Oct 26, 2016 06:07 UTC
  • Jumatano, 26 Oktoba, 2016

Leo Jumatano tarehe 24 Muharram 1438 Hijria sawa na Oktoba 26, 2016.

Siku kama ya leo miaka 21 iliyopita maajenti wa shirika la ujasusi la Israel Mossad walifanya mauaji ya kigaidi dhidi ya Katibu mkuu wa zamani wa Harakati ya Jihad Islami ya Palestina, Dakta Fathi Shiqaqi, akiwa huko Malta. Shiqaqi alizaliwa mwaka 1951 katika kambi ya wakimbizi wa Kipalestina katika Ukanda wa Gaza. Alihitimu masomo ya udaktari na kufanya kazi katika hospitali moja ya Baitul Muqaddas. Alianzisha harakati za mapambano dhidi ya utawala ghasibu wa Israel akiwa bado kijana. Mwaka 1979 Dakta Shiqaqi alikamatwa na kusweka jela nchini Misri kwa sababu ya kuandika kitabu kuhusu harakati za Imam Ruhullah Khomeini na ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran. Dakta Shuqaqi aliitangaza Siku ya Kimataifa ya Quds iliyoainishwa na Imam Khomeini, kuwa ni siku ya kuhuisha Uislamu na mapambano ya jihadi dhidi ya Wazayuni huko Palestina.

Dakta Fathi Shiqaqi

Tarehe 26 Oktoba miaka 22 iliyopita mfalme wa zamani wa Jordan Hussein na Waziri Mkuu wa zamani wa Israel Yitzhak Rabin walitia saini makubaliano eti ya amani. Mkataba huo ulishinikizwa na Marekani kwa ajili ya kile kilichotajwa na jitihada za kuanzisha mapatano kati ya Waarabu na Israel.

Mfalme Hussein wa Jordan na Waziri Mkuu wa israel, Yitzhak Rabin 

Na miaka 69 iliyopita katika siku inayosadifiana na hii ya leo, eneo la kiistratejia la Jammu na Kashimir liliunganishwa na India baada ya nchi hiyo kupata uhuru kutoka kwa mkoloni Muingereza na Pakistan kujitenga na India. Ilipangwa kuwa, eneo al Jammu na Kashmir lenye wakazi wengi Waislamu litajiunga na Pakistan lakini mtawala wa eneo hilo akichochewa na India na Uingereza, aliamua kuliunganisha na India na kupuuza matakwa ya wananchi. Baada ya kutangazwa habari hiyo Pakistan ililishambulia eneo hilo na kutwaa sehemu ya Jammu na Kashmir. Tangu wakati huo hadi sasa India na Pakistan zimepigana vita mara mbili juu ya umiliki wa eneo al Jammu na Kashmir na hitilafu za pande hizo mbili zingali zinaendelea.

Jammu na Kashimir

 

Tags