Oct 24, 2016 00:06 UTC
  • Jumatatu, Oktoba 24, 2016

Leo ni Jumatatu tarehe 22 Mfunguo Nne Muharram 1438 Hijria sawa na Oktoba 24, 2016.

Tarehe 24 Oktoba miaka 71 iliyopita uliundwa Umoja wa Mataifa na kuchukua nafasi ya Jumuiya ya Mataifa. Wawakilishi wa mataifa yaliyoafikiana katika Vita Vikuu vya Pili vya Dunia, yaani Marekani, Urusi, Uingereza na Ufaransa, waliandaa mazingira ya kuundwa umoja huo; na hatimaye katika mkutano uliofanyika San Francisco, Marekani, wawakilishi kutoka nchi 50 duniani walipitisha sheria za kuundwa umoja huo. Ijapokuwa umoja huo umefanikiwa katika baadhi ya mambo, lakini kuwepo haki ya veto kwa baadhi ya nchi ambazo ni Marekani, Russia, Uingereza, Ufaransa, na China kunalifanya Baraza la Usalama la umoja huo kufuata kibubusa siasa za nchi zenye haki ya kupiga kura ya turufu, na hasa Marekani.

Bendera ya Umoja wa Mataifa

Tarehe 24 Oktoba yaani siku kama hii ya leo miaka 52 iliyopita, nchi ya Zambia ilipata uhuru kutoka kwa mkoloni Mwingereza. Zambia ilianza kutawaliwa na Uingereza mwaka 1888, na katika kipindi cha muongo mmoja tokea mwaka 1953 hadi 1963, Zambia ikiwa pamoja na Nyasaland na Southern Rhodesia, ziliunda Shirikisho la Afrika ya Kati. Baada ya kusambaratika shirikisho hilo, hatimaye mwaka 1964, Northen Rhodesia ilijipatia uhuru kwa jina la Zambia.

Bendera ya Zambia

Siku kama ya leo miaka 24 iliyopita, alifariki dunia Abul-Qasim Halat, malenga, mchekeshaji na mtaalamu wa fani ya tarjama nchini Iran. Akiwa na umri wa miaka 16 Halat alianza kusoma mashairi na kuwa hodari mkubwa katika uwanja huo. Tarjama ya maneno ya Mtukufu Muhammad (saw) na Imam Ali (as), ni miongoni mwa athari zenye thamani kubwa za Abul-Qasim Halat. Mbali na vitabu hivyo, Halat aliandika majmui ya mashairi katika fani mbalimbali, baadhi zikihusu masuala ya akhlaqi na Irfani. Aidha Abul-Qasim Halat alikuwa mtaalamu pia katika lugha nne za Kifarsi, Kingereza, Kifaransa na Kiarabu.

Abul-Qasim Halat

Tarehe 24 Oktoba miaka 87 iliyopita ulianza mgogoro mkubwa wa kiuchumi wa Marekani unaojulikana kwa jina la Wall Street. Kimsingi Wall Street ni mtaa mashuhuri mjini New York ambao kutokana na kuwa na taasisi nyingi kubwa za kifedha na kibenki unatambuliwa kuwa kituo muhimu sana cha kiuchumi cha Marekani. Kituo hicho cha kiuchumi kilikumbwa na mgogoro mkubwa wa kifedha wakati wa Vita vya Kwanza vya Dunia na baada yake. Oktoba 24 mwaka 1929 janga kubwa la kifedha liligubika makao ya hisa ya Marekani huko Wall Street na kupelekea kukosa kazi zaidi ya wafanyakazi milioni 13 wa Marekani, njaa kali, kufilisika kwa viwanda na mabenki na mamilioni ya watu kupoteza makazi na nyumba zao.

Wall Street

Siku kama ya leo miaka 978 iliyopita alifariki dunia mmoja wa wasomi wakubwa wa Kiislamu, Sheikh Muhammad bin Hassan Tusi, ambaye ni mashuhuri kwa jina la Sheikhul Twaaifa. Sheikh Tusi alizaliwa katika mji wa Tus kaskazini mwa Iran na akaelekea Iraq kwa ajili ya kutafuta elimu ya juu baada ya kukamilisha elimu ya msingi. Alipata elimu kwa wanazuoni mashuhuri wa Iraq na miaka kadhaa baadaye akaweka msingi wa chuo kikuu cha kidini cha Najaf. Kituo hicho cha kidini kina historia ya miaka elfu moja na ni moja ya vituo muhimu mno vya elimu ya Kiislamu. Sheikh Tusi ameandika vitabu vingi sana katika taaluma mbalimbali. Miongoni mwa vitabu mashuhuri vya mwanazuoni huyo wa Kiislamu ni tafsiri ya Qur'ani tukufu ya al Tibyan na vitabu vya hadithi na fiqhi vya al Istibsar na al Tahdhiib.

Sheikh Muhammad bin Hassan Tusi