Jumatano, Nov 9, 2016
Leo ni Jumatano tarehe 9 Safar 1438 Hijria sawa na Novemba 9, 2016.
Katika siku kama ya leo miaka 1401 iliyopita kulingana na kalenda ya Hijria, aliuawa shahidi Ammar bin Yassir, sahaba mkubwa wa Mtume Muhammad (saw) na msaidizi wa karibu wa Imam Ali bin Abi Twalib (as). Ammar bin Yasir aliuawa katika vita vya Siffin vilivyojiri kati ya majeshi ya Imam Ali (as) na Muawiya bin Abi Sufian. Ammar alizaliwa miaka 57 kabla ya Hijra ya Mtukufu Mtume na wazazi wake wawili, yaani Yassir na Sumayyah, ndio waliokuwa mashahidi wa kwanza katika Uislamu. Sahaba huyu mtukufu alisimama imara dhidi ya maudhi ya makafiri na alishiriki katika vita mbalimbali pamoja na Bwana Mtume (SAW). Wakati mmoja Mtume alimwambia Ammar: "Ewe Ammar! Baada yangu kutatokea fitina, na katika hali hiyo mfuate Ali bin Abi Twalib na kundi lake, kwani Ali yuko pamoja na haki na haki iko pamoja na Ali.
Siku kama ya leo miaka 1017 iliyopita, alifariki dunia Abu Ali Maskawayh, mtaalamu, mwanahistoria na mwanafikra mkubwa wa Kiislamu. Miskawayh alizaliwa mwaka 320 katika mji wa Rei ulio karibu na mji mkuu wa Iran ya sasa. Miskawayh alikuwa mwalimu katika elimu za zama zake sambamba na kufanya utafiti katika elimu ya tiba, kemia, historia na falsala. Miongoni mwa athari zilizobakia za Abu Ali Miskawayh ni pamoja na kitabu kiitwacho "Tahdhibul-Akhlaq", "Tajaaribul-Umam" na "Jaavidaane Kherad."
Siku kama ya leo miaka 139 iliyopita, alizaliwa nchini Pakistan Allama Muhammad Iqbal Lahore mwandishi, mwanafikra na malenga mzungumza lugha ya Kifarsi. Baada ya kumaliza masomo yake ya juu, Iqbal Lahore alielekea katika nchi za Ujerumani na Uingereza kwa ajili ya kuendelea na masomo ya juu zaidi katika taaluma ya falsafa. Alianza kusoma mashairi akiwa kijana huku shairi lake la kwanza likiwa ni lile lililokuwa na jina la ‘Naleh Yatiim’. Allama Iqbal Lahore alikuwa mwanaharakati pia aliyepambana kwa minajili ya kuikomboa Pakistan kutoka mikononi mwa India. Allamah Lahore alifariki dunia mwaka 1938.
Na Siku kama ya leo miaka 63 iliyopita Dakta Sayyid Hussein Fatimi Waziri wa Mambo ya Nje wa serikali ya Dakta Muhammad Musaddiq aliuawa kwa kunyongwa na vibaraka wa utawala wa Shah nchini Iran. Dakta Fatimi kabla ya hapo alikuwa amehukumiwa kunyongwa na mahakama moja ya kijeshi ya kimaonyesho ya utawala wa Shah huku akiwa mgonjwa sana. Baada ya mapinduzi ya Marekani ya tarehe 28 Mordad mwaka 1332 Hijria Shamsiya hapa nchini na baada ya kujiuzulu Dakta Musaddiq, dakta Sayyid Hussein Fatimi alikuwa akisakwa na vibaraka wa utawala wa Shah na alikuwa akiishi kwa kujificha. Lakini baadaye alikamatwa na kunyongwa katika siku kama ya leo.