Ulimwengu wa Michezo, Okt 31
Ufuatao ni mkusanyiko wa matukio muhimu ya spoti kutoka kila kila dunia ndani ya siku saba zilizopita.
Iran bingwa wa Mashindano ya Dunia ya Karate
Timu ya karate wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeibuka ya kwanza katika duru ya 23 ya Mashindano ya Kimataifa ya Karate nchini Austria kwa kutia kibindoni jumla ya medali tano katika fainali dhidi ya Japan Jumapili. Medali ya dhahabu ilinyakuliwa na Amir Mehdizadeh katika kitengo cha wanakarate wa kiume wenye kilo zisizozidi 60 mtindo wa kumite, baada ya kumzidi maarifa Geoffrey Berens wa Uholanzi, katika mgaragazano wa fainali Jumamosi, ugani TipsArena, mjini Linz, kaskazini magharibi mwa nchi.
Sajjad Ganjzadeh aliipa Iran dhahabu ya pili baada ya kutamalaki mchezo kati yake na raia wa Morocco, Ashraf Ouchen, kitengo cha wenye kilo zaidi ya 84 upande wa wanaume. Medali za shaba za Jamhuri ya Kiislamu zilinyakuliwa na Ali Asghar na Zabihollah Porsheib katika safu ya wanaume wenye uzani wa kilo zisizozidi 75 na 85 kwa utaratibu huo. Hamideh Abbasali aliipa Iran medali nyingine ya shaba katika safu ya wanawake wenye uzito wa kilo zaidi ya 68, mtindo wa kumite. Duru ya 23 ya mashindano hayo yajulikanayo kama Karate World Championships yalifungua pazia lake Oktoba 25 na kumalizika Oktoba 30, kwa kuwaleta pamoja makarateka 2000 kutoka nchi 135.
UCI: Timu ya waendesha baiskeli ya Iran bora Asia
Habari kutoka Shirikisho la Kimataifa la Mchezo wa Kuendesha Baiskeli UCI zinasema kuwa, timu ya taifa ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ya mchezo huo ndiyo timu bora zaidi barani Asia. Kwa mujibu wa orodha mpya ya kila mwezi ya shirikisho hilo, Iran imeibuka kidedea kwa kuzoa jumla ya pointi 1,587 huku Kazakhstan ikiibuka ya pili kwa kupata alama 1,451.
Japan na Korea Kusini zimeibuka ya tatu na ya nne kwa usanjari huo, kwa kujikusanyia pointi 884 na 718. Wakati huo huo, klabu ya waendesha baiskeli wa Iran ya Pishgaman Kavir ya Yazd imeteuliwa kuwa klabu bora barani Asia, kwa pointi 915 ikifuatwa na klabu nyingine ya hapa nchini ya Tabriz Shahdari yenye pointi 884.
Kombe la Shirikisho Afrika
Licha ya kulamizishwa sare, klabu ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, imejiweka kwenye mazingira mazuri ya kutwaa Kombe la Shirikisho barani Afrika (Confederation). Mazembe ililazimishwa sare ya bao 1-1 na klabu ya Mouloudia Bejaia ya Algeria, katika duru ya kwanza ya mechi za kutinga fainali. Bao hilo la pekee la TP Mazembe lilifungwa na kiungo Jonathan Bolingi, kwenye kipute cha Jumamosi, kupitia mkwaju wa Penati.
Nahodha wa klabu ya Bejaia, Faouzi Yahya aliisawazishia timu yake bao katika kipindi cha pili, na kuipa matumaini timu yake itakaposafiri kwenda DRC. Fainali ya pili ya Kombe la Shirikisho itapigwa juma lijalo mjini Lubumbashi katika dimba la nyumbani la klabu ya Mazembe la Kamalondo.
Masumbwi: Mchina ala kichapo kutoka kwa Mtanzania
Mwanasumbwi wa ndondi za kulipwa nchini Tanzania, Abdallah Pazi almaarufu Dulla Mbabe alimuonyesha kivumbi hasimu wake Mchina, Chengbo Zheng katika pambano la kimataifa la WBO lililopigwa katika ukumbi wa Diamond Jubilee jijini Dar es Salaam. Katika hali ambayo wengi walidhani pambano hilo litakuwa na ushindani mkali, lakini Dulla Mbabe alionyesha ubabe wake kwenye uga wa masumbwi kwa kumgaragaza bingwa huyo wa China. Dulla alimsogeza Zheng kwenye kona na kummiminia ngumi nne mfululizo ambazo zilimdhoofisha asiweze kuendelea pambano likaishia hapa. Akizungumza baada ya pambano hilo, Dulla Mbabe alisema kuwa mpinzani wake ni bondia mzuri, lakini alimzidi kutokana na kujiandaa vizuri na kuimarisha mbinu za mchezo. Pambano lililofaa kutangulia la Cosmas Cheka dhidi ya Jason Bedemen wa Afrika Kusini lilikosa kufanyika baada ya mwanasumbwi huyo wa Afrika Kusini kugoma kupanda ulingoni akidai kuwa amebadilishiwa bondia.
Ligi ya Soka ya EPL
Michuano ya Ligi Kuu ya Soka ya Uingereza iliendelea kuroroma mwishoni mwa wiki huku mchuano kati ya Arsenal na Sunderland ukiteka fikra za wengi. Licha ya kuchezea nyumbani, vijana wa Sunderland walikubali kichapo cha mabao 4-1. Gunners walikuwa wa kwanza kucheka na nyavu katika dakika ya 19, kupitia kiungo Alexis Sánchez, baada ya kuandalia pasi safi na Oxlade-Chamberlain, bao lililoonekana kuwa la kipekee katika kipindi cha kwanza.
Sunderland hata hivyo katika kipindi cha pili walifanya mambo kuwa 1-1 kunako dakika ya 65 kupitia mkwaju wa penalti uliopigwa na Jermain Defoe. Baada hilo liliwachochea Wabeba Bunduki wafanye mabadiliko zikiwa zimesalia dakika 20 hivi zimalizike dakika 90 za ada. Kiungo Olivier Giroud ambaye aliingia kuvaa viatu vya Alex Iwobi aliipa Gunners bao la pili chini ya dakika 3 baada ya kuingia uwanjani na nguvu mpya. Dakika 5 baadaye Giroud aliongeza bao la tatu katika dakika ya 76, ambapo alifunga kwa kichwa huku Sanchez akifunga la mwisho dakika mbili baadaye. Ushindi huo umeifanya Arsenal ikwee kileleni mwa jedwali la EPL kwa sasa, ikiwa na pointi 23. Kwengineko, Manchester United licha ya kuupiga nyumbani Old Trafford walishinda kufurukuta mbele ya Burnley na kulazimishwa suluhu ya 0-0. Michuano mingine ya Ligi ya Premier ilishuhudia Middlesbrough ikiitandika Bournemouth mabao 2-0 wakati ambapo mabingwa watetezi Leicester walikuwa wakilazimishwa are ya bao 1-1 na Tottenham. Man City waliibamiza West Brom mabao 4-0 wakati Hull City ilikuwa ikipokea kichapo cha bao 1-0 kutoka Watford. Liverpool ambayo iliigaragaza Crystal Palace mabao 4-2, inazidi kubabana kileleni mwa ligi ikiwa na pamoja na Gunners na Man City zikiwa na alama 23 kila mmoja, ingawa zinatofautiana kwa idadi ya mabao. Chelsea ambayo iliilaza Southampton nyumbani Hampshire mabao 2-0 kwa sasa imeridhika na nafasi ya nne kwenye msimamo wa ligi ikiwa na pointi 22 huku Tottehman ikifunga orodha ya tano bora kwa sasa ikiwa na alama 20.
……………………………….TAMATI………………………….