Jumatatu tarehe 31 Oktoba 2016
Leo ni Jumatatu tarehe 29 Muharram 1438 Hijria sawa na 31 Oktoba 2016.
Siku kama ya leo, miaka 535 iliyopita alifariki dunia Muhammad Heravi, mwanahistoria wa Waislamu huko mjini Herat, magharibi mwa Afghanistan ya leo. Heravi, alizaliwa katika familia maarufu mjini Balkh, kaskazini mwa nchi hiyo lakini aliishi zaidi umri wake wote katika mji wa Herat. Kutokana na elimu yake kubwa, alipewa heshima na mazingatio makubwa na Ali-Shir Nava'i, waziri mwanasayansi wa silsila ya watawala wa Mughal, ambaye alikuwa akiwaheshimu sana wasomi na wanazuoni. Kitabu mashuhuri zaidi cha mwanazuoni huyo ni Tarikh Raudhati Safaa kinachochunguza historia ya dunia tangu kuumbwa kwake hadi zama za msomi huyo.
Tarehe 31 Oktoba 1984 yaani miaka 32 iliyopita, aliuawa Bi. Indira Gandhi, Waziri Mkuu wa wakati huo wa India. Mauaji hayo yalifanywa na walinzi wawili wa kiongozi huyo ambao walikuwa Masingasinga. Masingasinga hao walifanya mauaji hayo baada ya Gandhi kutoa amri ya kushambuliwa hekalu la dhahabu lililoko katika jimbo la Punjab, ambalo lilihesabiwa na masingasinga kuwa ni eneo takatifu. Masingasinga ambao wanaunda asilimia mbili ya watu wa India na wengi wao wanaishi katika jimbo la Punjab, walikusanya silaha zao kwenye hekalu hilo kwa shabaha ya kufanya uasi na kutaka kujitenga jimbo hilo.***
Katika siku kama ya leo miaka 23 iliyopita, aliaga dunia Federico Fellini mtengenezaji filamu maarufu wa Kiitalia. Fellini ni miongoni mwa watengenezaji na waongozaji filamu wakubwa wa karne ya ishirini. Fellini alianza kazi ya kuandika filamu tangu mwaka 1938 na baadaye akajiingiza katika fani ya utengenezaji filamu. Baada ya kumalizika Vita vya Pili vya Dunia mwaka 1945, Federico Fellini akiwa msaidizi wa mtengeneza filamu aliyejulikana kwa jina la Roberto Rossellini walitengeneza filamu iliyojulikana kwa jina la "Rome Open City". Aidha mwaka 1993, yaani miezi sita kabla ya kifo chake, Fellini alitunukizwa tuzo ya Oscar kutokana na kazi zake za thamani katika ulimwengu wa filamu.
Siku kama ya leo, miaka 102 iliyopita, serikali ya wakati huo ya Iran ilitangaza kutopendelea upande wowote katika Vita vya Kwanza vya Dunia. Hata hivyo udhaifu wa kisiasa wa watawala wa wakati huo, matatizo ya ndani, matatizo ya kivita na kupenda kujitanua kwa nchi zilizokuwa zikipigana katika vita hivyo, ni mambo yaliyopelekea nchi hii kwenda kinyume na ahadi yake ya kutofungamana na upande wowote katika vita hivyo. Ni kutokana na hali hiyo, ndipo Iran ikajikuta katika hujuma na mashambulizi ya majeshi ya Uingereza, Urusi ya zamani na jeshi la Othmania na kuisababishia hasara kubwa.
Miaka 36 iliyopita katika siku kama ya leo Mhandisi Muhammad Jawad Tundguyan Waziri wa Mafuta wa wakati huo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran pamoja na viongozi kadhaa wa wizara hiyo hiyo walitekwa nyara na wanajeshi vamizi wa Iraq mwezi mmoja baada ya Iraq kuivamia Iran. Utekaji nyara huo ulijiri wakati waziri huyo wa mafuta wa Iran alipokuwa katika safari ya kuzitembelea taasisi za mafuta za kusini mwa nchi. Utawala wa Saddam ulikadhibisha kwa muda kumteka nyara Mhandisi Tundguyan, lakini baadaye ulidai kuwa waziri huyo alijiuwa akiwa mateka. Hatimaye uchunguzi wa kidaktari na ushahidi uliotolewa na mateka wengine waliokuwa naye ulithibitisha kuwa Waziri wa Mafuta wa Iran alikufa shahidi kutokana na mateso makubwa aliyofanyiwa na maajenti wa utawala wa Baath wa Iraq.