Sep 29, 2016 02:42 UTC
  • Alhamisi, Septemba 29, 2016

Leo ni Alkhamisi tarehe 27 Dhulhija 1437 Hijria sawa na 29 Septemba 2016.

Leo tarehe 8 mwezi Mehr kwa mwaka wa Hijria Shamsia ni siku ya kumuenzi Jalaluddin Muhammad bin Bahauddin maarufu kwa jina la Maulawi, arifu na mshairi mkubwa wa Iran. Alizaliwa mwaka 604 Hijiria Shamsia katika mji wa Balkhi ambao zama hizo ulikuwa sehemu ya ardhi ya Iran baada ya muda akahamia katika mji wa Konya nchini Uturuki akiandamana na baba yake na baadaye kuelekea Syria kwa ajili ya masomo ya juu. Miongoni mwa vitabu muhimu zaidi vya Maulawi ni Mathnawi Maanawi, Fihi ma Fihi, Maktubat Maulana na Rubaiyat. Jalaluddin Rumi alifariki dunia tarehe 5 Jamadul Thani mwaka 672 akiwa na umri wa miaka 68 na kuzikwa katika mji wa Konya nchini Ituruki.

Siku kama ya leo miaka 746 iliyopita, aliaga dunia Sheikh Muslihuddiin Saadi Shirazi malenga, mshairi na mwalimu stadi wa tungo za mashairi na nathari wa Kifarsi. Baada ya kukipitisha kipindi cha utoto na kuinukia kwake katika mji alikozaliwa wa Shiraz nchini Iran, akiwa kijana, Saadi Shirazi aliamua kwenda katika mji wa Baghdad huko Iraq. Akiwa huko alisoma katika shule ya Nidhamiya na baadaye kufanya safari katika maeneo ya Sham, Hijaz, Roma na katika maeneo mengine. Katika safari zake hizo, malenga huyo mashuhuri alifanikiwa kufahamiana na jamii mbalimbali na kuona mengi yaliyoimarisha kipawa chake cha kutunga mashairi. Saadi Shirazi ni miongoni mwa malenga na washairi wakubwa katika ulimwengu wa Kiislamu. Saadi Shirazi ameandika vitabu kadhaa, muhimu zaidi ni kile cha tungo za mashairi cha Bustan na kitabu chake cha nathari cha Golestan.

Tarehe 29 Septemba miaka 115 iliyopita, alizaliwa mwanafizikia mashuhuri wa Italia Enrico Fermi katika mji wa Roma. Baada ya kukamilisha masomo ya chuo kikuu aliweza kuvumbua kanuni ya Mwendo wa Molekuli ya Gesi. Fermi alifanya uchunguzi kuhusu mabadiliko ya atomu na akafanikiwa kutengeneza betri ya atomu kwa kuipasua na kutoa nje nishati yake. Mwanafizikia huyo wa Italia alifariki dunia mwaka 1954.

Na siku kama ya leo miaka 114 iliyopita, alifariki dunia mwandishi wa Kifaransa, Emile Zola. Zola alizaliwa mjini Paris mwaka 1840. Alipata kuandika vitabu vingi katika elimu tofauti. Miongoni mwa vitabu mashuhuri vya mwandishi huyo wa Ufaransa ni "Therese Raquin” "Nana", "The Belly of Paris na "Germinal."