetu isipo kuwa makafiri. Na wewe hukuwa kabla yake unasoma kitabu chochote, wala hukukiandika kwa mkono wako wa kulia. Ingelikuwa hivyo wangelifanya shaka wabatilifu. Bali hii (Qur'ani) ni Ishara zilizo wazi katika vifua vya waliopewa ilimu. Na hawazikatai Ishara zetu isipokuwa madhalimu.
Wapenzi wasikilizaji tunapozingatia aya hizi tukufu tunaona kwamba zinabainisha wazi mambo kadhaa. La kwanza ni kwamba zinasisitiza kuwa Qur’ani Tukufu inatoka kwa Mwenyezi Mungu na kwamba aliiteremshwa kwa Mtume wake Mtukufu (saw) ambaye kabla ya hapo alikuwa hajawahi kusoma kitabu kingine chochote wala kukiandika kwa mkono wake wa kulia, yaani hakukiandika kitabu hicho yeye mwenyewe wala kukinukuu kutoka kwenye kitabu kinginge kabla ya hicho kama walivyodai washirikina kwamba Qur’ani Tukufu ilinakiliwa kutoka vitabu vingine vya kale.
Hakika na jambo la pili ambalo tunajifunza kutokana na aya hizi ni kwamba kuna watu ambao walipewa elimu na Mwenyezi Mungu kuifanya Qur’ani kuwa Ishara zilizo wazi kwenye vifua vyao, na kwamba miongoni mwa watu kunao wale wanaoiamini Qur’ani hii kwa kuwafuata wale waliopewa elimu na Kitabu, na wakati huohuo kuna wale ambao huipinga nao ni makafiri na madhalimu.
Je, ni nani hawa waliopewa elimu na Mwenyezi Mungu na kujaaliwa Qur’ani kuwa ishara za wazi kwenye vifua vyao? Ili kupata jibu la swali hili tunairejea Qur’ani yenyewe ambapo tunapata kwamba inafafanua wazi kuwekwa kwa kitabu hiki kitakatifu kwenye vifua vya kundi maalumu la watu na wakati huohuo kubainisha wazi kwamba Qur’ani iliteremshwa kwenye moyo wa Mtume Mtukufu (saw).
Mwenyezi Mungu anasema katika aya ya 97 ya Surat al-Baqarah: Sema: Aliye kuwa ni adui wa Jibril, hakika yeye ameiteremsha (Qur'ani) moyoni mwako kwa idhini ya Mwenyezi Mungu, inayosadikisha yale yaliyokuwa kabla yake, na ni uwongofu na bishara njema kwa Waumini.
Na Mwenyezi Mungu anasema katika aya za 192 hadi 195 za Surat as-Shua’ra: Na bila ya shaka hiyo ni uteremsho wa Mola wa walimwengu wote. Ameiteremsha Roho muaminifu. Juu ya moyo wako, ili uwe katika waonyaji. Kwa ulimi wa Kiarabu ulio wazi.
Kwa maelezo haya tunafahamu kwamba watu hawa waliopata fursa ya kuteremshwa Qur’ani kwenye vifua vyao wanapasa kuwa ni watu wasafi na watoharifu kiasia cha kuwawezesha kuwa chombo na mahala pasafi pa kuteremkia kitabu hicho kitakatifu kupitia Malaika Jibril. Kwa msingi huo hao ndio waja wema na bora kati ya waja wote wa Mwenyezi Mungu ambao walitakaswa na Mola wao na nyoyo zao kufanywa kuwa chombo kinachofaa kuhifadhiwa kitabu hicho kitakatifu kutoka kwa Mtume Mtukufu (saw). Hili ndilo jambo linalosisistizwa na aya ya 32 ya Surat al-Faatir kama tutakavyoona hivi karibuni, hivyo endeleeni kuwa pamoja nasi.
Mwenyezi Mungu anasema katika aya za 31 na 32 za Surat al-Faatir: Na hayo tuliyokufunulia kutoka Kitabuni ni kweli yenye kusadikisha yaliyokuwa kabla yake. Hakika Mwenyezi Mungu kwa waja wake ni Mwenye habari na Mwenye kuona. Kisha tumewarithisha Kitabu wale ambao tumewateuwa miongoni mwa waja wetu. Kati yao yupo aliyejidhulumu nafsi yake, na yupo wa katikati, na yupo aliyetangulia katika mambo ya kheri, kwa idhini ya Mwenyezi Mungu. Hiyo ndiyo fadhila kubwa.
Ni wazi kutokana na aya hizi tukufu kwamba Mwenyezi Mungu aliliteua kundi la watu aliowatakasa na kisha kuwarithisha Qur’ani ambayo alimteremshia Mtume wake Mtukufu al-Habib al-Mustafa (saw). Kwa maelezo hayo ni wazi kwamba kundi hili haliwezi kuwa ni la madhalimu wala watu wa katikati ambao hushughulishwa tu na nafsi zao bila kujali waja wengine wa Mwenyezi Mungu. Kundi hilo ndilo lililo na sifa ya watu wema waliotangulia katika mambo ya kheri kwa idhini ya Mwenyezi Mungu, yaani kwa uwezo na ilhamu yake. Na hizi ndizo miongoni mwa sifa za waja wema walioteuliwa na Mwenyezi Mungu kuwa Maimamu kama anavyobainisha wazi hilo katika aya ya 73 ya Surat al-Anbiyaa ambapo anasema: Na tukawafanya maimamu wakiongoza kwa amri yetu. Na tukawapa wahyi watende kheri, na wasimamishe Swala, na watoe Zaka; na walikuwa wanatuabudu Sisi tu.
Hakuna mtu yoyote katika Umma wa Muhammad (saw) ambaye amesifiwa na Qur’ani Tukufu kuwa ni mtoharifu na hilo kuthibitishwa na Mwenyezi Mungu mwenyewe, isipokuwa Ahlul Beit wa Mtume Mtukufu (saw) kama tulivyoona hilo katika aya ya Tat’hir. Na wala hakuna mtu yoyote katika umma huu ambaye Mtume Mtukufu (saw) amethibitisha kuwa kwake na elimu kamili kuhusiana na mafundisho na mambo yote yaliyotajwa kwenye Qur’ani Tukufu isipokuwa Ahlul Beit na Maimamu kutoka kwenye kizazi chake (saw), kama inavyothibitisha wazi suala hilo hadithi ya Thaqalain na hadithi nyinginezo sahihi na za kuaminika kutoka kwa mtukufu huyo.
Kwa maelezo hayo inabainika wazi kwamba Mwenyezi Mungu aliwarithisha Maimamu hawa wema (as) Kitabu chake na kukifanya kuwa aya zilizo wazi kwenye vifua vyao, na kulifanya hilo kuwa mahususi kwao tu bila ya kuwajaalia watu wengine jambo hilo. Kwa msingi huo inabainika wazi kwamba waja hawa wema tu ndio watu wanaopasa kurejelewa katika kuelewa vyema maarifa na hakika za Qur’ani Tukufu. Hii ni kwa sababu aya zilizo wazi za Qur’ani Tukufu zimewekwa kwenye vifua vyao na Mwenyezi Mungu ambaye aliwapa elimu ya yale yote yaliyomo kwenye kitabu hicho cha mbinguni, ambapo aliwateua wao tu kuwa marejeo maasumu yasiyofanya dhambi wala kukosea katika kukifahamu kitau hicho kitukufu. Wao (as) ndio wanaotangulia na kuwa kwenye mstari wa mbele katika kufanya mambo ya kheri na kwa hivyo hawawezi kuwa mabakhili katika kutoa kile wanachoombwa na wahitaji wanaotaka kujua maarifa ya Qur’ani yaliyohifadhiwa. Wao ndio wanaokikinga kitabu hicho kutokana na fitina na upotovu wa wapotoshaji wa Qur’ani ambao hujaribu kukifasiri na kukifafanua kitabu hicho hali ya kuwa hawafai wala kuwa na ujuzi na maarifa ya kufanya hivyo. Tunamwomba Mwenyezi Mungu atuepushe na fitina ya waovu hao kwa baraka za kushikamana kikamilifu na Vitu Viwili Vizito vya uongofu tulivyoachiwa na Mtume Mtukufu (saw).
*******
Wapenzi wasikilizaji, hakika hizi ambazo tumepata kujifunza kutokana na aya tulizozisoma zimezungumziwa pia na hadithi tukufu kadhaa ambazo tutazijadili katika kipindi chetu kijacho cha Maswali Yetu na Majibu ya Thaqalain, panapo majaaliwa. Basi kutoka Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inayokutangazieni kutoka mjini Tehran hatuna la ziada ila kukuageni huku tukikutaieni kila la kheri maishani. Kwaherini.