Oct 23, 2016 01:01 UTC
  • Jumapili, Oktoba 23, 2016

Leo ni Jumapili tarehe 21 Muharram mwaka 1438 Hijria, sawa ya Oktoba 23 mwaka 2016.

Siku kama ya leo miaka 1008 iliyopita alifariki dunia, Abu Naeem Hassan Bib Abdillah Isfahani, mtaalamu wa hadithi na alimu mkubwa wa Iran. Alizaliwa mwaka 336 Hijiria mjini Isfahani, katikati mwa Iran. Kwa kuzingatia kuwa baba na mama yake walikuwa wasomi, Abu Naeem Hassan Bib Abdillah Isfahani alishikama na njia yao kielimu ambapo alitokea kuwa msomi mtajika wa zama hizo. Hata hivyo shakhsia huyo hakuishia hapo na badala yake alifanya safari katika maeneo tofauti ya dunia kwa ajili ya kuongeza maarifa na ujuzi wa kielimu. Miongoni mwa miji aliyofanya safari ni pamoja na Khorasan, Baghdad, Kufa, Iraq, Makkah na Sham. Miongoni mwa vitabu vya msomi huyo ni pamoja na 'Hilyatul-Awliyaai,' 'Dalaailun-Nubuwwah' na 'Kitaabul-Mahdi.'

Siku kama ya leo miaka 712 iliyopita, alifariki dunia Hassan Bin Yusufu Bin Mutwahhari Hilli, maarufu kwa jina la Allamah Hilli, faqihi na msomi mashuhuri wa Kiislamu. Allamah Mutwahhari Hilli alikuwa mkazi wa mji wa Hillah, moja ya miji mashuhuri ya nchini Iraq, huku baba yake akiwa ni mmoja wa wataalamu wa sharia za Kiislamu wa zama hizo. Akiwa mdogo Hassan Bin Yusufu Bin Mutwahhari Hilli alijifunza Qur'ani na elimu ya dini ya Kiislamu kutoka kwa baba yake mazazi na kisha kwa maulama wakubwa wa zama hizo kama vile Khojah Nasird-Din Toosi. Haukupita muda mrefu mara shakhsia huyo akafikia daraja la ijtihadi. Ustadh Shahid Mutwahhari, mmoja wa maulama wakubwa wa nchini Iran anamuelezea Hassan Bin Yusufu Bin Mutwahhari Hilli kama ninavyonukuu: "Allamah Hilli, ni mmoja wa wasomi wakubwa wa zama hizo. Alitabahari katika fiqhi, theolojia, mantiki, falsafa na elimu ya wapokezi wa hadithi huku akiandika pia vitabu vingi vinavyokaribia 100…" Mwisho wa kunukuu. Kitabu cha 'Nahjul-Fuqahaai' 'Nahjul-Iman fi Tafsiril-Qur'an Majid' na 'Muntahal-Matwaalib' ni miongoni mwa athari za Hassan Bin Yusufu Bin Mutwahhari Hilli.

Siku kama ya leo miaka 144 iliyopita, alifariki dunia Theophile Gautier, malenga na mwandishi wa Kifaransa. Gautier alizaliwa mwaka 1811 na kuhitimu masomo yake huko Paris, mji mkuu wa Ufaransa. Theophile Gautier kwa muda fulani alikuwa mwandishi wa gazeti na alikuwa na hamu kubwa ya kuwa mchoraji au mwanamuziki. Lakini hatimaye alijifunza fasihi hususan mashairi. Ameandika  vitabu kadhaa katika uwanja huo ambavyo hii leo vinapatikana katika maktaba za Ulaya.

Siku kama ya leo miaka 108 iliyopita aliuawa shahidi na majasusi wa Urusi ya zamani msomi mwanamapambano Allamah, Mirza Ali Thiqatul-Islam Tabrizi. Alikuwa na ushawsihi katika harakati za kupigania utawala wa kitaifa wa wananchi wa Azerbaijan Iran. Vibaraka wa Urusi kwa kuungwa mkono na utawala wa kidikteta wa wakati huo nchini Iran wa Mohammad Ali Shah Qajar, waliuvamia kijeshi mji wa Tabriz. Hata hivyo walikabiliana na mapambano ya wakazi wa mji huo waliokuwa wanaongozwa na Thiqatul-Islam Tabrizi na baada ya mapigano makali askari hao wa Urusi ya zamani walishindwa vibaya na kuamua kuondoka katika mji huo. Kwa bahati mbaya kulijiri uhaini ambapo ulienda sambamba na kuweka chini silaha wanamapambano huku siku ya pili jeshi hilo likivamia kwa mara nyingine mji huo na kutekeleza jinai kubwa dhidi ya wakazi wake akiwemo Thiqatul-Islam Tabrizi.

Siku kama ya leo miaka 74 iliyopita, vita vya kihistoria vilivyopewa jina la al-Alamein vilitokea katika mji wenye jina  hilohilo huko kaskazini mwa Misri kati ya wanajeshi wa Uingereza na jeshi la Manazi wa Ujerumani. Vita hivyo vilimalizika baada ya kushindwa jeshi la Ujerumani, japokuwa mapigano kati ya pande hizo mbili yaliendelea katika maeneo mengine ya kaskazini mwa Afrika. Amani kamili ilipatikana katika maeneo hayo baada ya kushindwa kikamilifu jeshi la Ujerumani wakati wa Vita vya Pili vya Dunia.

Na siku kama ya leo miaka 69 iliyopita alizaliwa Abdel Aziz al-Rantisi, kiongozi wa harakati ya mapambano ya Palestina. Kuanzia vita vya mwaka 1948 Al-Rantisi aliishi kwa kipindi cha miezi sita yeye na familia yake eneo la Ukanda wa Gaza katika kambi ya wakimbizi ya Khan Yunus. Baada ya kuuawa shahidi na utawala haramu wa Israel Ahmed Yassin, kiongozi wa harakati ya HAMAS, uongozi wa harakati hiyo ulimkabidhi jukumu la uongozi huo Abdel Aziz al-Rantisi, huku akiwa na umri wa miaka 26. Mwanamapambano huyo aliuawa shahidi tarehe saba Aprili mwaka 2004 na helikopta ya jeshi la Israel akiwa na watu wengine watatu na akiwa na umri wa miaka 57.