Maswali Yetu na Majibu ya Thaqalain (140)
Assalaam Aleikum wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na karibu kusikiliza sehemu ya 140 katika mfululizo wa vipindi hivi vya kiitikadi vya Maswali Yetu na Majibu ya Thaqalain.
Leo bado tunaendelea kujibu swali ambalo tumekuwa tukilijadili kwa kina katika vipindi kadhaa vilivyopita. Swali lenyewe linasema, je, ni kwa nini Mtume Mtukufu (swa) katika hadithi mashuhuri ya Thaqalain alibana uongofu wa Waislamu katika kushikamana kwao kwa pamoja na Vizito Viwili ambavyo ni Kitabu cha Mwenyezi Mungu, Qur’ani Tukufu na kizazi chake kitoharifu (as)?
Katika mijadala yetu iliyopita tulipata majibu kadhaa ya Qur’ani Tukufu na kufahamu kwamba suna ya Mwenyezi Mungu imesimama juu ya msingi wa kutimiza hoja kwa waja wake kwa kufungamanisha maneneo yake matakatifu na waja wake wema ambao ni maasumu wasiotenda dhambi wala kufanya kosa katika ufikishaji ujumbe, ili wawabainishie watu uelewa na maarifa sahihi ya Mwenyezi Mungu na wakati huohuo kupinga upotovu unaonezwa na watu waovu walio na maradhi kwenye nyoyo zao na ambao daima hufanya juhudi za kuwapotosha watu kwa kufasiri visivyo maneno ya Mwenyezi Mungu bila ya kutoa dalili yoyote ya kukinaisha kimantiki. Ni kwa msingi huo ndipo Mwenyezi Mungu Mtukufu akasema bayana kwamba amejaalia Qur’ani Tukufu kuwa Ishara za wazi alizoziweka kwenye vifua vya waja wema waliopewa elimu ili wapate kuwa marejeo ya uelewa na ufahamu sahihi kwa waja wake. Watukufu hao hufasiri na kufafanua kitabu hicho cha mbinguni kwa njia sahihi na iliyo mbali na matamanio yao binafsi. Wema hao ni wale ambao wametakaswa na kukingwa na matamanio potoevu, shaka na kila jambo linalozuia ufahamu sahihi na salama wa maneno ya Mwenyezi Mungu. Tulifahamu kutokana na aya tulizosoma katika vipindi kadhaa vilivyopita kwamba watukufu hao si wengine bali ni Ahlul Beit wa Mtume Muhammad (saw), ambao Mwenyezi Mungu mwenyewe amethibitisha usafi na utakasifu wao kutokana na kila uchafu na hili ni jambo ambalo pia linathibitishwa na hadithi nyingi ambapo tutakunukulieni baadhi ya hadithi hizo hivi punde, karibuni.
Imam Baqir (as) amenukuliwa katika kitabu cha Baswair akisema: ‘Uchafu ni shaka, na wala hatushuku katika dini yetu….. bali ni Ishara zilizo wazi kwenye vifua vya wale waliopewa elimu…..’
Akasema mpokezi wa hadithi, ambaye ni Abu Baswir: ‘Nikasema, je, ni nyinyi?’
Akasema (as): ‘Je, atakuwa ni nani mwingine?’
Madhumuni ya hadithi hii pia imepokelewa katika hadithi nyingine kadhaa ambazo zimeashiria kwa njia ya kuvutia aya ya Tat’hir. Zinasema kwamba Mwenyezi Mungu aliwatakasa Ahlul Beit (as) kutokana na uchafu ili apate kuwapa elimu ambayo aliiweka kwenye vifua vyao na hivyo kuvifanya kuwa kama chombo cha kuhifadhiwa Qur’ani Tukufu ndani yake na kuwa mfano wa Ishara zizlizo wazi ambazo hazina shaka wala mambo yasiyoeleweka vyema ndani yake.
Na hadithi nyingine ambayo imepokelewa katika vitabu vya Baswair, al-Kafi na vinginevyo inasema kwamba Abu Baswir alimuuliza Imam Swadiq (as) kuhusiana na kauli ya Mwenyezi Mungu inayosema: Bali hii (Qur'ani) ni Ishara zilizo wazi katika vifua vya waliopewa ilimu, na Imam (as) akamjibu kwa kusema: ‘Wallahi aliyoyasema yamo kwenye Musahafu.’ Yaani kwa maana kwamba Qur’ani Tukufu ni Ishara za wazi na zilizokamilika moja kwa moja ambazo haziambatani na shaka wala uelewa mbaya kwa wale waliopewa elimu kamili ya Qur’ani na Mwenyezi Mungu. Ni kwa msingi huo ndipo Imam Baqir (as) akasema katika hadithi ya tatu kwamba wao ndio waliokusudiwa katika aya inayozungumzia kuwekwa elimu kwenye vifua vya waliopewa elimu.
*********
Imam Swadiq (as) pia amepokelewa akisema: ‘Hakika miongoni mwa elimu tuliyopewa ni ya kufasiri Qur’ani.’
Imam Baqir (as) amepokelewa katika Tafsiri ya al-Ayyashi akisema kuhusiana na kauli ya Mwenyezi Mungu mwishoni mwa Surat ar-Ra’ad inayosema: Sema: Mwenyezi Mungu anatosha kuwa shahidi baina yangu na nyinyi, na pia yule mwenye ilimu ya Kitabu: ‘Alimaanisha sisi na Ali (as) ni mbora wetu baada ya Mtume (saw).’ Imam Swadiq (as) amenukuliwa katika tafsiri hiyohiyo ya al-Ayyashi akisema: ‘Sisi ni Ahlul Beit ambao Mwenyezi Mwenyezi Mungu anaendelea kuteua miongoni mwetu watu wanaojua Kitabu tokea mwanzo hadi mwisho wake.’ Imam Swadiq (as) vilevile amesema: ‘Hakika Mwenyezi Mungu alimfundisha Mtume wake (saw) uteremsho (dhihiri ya aya za Qur’ani) na ufafanuzi (maana halisi na ya kina ya aya za Qur’ani) naye Mtume akamfundisha Ali elimu hiyo.’ Kuna hadithi nyingine nyingi ambazo zimepokelewa kuhusiana na suala hili kama ilivypokolewa katika kitabu cha Yaqeen kuhusiana na uongozi wa Imam Ali (as) ambapo Anas bin Malik amenukuliwa kupitia mapokezi tofauti kutoka kwa Mtume Mtukufu (saw) kwamba alimwambia Imam Ali (as): ‘Wewe unatokana na mimi, unatekeleza mambo kwa niaba yangu, unatekeleza wajibu wa dhima yangu na kufikisha ujumbe wangu.’ Ali (as) akasema: ‘Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu! Je, kwani haukufikisha Ujumbe?’ Mtume (saw) akasema: ‘Ndio nimefikisha lakini utawafundisha watu baada yangu mambo wasiyoyajua katika kufasiri Qur’ani.’
Imepokelewa katika kitabu cha Ta’weel al-Ayaat cha Sharaf ad-Deen al-Husseini kwamba Abdul Aziz al-Abdi alimuuliza Imam Swadiq (as) kuhusiana na watu wanaokusudiwa na Mwenyezi Mungu katika kauli yake inayosema: Bali hii (Qur'ani) ni Ishara zilizo wazi katika vifua vya waliopewa ilimu, akasema (as): ‘Wao ni Maimamu katika kizazi cha Muhammad – Swala za Mwenyezi Mungu ziwe juu yao wote – ziendelee kuwepo na kudumu katika zama zote.’
Na Imam Ali (as) amepokelewa katika kitabu cha al-Ihtijaaj na Aamali cha at-Tusi kwamba alisema: ‘Niulizeni kuhusiana na Kitabu cha Mwenyezi Mungu kwa sababu Wallahi! Hakuna aya yoyote iliyoteremka katika Kitabu cha Mwenyezi Mungu ewe ni nyakati za usiku au mchana, wakati (Mtume) akiwa kwenye harakati (akitembea) njiani au akiwa amesimama ila Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) alinisomea na kunifundisha tafsiri yake.’
Akasema Abul Kuwwa, ambaye alikuwa miongini mwa Khawarij waliokuwa na chuki kubwa dhidi ya Imam Ali (as): ‘Ewe Amirul Mu’mineen! Na yale yaliyokuwa yakimteremkia (Mtume) hali ya kuwa uko mbali naye? Yaani alikuwa akikufundisha vipi hayo? Imam (as) akamjibu kwa kusema: ‘Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) alikuwa akinihifadhia yale yaliyokuwa yakimteremkia katika Qur’ani hali ya kuwa mimi niko mbali naye na kunisomea niliporejea kwake. Alikuwa akisema: Ewe Ali! Yaliteremka kadha wa kadha baada yako na tafsiri yake ni kadha wa kadha, na hivyo kunifundisha tafsiri (maana ya kina) na uteremsho (maana ya dhahiri) wake.’
Ndugu Wasikilizaji, inabainika wazi kutokana na hadithi tulizosoma na nyinginezo nyingi za kuiaminika ambazo zimepokelewa katika madhehebu zote mbili za Shia na Suni kwamba elimu kamili na isiyo na makosa yoyote ya Qur’ani Tukufu na ambayo ilirithiwa kutoka kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) imehifadhiwa kikamilifu kwa Maimamu watoharifu wa kizazi cha Mtume (saw) nao ndio kusudio halisi la walio na ilimu ya Kitabu.
Ni kwa msingi huo ndipo ikawa kushikamana nao (as) ni kushikamana sawasawa na Qur’ani Tukufu na hakika zake zote zilizokamilika na safi, zilizoteremshwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Ni kutokana na ukweli huu ndio maana Mtume Mtukufu (saw) akabana uongofu wa Waislamu na kushikamana kwao kikamilifu na kwa pamoja na Qur’ani Tukufu na Ahlul Beit wake kwa sababu kushikana na Qur’ani hakutimii kielimu ila kwa kushikamana na Ahlul Beit (as) ambao Mwenyezi Mungu amewapa elimu kamili ya kitabu chake chote.
Kwa natija hii muhimu ndio tunafikia mwisho wa kipindi hiki cha Maswali Yetu na Majibu ya Thaqalain ambacho kama kawaida kimekujieni kupitia Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuiri ya Kiislamu ya Iran kutoka mjini Tehran. Basi hadi juma lijalo panapo majaaliwa, tunakuageni nyote kwa kusema, Wassalaam Aleikum Warahmatullahi Wabarakatuh.