Jumapili, Septemba 25, 2016
-
William Faulkner
Leo ni Jumapili tarehe 23 Mfunguo Tatu Dhul-Hijjah mwaka 1437 Hijiria, mwafaka na Septemba 25, 2016 Miladia.
Siku kama ya leo miaka 119 iliyopita alizaliwa katika jimbo la Mississippi, Marekani mtaalamu wa fasihi na mwandishi wa Kimarekani kwa jina la William Faulkner. Faulkner hakukamilisha masomo yake ya juu na alianza kujishughulisha na kazi mbalimbali kwa ajili ya kuendesha maisha. Mwandishi huyo mashuhuri alianza kuandika hadithi mwaka 1925 baada ya kufahamiana na Sherwood Anderson mwandishi mwenzie wa Kimarekani. Katika hadithi zake Faulkner alikuwa akibainisha hali mbaya ya kijamii huko Marekani hususan ubaguzi wa rangi uliokuwa ukiwakabili raia weusi wa nchi hiyo. Riwaya za mwandishi huyo zimekuwa na taathira kubwa katika sekta ya uandishi wa sasa nchini Marekani. Mwaka 1950 mwandishi huyo alitunukiwa tuzo ya fasihi ya Nobel.
Siku kama ya leo miala 78 iliyopita, alifariki dunia mtaalamu mkubwa wa hadithi Ayatullah Haj Sheikh Abbas Qumi, mwandishi wa kitabu mashuhuri cha dua cha Mafatihul-Jinan. Sheikh Abbas Bin Muhammad Ridha Bin Abil-Qasim Qumi, ni mmoja wa maulama wakubwa wa karne ya 14 Hijiria huku akiwa mtaalamu mkubwa wa hadithi upande wa Kishia. Baada ya kuhitimu masomo yake ya msingi mjini Qum, mwaka 1316 Hijiria alifanya safari mjini Najaf, Iraq na kupata kusoma kwa maulama wakubwa wa zama hizo akiwemo Allamah Haj Mirza Hussein Nuri na kuanza kumsaidia kazi ya uandishi mwalimu wake huyo. Baada ya kufariki dunia mwalimu wake, alirejea mjini Qum na kuanza kujishughulisha na masuala ya dini sanjari na kuandika vitabu vikubwa. Katika umri wake aliweza kuandika makumi ya vitabu ambapo kila kimojawapo kina thamani kubwa katika ulimwengu wa Kiislamu. Moja ya vitabu vyake mashuhuri na vyenye kupewa umuhimu mkubwa na Waislamu ni kitabu cha dua za Ahlu Bayti wa Mtume (saw) cha Mafaatihul-Jinan. Kitabu kingine cha msomi huyo ni 'al-Anwaarul-Bahiyyah fii Tawaarikhul-Hujajul Ilaahiyyah,' 'al-Baaqiyaatus-Swaalihaat fi al-Ad iyat was Swalawaatil-Mustahabbaat' 'Safiinatul-Bihaar' 'Madiinatul-Hikami wal-Aathaar' 'Manaazilul-Aakhirat' na kadhalika.
Siku kama ya leo miaka 47 iliyopita, iliasisiwa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC). Jumuiya hiyo ni ya pili kwa ukubwa baada ya Umoja wa Mataifa kwa kuwa na nchi wanachama 57 katika mabara zaidi ya manne. Jumuiya hiyo inahesabiwa kuwa sauti ya ulimwengu wa Kiislamu yenye jukumu la kulinda maslahi ya Waislamu, kueneza moyo wa amani na kuratibu masuala ya Waislamu. Jumuiya hiyo iliundwa katika mkutano wa Kihistoria uliofanyika Rabat nchini Morocco tarehe 25 Septemba mwaka 1969 kama jibu la hatua ya Wazayuni wa Israel ya kuchoma moto Msikiti wa al Aqsa hiko Baitul Muqaddas.
Siku kama ya leo miaka 34 iliyopita, alifariki dunia Reza Mafi, msanii na hatibu mkubwa wa zama hizi. Mafi alizaliwa mjini Mash'had nchini hapa. Alipendelea sana fani ya kuhutubu ambapo alienda kujifunza fani hiyo kwa mwalimu wake I'tisami ambapo pia alijifunza fani ya uandishi wa hati nzuri. Aliendeleza fani hiyo kwa walimu wakubwa wa Iran na kutokea kuwa hatibu mkubwa na mchoraji mashuhuri nchini Iran. Athari za uchoraji wake hadi leo zinapatikana ndani na nje ya nchi hii. Maonyesho ya mwisho ya msanii huyo yalifanyika mwaka 1358 Hijiria Shamsia sawa na mwaka 1979 yaliyofanyika kwa ajili ya kuwakumbuka mashahidi wa njia ya uhuru mjini Tehran.
Siku kama ya leo miaka 25 iliyopita, alifariki dunia Ayatullah Haj Sayyid Mustafa Musawi Khvansar maarufu kwa jina la 'Kashif', mmoja wa maulama wakubwa wa nchini Iran na ulimwengu wa Kiislamu kwa ujumla. Sayyid Mustafa Musawi Khvansar alizaliwa mjini Qum. Alisoma elimu ya dini kwa Ayatullah Borujerdi na kufanikiwa kufikia daraja ya juu katika uwanja huo. Ameacha athari mbalimbali kama vile kitabu cha 'Tawdhihul-Masaail' 'Manaasiku Hajj' 'Izdiwaaj fil-Islami' na kadhalika.
Na siku kama ya leo miaka 13 iliyopita alifariki dunia Edward Said, mwandishi na mwanafikra wa Kipalestina kutokana na maradhi ya saratani. Said alizaliwa mwaka 1935 katika familia ya Kikristo. Alielekea Marekani kwa ajili ya kudumisha elimu akiwa na umri wa miaka 17 na akafanikiwa kupata shahada ya uzamivu katika Chuo kikuu cha Harvard. Kitu kilichompa umashuhuri zaidi Prof. Edward Said katika upeo wa kimataifa ni jitihada zake kubwa za kuwatetea wananchi wanaodhulumiwa wa Palestina bila ya kusita. Mwanafikra huyo mtajika alifikisha sauti ya kudhulumiwa wananchi wa Palestina katika masikio ya walimwengu kupitia makala na vitabu vyake. Ameandika vitabu vingi na muhimu zaidi ni kile alichokipa jina la Orientalism ambacho ndani yake anaeleza jinsi wataalamu wa masuala ya Mashariki wa Wamagharibi wanavyotumiwa kama wenzo wa wakoloni kwa ajili ya kuhalalisha uporaji wa mali na maliasili za mataifa ya mashariki mwa dunia.