Oct 29, 2016 02:44 UTC
  • Jumamosi, 29 Oktoba, 2016

Leo ni Jumamosi tarehe 27 Mfunguo Nne Muharram 1438 Hijria mwafaka na tarehe 29 Oktoba mwaka 2016 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 9 iliyopita yaani tarehe 9 Aban 1386 Hijria Shamsia, Qeysar Aminpour mshairi mwanamapinduzi wa Iran aliaga dunia akiwa na umri wa miaka 48. Qeysar Aminpour alizaliwa katika mji wa Gotvand katika mkoa wa Khuzestan kusini mwa Iran. Alihitimu shahada ya uzamivu katika Chuo Kikuu cha Tehran kwenye taaluma ya lugha na fasihi ya Kifarsi. Qeysar Aminpour alikuwa na kipaji cha hali ya juu katika utunzi wa mashairi.

Miaka 36 iliyopita katika siku kama ya leo kulingana na kalenda ya Hijria Shamsia, alikufa shahidi Muhammad Hussein Fahmide mwanafunzi na kijana basiji. Jina la Muhammad Hussein Fahmideh limebakia katika kumbukumbu za wananchi wa Iran. Fahmideh ni shujaa wa kukumbukwa daima ambapo alishiriki katika vita vya kichokozi vya vilivyoanzishwa na utawala wa wakati huo wa dikteta Saddam Hussein wa Iraq dhidi ya Iran akiwa na umri wa miaka 13 tu. Licha ya umri wake mdogo Fahmideh aliweza kuleta hamasa kubwa na kuwa nembo ya kusimama kidete mbele ya wavamizi. Imam Khomeini MA mwanzishi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alimtaja shahidi Fahmideh kuwa ni kiongozi. Hii leo shahidi Fahmideh ni kigezo cha vijana chipukizi na wanafunzi.

Katika siku kama ya leo miaka 60 iliyopita, askari jeshi wa utawala wa Kizayuni wa Israel walishambulia Peninsula ya Sinai iliyoko Misri. Mashambulio hayo yalianza baada ya Rais wa wakati huo wa Misri Gamal Abdul Nassir kutaifisha mfereji wa Suez. Siku mbili baada ya mashambulio hayo, Uingereza na Ufaransa zilipeleka majeshi yao pembezoni mwa mfereji huo kwa lengo la kuusaidia utawala ghasibu wa Israel. Mnamo mwaka 1957 majeshi vamizi ya Ufaransa, Uingereza na utawala haramu wa Israel yaliondoka katika ardhi ya Misri kufuatia mashinikizo ya fikra za waliowengi, madola mengi ya Magharibi na upatanishi wa Umoja wa Mataifa.

Miaka 60 iliyopita katika siku kama ya leo, katika jinai yao nyingine, Wazayuni waliwauwa kwa umati wakazi wa kijiji cha Kafr Qasim huko Palestina. Wanajeshi wa utawala wa Kizayuni walitangaza utawala wa kijeshi katika kijiji hicho. Wanajeshi wa utawala wa Kizayuni waliwauwa kwa umati wanaume, wanawake na watoto madhlumu wa Palestina wasiopungua 49 na kujeruhi makumi ya wengine huko Kafr Qasim.

Siku kama ya leo miaka 83 iliyopita alifariki dunia Léon Charles Albert Calmette mgunduzi wa chanjo ya BCG. Albert Calmette alikuwa tabibu mtajika na mahiri wa Kifaransa ambaye alihitimu masomo yake katika Chuo Kikuu cha Paris. Chanjo ya B.C.G hutumika kukinga maambukizi ya ugonjwa wa kifua kikuu au TB. Kugunduliwa chanjo hiyo kumepunguza vifo vya watu wanaopatwa na ugonjwa wa TB duniani kote.

Na katika siku kama ya leo miaka 93 iliyopita, mfumo wa utawala wa serikali ya jamhuri uliasisiwa nchini Uturuki kwa uongozi wa Rais Mustafa Kemal mashuhuri kwa jina la Ataturk. Kemal Ataturk aliiongoza kidikteta nchi hiyo kwa muda wa miaka 15 na kufanya hujuma za kufuta sheria, nembo pamoja na matukufu ya Kiislamu na wakati huo huo, kueneza utamaduni na nembo za Kimagharibi nchini humo. Hata baada ya kufariki dunia kiongozi huyo aliyekuwa na uadui na Uislamu mnamo mwaka 1938, njama hizo dhidi ya Uislamu nchini Uturuki ziliendelezwa na wafuasi wake. ***