Ijumaa Oktoba 7, 2016.
Leo ni Ijumaa tarehe 5 Muharram 1438 Hijria sawa na Oktoba 7, 2016.
Miaka 88 iliyopita katika siku kama ya leo mwafaka na tarehe 16 Mehr mwaka 1307 Hijiria Shamsia, vikosi vya utawala Shah Pahlavi wa Iran vilivamia nyumba ya Ayatullah Muddares na kumpiga na kumjeruhi, kisha akahamishiwa nje ya mji wa Tehran baada ya mwanazuoni huyo kupinga udikteta wa Ridhakhan Pahlavi. Mwishowe Ayatullah Mudarres alibaidishwa katika mji wa Kashmar kaskazini mashariki mwa Iran na kuuawa shahidi na vikosi vya Ridhakhan mwaka 1316 Hijiria Shamsia akiwa katika mji huo.
Miaka 67 iliyopita katika siku kama hii ya leo, Ujerumani ya Mashariki iliasisiwa na kuwa na mfumo wa Jamhuri ya Kidemokrasia. Katika miezi ya mwishoni mwa Vita vya Pili vya Dunia, Shirikisho la Umoja wa Sovieti liivamia na kuikalia kwa mabavu ardhi ya Ujerumani ya Mashariki, na madola ya Magharibi yakadhibiti sehemu ya magharibi mwa nchi hiyo. Hata hivyo baadaye Umoja wa Sovieti ulijitoa katika Baraza la Makamanda wa Waitifaki baada ya kutofautiana na madola ya Magharibi juu ya namna ya kuiendesha nchi hiyo.
Siku kama ya leo miaka 29 iliyopita utawala wa Baath wa Iraq uliushambulia mji wa Sumar ulioko magharibi mwa Iran kwa kutumia silaha za kemikali. Raia wengi waliuawa shahidi katika mashambulizi hayo. Katika kipindi chote cha vita vya kulazimishwa vilivyoanzishwa na Iraq dhidi ya Iran utawala wa Saddam Hussein ulitumia mara nyingi silaha za kemikali dhidi ya maeneo ya raia nchini Iran. Mashambulizi hayo yameua shahidi au kujerihi karibu watu laki moja wakiwemo wanajeshi na raia wa kawaida wa Iran. Baadhi wa majeruhi wa mashambulizi hayo ya silaha za kemikali wangali wanasumbulkiwa na athari mbaya za silaha hizo hadi hii leo licha ya kupita miongo mitatu sasa baada ya kufanyika mashambulizi hayo.
Ni vyema kukumbusha hapa kuwa, nchi za Magharibi ndizo zilizoupa silaha za kemikali utawala wa Saddam ambazo ulizitumia dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Na tarehe7 Oktoba miaka 15 iliyopita sawa na tarehe 7 Oktoba 2001, Marekani iliivamia Afghanistan. Uvamizi huo ulifanyika kwa kisingizio cha kuliangamiza kundi la wanamgambo wa Al-Qaida ambao kwa mujibu wa Washington walihusika na tukio la Septemba 11 2001 nchini Marekani. Katika kipindi cha wiki kadhaa, ndege za kivita za Marekani, zilifanya mashambulizi dhidi ya ngome za kundi la Taliban ambalo katika kipindi hicho lilikuwa likidhibiti eneo kubwa la ardhi ya Afghanistan sambamba na kuliunga mkono kundi la Al-Qaida lililokuwa likiongozwa na Osama bin Laden. Mashambulizi hayo mazito ya Marekani yaliua na kujeruhi maelfu ya raia wasio na hatia wa Afghanistan huku wengine wakilazimika kuwa wakimbizi. Hata hivyo pamoja na Marekani kusaidiwa na muungano wa vikosi vya kaskazini mwa Afghanistan na kufanikiwa kuuangusha utawala wa Taliban, hadi leo haijaweza kumtia mbaroni Mulla Omar na viongozi wengine wa kundi hilo la Taliban.