Nov 01, 2016 06:47 UTC
  • Familia Salama (11)

Hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni kujiunga nasi katika mfululizo huu wa makala kuhusu Familia salama.

Makala hizi huangazia masuala mbali mbali ya afya ya familia kama vile lishe, mazoezi, madhara ya matumizi ya mihadarati, umuhimu wa mahaba katika familia n.k. Katika makala ya leo tutaangazia kuhusu changamoto ya uraibu wa mihadarati au dawa za kulevya. Karibuni kujiunga nasi hadi mwisho.

Utegemezi wa dawa za kulevya ni hali ya kuugua au isiyo ya kawaida ambayo hutokana na matumizi ya mihadarati mara kwa mara. Tatizo la dawa za kulevya linahusisha uendelezaji matumizi sugu ya dawa hadi kufikia tabia ya kutafuta dawa za kulevya.
Uraibu wa dawa za kulevya ni moja ya matatizo makubwa ya zama za leo na kila mwaka idadi kubwa ya watu hupoteza maisha kutokana na utumizi wa mihadarati.
Ongezeko la idadi hiyo ya waaathirika wa dawa za kulevya ni ya kasi kubwa duniani kiasi cha Ludwig Kurt mtaalamu maarufu wa toxikolojia duniani kusema: "Mbali na chakula, mada ambayo utumizi wake unaongozeka sana duniani katika utumizi miongoni mwa watu wengi ni dawa za kulevya."
Umoja wa Mataifa ulitangaza katika Siku ya Kimataifa ya Kupambana na Mihadarati Manmo tarehe 26 Juni mwaka 2015 kuwa: "Karibu asilimia Tano ya watu wazima au watu milioni 250 wenye umri wa kati ya miaka 15 na 64 wametumia japo aina moja ya mihadarati mwaka 2014 ambapo kati yao milioni 27 wako katika hali mbaya ya uraibu."

Madhara yamadawa ya kulevya

 

Hali kadhalika, Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Mihadarati na Uhalifu UNODC inasema watu wengine milioni 12 wanajidunga sindano za dawa za kulevya na asilimia 14 kati yao wanaishi na Virusi vya Ukimwi, VVU. Kwa msingi huo dawa za kulevya pia zimechangia pakubwa kuenea ugonjwa hatari wa Ukimwi.
Ban Ki moon Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa alitoa taarifa na kubainisha masikitiko yake kuwa kati ya kila watu watatu waraibu wa dawa za kulevya, mmoja ni mwanamke.
Wataalamu wanaamini kuwa, kati ya sababu za watu kutumbukia katika uraibu au utegemezi wa dawa za kulevya ni kutaka kuonja, kutaka starehe bandia, kusahau matatizo, kutaka kujihatarisha, kuhisi kuwa na umri wa juu, kujiunga na makundi ya wenye uraibu n.k
Uraibu wa dawa za kulevya ni tatizo kubwa katika jamii ambalo limetikisa misingi ya ustawi wa jamii mbali mbali duniani.
Hali kadhlika uraibu wa dawa za kulevya ni chanzo cha kuvurugika familia na kupunguza pato na uzalishaji utarjii katika jamii.
Uchunguzi uliofanyika umebaini kuwa familia ina nafasi kubwa katika kuibuka tatizo la dawa za kulevya. Hii ni kwa sababu familia ni sehemu ya kwanza ya kustawi shakhsia na ni hapo ndipo watoto na mabarobaro hupata vigezo vya kuiga katika maisha.
Kutofahamu na upuuzaji wa wazazi pamoja na uhusiano dhaifu baina yao na watoto, ukosefu wa nidhamu katika familia na kutengana wazazi ni kati ya nukta ambazo huchangia watoto kuanza kuwa waraibu wa dawa za kulevya.
Wataalamu wanasema moja ya sababu ambazo hupelekea mabarobaro na vijana kutumbukia katika uraibu wa dawa za kulevya ni kuwa baadhi huanza kuona utumizi wa mihadarati katika familia au watu walio karibu na familia. Kuwepo mihadarati ndani ya nyumba hupelekea mwenye hamu ya kujaribisha kutafuta fursa inayojitokeza kutumia mihadarati.
Wataalamu pia wanasema wakati wazazi au walezi wanakuwa wepesi wa kuwapa ruhusa watoto kufanya kila wanalotaka na kujumuika na kila aina ya marafiki pia huchangia kuanza uraibu au utegemezi wa mihadarati.

Mihadarati na unywaji pombe husababisha pia madhara mengine mengi kama kuenea maambukizi ya ukimwi

 

Hali kadhalika wati wazazi wanakuwa wanajishughulisha na kazi zao za kila siku huwa hawapati wakati wa kutosha wa kuwa na watoto wao na kuchunguza tabia na nyendo zao na kwa msingi huo baadhi hutumbukia katika makundi hatari ya wanaotumia mihadarati. Kwa hivyo wazazi pamoja na kushughulishwa na kazi zao wanapaswa kujitahidi kuhakikisha kuwa wanapata wakati wa kukaa na watoto ili wafahamu fikra zao na marafiki zao. Iwapo katika familia wazazi hawatatekeleza majukumu na kazi zao ipasavyo watoto watatumbikia katika uraibu hatari wa dawa za kulevya.
Pamoja na hayo baadhi ya wakati iwapo wazazi watawabana watoto sana jambo hilo pia hupelekea wengine kutumbukia katika uraibu wa dawa za kulevya wakipata mwanya mdogo. Kwa msingi huo kuna haja ya kuleta mlingano katika suala zima la kuwadhibiti watoto. Yaani wasiachiliwe wawe huru kufanya kila wanalotaka na pia wasibanwe kiasi cha kukosa sehemu ya kupumua.
Sababu nyingine ambayo inaweza kuchangia watoto kutumbukia katika uraibu wa mihadarati ni kukosa kuzingatia matakwa ya kimantiki ya watoto, kuwadhlilisha au kutowaheshimu watoto, au mzazi kuwa mkali kupita kiasi kwa watoto. Watoto ambao wazazi wao ni wenye kuwabana sana na ambao hawapewi uhuru au fursa ya kubainisha maoni yao hupoteza ile hali ya kujiamini. Katika hali kama hii kutokana na kuwa hawana uzoefu wa kuchukua maamuzi, huweza kushawishiwa haraka kuingia katika uraibu wa dawa za kulevya.
Kutozingatia majukumu ya kidini na kukosa imani ya kidini katika familia pia hupelekea kukosekana vizingiti na mipaka katika familia. Jambo hili huandaa mazingira ya mabarobaro na vijana kujiingiza kirahisi katika utumizi wa dawa za kulevya. Kwa hivyo wazazi wanapaswa kuwa na ujuzi na umahiri wa kulea ili kwa njia hiyo watoto waweze kujiamini. Wazazi wanapaswa kuwafunza watoto wao kuhusu thamani ya kusema la kwa marafiki au wenzao wa rika moja ambao wanajaribu kuwatumbukiza katika uraibu wa dawa za kulevya.
Hatua hii inaweza kuwa na faida na taathira chanya wakati tu wazazi wenyewe wanapokuwa kigezo cha kuigwa na watoto na wawe ni wakweli katika kauli zao. Iwapo wazazi watatenda kinyume cha kile wanachosema, basi wasitegemee watoto wao wawasikilize.


@@@

Tunamaliza kwa kutambua ukweli kuwa tayari jamii nyingi zimeathiriwa na uraibu wa dawa za kulevya kote duniani hasa katika nchi za Afrika Mashariki. Pamoja na hayo utegemezi wa dawa za kulevya ni ugonjwa sugu lakini unaotibika. Kwa watu wengi, matumizi ya dawa za kulevya hugeuka sugu, na kurejelea matumizi huwezekana hata baada ya muda mrefu wa kuacha. Kama ugonjwa sugu, unaorejearejea, uraibu wa mihadarati unahitaji matibabu endelevu ili kuongeza vipindi baina ya urejeleaji na upunguzaji athari zake. Kupitia matibabu yanayoambatana na mahitaji ya mtu binafsi, watu wanaotegemea dawa za kulevya wanaweza kupona na kuishi maisha bora.