Hadithi ya Uongofu (31)
-
Hadithi ya Uongofu (31)
Ni wasaa na wakati mwingine wapenzi wasikilizaji wa kuwa nanyi katika kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu. Katika kipindi chetu kilichopita nilikunukulieni baadhi ya hadithi zinazohusiana na kutatua shida za watu na athari zinazopatikana kwa mtu anayefanya amali hiyo inayopendwa na Mwenyezi Mungu. Sehemu ya 31 ya kipindi hiki juma hili itazungumzia baadhi ya nukta ambazo anapaswa kuzizingatia yule anayefanya amali hii yaani ya kumsaidia mtu na kutatua shida na matatizo yake.
Ikhlasi ni sharti muhimu kabisa la kutakabaliwa ibada na taklifu za kidini. Ikhlasi maana yake ni kufanya jambo fulani au amali fulani kwa ajili ya Mwenyezi Mungu tu na kwa ajili ya kutaka radhi za Mola Muumba. Kwa maana kwamba, sio kwa ajili ya kutaka kusifiwa, ria au kujionesha kwa watu. Katika suala la kusaidia watu na kutatua shida na kuwakidhia hawaiji zao pia, sharti muhimu la kutakabaliwa amali hiyo ni kulifanya hilo kwa ikhlasi na kwa nia safi kabisa yaani kwa ajili ya Mwenyezi Mungu na kwa ajili ya kutaka radhi Zake. Hivyo basi kama mtu atamsaidia Mwislamu mwenzake na kumtatulia shida yake, lakini akawa anafanya hilo kwa ajili ya kutafuta umashuhuri, ria, kujionesha au kutaka kunufaika kisiasa au kijamii, amali yake hiyo haina thamani yoyote ile mbele ya Mwenyezi Mungu. Kazi ambayo inafanyika na kufanywa kwa ajili ya Mwenyezi Mungu ina ishara zake. Moja ya ishara hizo ni mtu aliyefanya amali hiyo kutotaka kusifiwa na watu au kupongezwa kwa amali yake hiyo. Imam Ja'afar Swadiq (a.s) anasema kuwa: Kazi yenye ikhlasi ndani yake ni ile ambayo hutaki kusifiwa isipokuwa na Mwenyezi Mungu. Katika hadithi Qudsi ya Mtume saw amenukuliwa kauli ambayo ni kutoka kwa Mwenyezi Mungu akisema kwamba:
"Mimi ni mshirika bora kabisa. Kila mtu ambaye katika amali yake ataniletea mshirika, basi amali yote iliyofanywa ninamuachia mshirika wangu. Na sikubali amali yoyote isipokuwa ile ambayo imefanywa kwa ajili yangu tu."
Kuheshimiwa na kuwa na heshima baina ya watu ni moja ya mambo ya dharura katika maisha ya kijamii. Ni kwa kuzingatia uhakika huo ndio maana dini tukufu ya Kiislamu imelipa umuhimu mkubwa suala la kulindwa na kuhifadhiwa heshima ya waumini kiasi kwamba, waumini wanaamrishwa na kutakiwa walinde heshima zao na inawataka wengine walinde na kuhifadhi heshima na itibari za waumini.
Tunakiendeleza kipindi chetu cha juma hili kwa kisa kifuatacho:
"Siku moja bwana mmoja miongoni mwa Waislamu wa Madina alikuwa akidaiwa na kadiri alivyofanya hakuweza kulipa deni lake. Katika upande mwingine, mwenye pesa yake, yaani mtu aliyekuwa amemkopoesha bwana yule alikuwa akidai pesa yake na akisisitiza kulipwa haraka iwezekanvyo. Bwana mdaiwa ambaye alikuwa amekosa raha kutokana na mwenye deni kumuandama, aliamua kumuendea Imam Hussein bin Ali bin Abi Twalib (a.s). Alipofika kwa Imam Hussein kabla hata hajatamka kitu, Imam akawa amefahamu kwamba amekuja kwa ajili ya shida. Ili bwana yule asione haya na soni wakati wa kueleza shida yake na ili heshima na itibari yake ihifadhiwe, Imam alimtaka bwana yule aandike shida yake katika barua. Bwana yule akaandika barua akisema: Ewe Abu Abdillah! fulani ananidai dinari 500 na anasisitiza nimlipe deni lake, nakuomba uzungumze naye anipe muhula mpaka nitakapokuwa na pesa ili niweze kumlipa deni lake. Baada ya Imam Hussein (a.s) kusoma barua ya bwana yule, alielekea nyumbani kwake na akarejea akiwa na mfuko wenye dinari elfu moja na kisha baada ya kumpatia bwana yule mfuko ule akamwambia: Chukua dinari mia tano katika pesa hizi na ulipe deni lako; na dinari mia tano nyingine zilizobakia fanyia mambo yako mengine ya kimaisha na usimueleze mtu yeyote shida yako isipokuwa watu watatu: Mtu wa kwanza ni muumini na mwenye kushikamana na dini, ambaye dini ni mlinzi wake; mtu wa pili ni muungwana na mtu wa tatu ni yule ambaye asili na nasaba ya familia yake inajulikana yaani familia inayosifika na kutambulika kwa kuheshimu thamani za kimaadili na kiakhlaqi. Watu hawa wanatambua kwamba, wewe hauko tayari kupoteza heshima na itibari yako kwa sababu ya kuhitajia kwako, hawa ni watu wenye kuhifadhi heshima yako na ni wenye kukutekelezea shida yako."
Nukta ya kuzingatia wakati wa kuwasaidia watu wengine ni hii kwamba, msaidiaji anapaswa kujiepusha na masimbulio na masimango kwani kufanya hivyo huondoa kabisa thamani ya amali aliyofanya mtu huyo ya kumsaidia mwenziwe mwenye shida. Inaelezwa katika hadithi kwamba, kama mmefanya amali ya kupendeza, basi isahauni kwani yamkini kwa kuikumbuka mkafanya masimbulizi na hivyo mkapoteza thamani na itibari ya amali yenu hiyo ya kheri.
Mwenyezi Mungu katika Qur'ani Tukufu anawataka waumini wasiharibu sadaka na mali wanazotoa kusaidia watu kwa masimango na masimbulizi. Anasema katika aya ya 264 ya Surat al-Baqarah kwamba:
Enyi mlioamini! Msiharibu sadaka zenu kwa masimbulizi na maudhi, kama anayetoa mali yake kwa kuwaonyesha watu, wala hamuamini Mwenyezi Mungu wala Siku ya Mwisho. Basi mfano wake ni kama mfano wa jabali ambalo juu yake pana udongo, kisha likapigwa na mvua kubwa, ikaliacha tupu. Basi hawatakuwa na uweza wowote kwa walivyochuma. Na Mwenyezi Mungu hawaongoi watu makafiri.
Hivyo basi kutoa msaada ambao unaambatana na masimango ni mithili ya mvua kali ambayo huja na kusomba amali ya akheri aliyoifanya mtu lakini ikawa imefuatiwa na masimbulizi.
Katika aya ya 265 ya Surat al-Baqarah Mwenyezi Mungu anabainisha na kueleza athari za amali anayoifanya mtu na ambayo ikawa ni ya ikhlasi na kwa ajili tu ya kutaka radhi za Mwenyezi Mungu. Aya hiyo inasema:
Na mfano wa wale wanaotoa mali zao kwa kuitafuta radhi ya Mwenyezi Mungu na kuzipa nguvu roho zao ni kama mfano wa bustani iliyo mahali pa juu, ikaifikia mvua kubwa na ikaleta mazao yake maradufu; na hata kama haifikiwi na mvua kubwa basi manyunyu hutosha. Na Mwenyezi Mungu anayaona mnayoyatenda.
Jambo jingine lililousiwa na kutiliwa mkazo katika kuwasaidia watu na kuwatatulia shida zao ni kuharakisha kufanya hivyo. Kikawaida, kama haraka haraka huwa haina baraka na kwa mujibu wa mafundisho ya Uislamu kufanya mambo kwa haraka ni miongoni mwa amali ambazo hazipendezi isipokuwa fursa iliyopatikana kwa ajili ya kufanya jambo la kheri. Kufanya haraka katika kutatua shida ya mtu kuna umuhimu katika pande kadhaa. Muhimu zaidi ni kuwa, yamkini fursa iliyopatikana isipatikane tena. Imam Ali bin Abi Twalib (a.s) anazishabiisha fursa mwafaka kwa ajili ya kufanya jambo na upepo wa msimu wa kipupwe ambao upo katika hali ya kupita na kwenda zake. Imam Ja'afar Swadiq (a.s) anasema kuwa, baba yangu Imam Muhammad Baqir (a.s) alikuwa akisema: Madhali umekata shauri kufanya jambo la kheri, basi harakisha kulifanya, kwani hujui baadaye nini kitatokea.
Kwa leo tunakomea hapa wapenzi wasikilizaji, tukutane tena wiki ijayo. Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh...