Jumamosi, 15 Oktoba, 2016
Leo ni Jumamosi tarehe 13 Mfunguo Nne Muharram 1438 Hijria sawa na tarehe 15 Oktoba mwaka 2016 Miladia.
Siku kama ya leo miaka 25 iliyopita, nchi ya Bosnia Herzegovina ilijitangazia uhuru kutoka kwa Yugoslavia. Jamahuri ya Bosnia Herzegovina kijiografia inapatikana kusini mwa Ulaya ikipakana na nchi za Croatia na Yugoslavia kando ya Bahari ya Adriatic. Baada ya kumalizika Vita vya Kwanza vya Dunia Bosnia Herzegovina iliunganishwa na nchi ya Yugoslavia. Hata hivyo kufuatia harakati za kujitenga, Bosnia Herzegovina nayo ikiwa pamoja na Serbia, Slovenia na nchi nyingine ilijitenga na Yogoslavia na kujitangazia uhuru. ***

Miaka 38 iliyopita katika siku kama ya leo, kulitokea maafa makubwa katika Msikiti Mkuu wa mji wa Kerman kusini mwa Iran baada ya vikosi vya usalama vya utawala dhalimu wa Shah kuwashambulia waumini katika msikiti huo. Waumini hao walikuwa wamekusanyika kwa ajili ya kumbukumbu ya Arobaini ya mashahidi wa tarehe 17 Shahrivar 1357 Hijria Shamsia mjini Tehran. Waumini wengi waliuawa shahidi na kujeruhiwa katika shambulio hilo la kinyama. Tukio hilo lilipelekea kuibuka wimbi jipya na kubwa la malalamiko na upinzani wa wananchi wa Iran dhidi ya jinai za utawala wa Shah. ***

Na siku kama ya leo miaka 172 iliyopita alizaliwa mwanafalsafa wa Kijerumani Friedrich Wilhelm Nietzsche. Baada ya kuhitimu masomo, Nietzsche alianza kufundisha katika Chuo Kikuu cha Basel. Mwanafalsafa huyo alikuwa akipinga dini na misingi ya kimaadili na katika falsafa na mitazamo yake alikuwa akiamini nadharia ya "Superman", kwa maana ya mtu mwenye uwezo kupita kiasi. Nietzsche alikuwa akiamini kwamba, mtu mwenye uwezo kupita kiasi au Superman ni matokeo ya irada na matashi ya mwanadamu na huwa juu ya mema na mabaya yote. Mwanafalsafa huyo ameandika vitabu kadhaa ikiwa ni pamoja na Beyond Good and Evil, The Birth of Tragedy na Thus Spoke Zarathustra. Katika kipindi cha mwishoni mwa uhai wake Friedrich Wilhelm Nietzsche alipoteza mlingano wa kifikra na alifariki dunia mwaka 1900.