Nov 09, 2016 10:16 UTC
  • Maswali Yetu na Majibu ya Thaqalain (143)

Assalaam Aleikum wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswqhili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inayokutangazieni kutoka hapa mjini Tehran. Kipindi kilicho hewani kama kawaida ya siku na wakati kama huu si kingine bali ni kipindi cha Maswali Yetu na Majibu ya Thaqalain.

Kwa mujibu wa hadithi ya Thaqalain na aya tulizojadili katika vipindi vilivyopita, tulipata kujua na kutambua kwamba uongofu na kuepuka upotovu hautimii ili kwa kushikamana kikamlifu na kwa pamoja na Qur’ani Tukufu na Ahlul Beit wa Mtume (saw). Je, hili lina maana kwamba hatuwezi kunufaika na Qur’ani Tukufu bila ya kuzirejea hadithi tukufu au kwa mmoja wa Maimamu maasumu wa Nyumba ya Mtukufu Mtume (saw)?

Hili ni swali la msingi na muhimu mno ambalo tutalijibu kwa kutegemea minara miwili ya uongofu inayotuepusha na kiza la upotovu, ambayo ni Qur’ani Tukufu na Hadithi za Ahlul Beit (as). Kwa hivyo kuweni pamoj nasi ili tupate kunufaika kwa pamoja na yale tuliyokuandalieni kwa juma hili, karibuni.

 

Ndugu wasikilizaji, ili kujibu swali hili tunaiangazia aya tukufu ya 29 ya Surat Swad ambapo Mwenyezi Mungu ambaye ni mkweli wa wasemaji wote katika kusifu kitabu chake anasema: Na hiki Kitabu, tumekuteremshia wewe, kimebarikiwa, ili wazizingatie Aya zake, na wawaidhike wenye akili.

Kwa kuzingatia aya hii ya Qur’ani Tukufu ni kitabu kilicho na manufaa mengi kwa wanadamu ambacho Mwenyezi Mungu alikiteremsha kwa Mtume wake (saw) ali kwanza watu wapata kutafakari kukihusu na kisha wenye akili wapate kunufaika zaidi na yaliyomo humo. Kwa maelezo hayo tunapata kufahamu kwamba kutafakari juu ya Qur’ani Tukufu ni amri ambayo imetolewa na kutakiwa kutekelezwa na wanadamu wote kwa sababu hilo ni jambo linalowezekana kwao lakini wale wanaonufaika zaidi na kitabu hicho kitakatifu ni wale wenye akili kutokana na kuzingatia na kutafakari kwao kwenye aya za kitabu hicho. Na hii ina maana kwamba aya za kitabu hiki cha mbinguni ambazo zinasema wazi kwamba Qur’ani Tukufu ni mwongozo kwa wale walio na takwa na kwamba kinawanufaisha walio na nyoyo zilizo hai zinaashiria manufaa ya kielimu kutokana na kitabu hicho na sio manufaa ya kinadharia tu yaani kufahamu tu maana ya aya zake bila kuzitekeleza kivitendo. Kwa msingi huo Mweyezi Mungu amewakemea watu wapotovu ambao hawatafakari Qur’ani ili kupata kujua maarifa na haki iliyomo humo kwa kusema katika aya ya 24 ya Surat Muhammad (saw): Je! Hawaizingatii hii Qur'ani? Au kwenye nyoyo (zao) zipo kufuli? Na pia anasema katika aya ya 82 ya Surat an-Nisaa: Je, hawaizingatii hii Qur'ani? Lau kama ingelitoka kwa asiyekuwa Mwenyezi Mungu bila ya shaka wangelikuta ndani yake khitilafu nyingi.

Ni wazi kutokana na aya hizi kwamba kutafakari na kuzingatia Qur’ani ni sababu na njia ya kujua miujiza ya Mwenyezi Mungu na kwamba inatoka kwa Mwenyezi Mungu moja kwa moja. Kwa msigi huo ni wazi kwamba jambo linalozuia kufuatwa kitabu hiki ni kiza, ujahili na kutu inayozikumba nyoyo na kuzifanya zisione ukweli wa mambo na wala sio akili salama inayofahamu hekima na mawaidha ya kitabu hiki kitakatifu.

Image Caption

 

Inafahamika wazi hapa kutokana na yale tuliyosema kwamba baadhi ya hakika za Qur’ani Tukufu zinaweza kufikiwa na kufahamika kwa kuzinagtia na kuitafakari kwenye aya zake moja kwa moja na kuzizinagtia kwa makini pamoja na kufungua wazi akili na nyoyo za watu wanaozisoma kama anavyobaisha hilo wazi Imam Swadiq (as) kwa kusema katika hadithi iliyopokelewa kwenye kitabu cha al-Kafi kwamba: ‘Hakika kwenye Qur’ani hii kuna mnara wa nuru ya wongofu na taa zinazoondoa giza. Hivyo na achague mchaguzi macho yake na ayafunguilie macho yake mwangaza kwa sababu kutafakari ni uhai kwa moyo unaoona, kama anavyotembea mtu aliye na nuru kwenye giza.’

Kuna hadithi nyingi mno zilizo na madhumuni haya ambazo zimepokelewa kutoka kwa Ahlul Beit (as). Hadithi hizi bila shaka zinatoa wito wa kuzingatiwa kwa kina Qur’ani Tukufu na aya zake kwa msingi wa fikra salama ambazo ziko mbali na ufasiri wa Qur’ani ambao unategemea mtazamo wa mtu binafsi, misimamo (itikadi) ya awali na matamanio ya mtu binafsi.

Ni wazi kuwa kwa kuzingatiwa nguzo na misingi hii kuna uwezekano wa kufahamika baaadhi ya hatua katika hatua na maarifa mengi na ya dhahiri ya Qur’ani Tukufu. Lakini hadithi nyingi zinabainisha na kusisitiza wazi kwamba kitabu hiki kitakatifu kina maarifa ya kina ambayo yanahitajia elimu ya kina zaidi ili kuweza kuyafikia. Kitabu cha al-Kafi kinamkunuu Mtume Mtukufu (saw) akisema katika sehemu moja ya hadithi ndefu kwamba: ‘Mnapokumbwa na fitina kama usiku uliojaa giza mnapasa kushikamana na Qur’ani  kwa sababu ni ponyo linaloponya, na mtu anayeiweka mbele yake basi humuongoza kuelekea Pepo na mtu anayeiweka nyuma yake humuongoza kwenye moto. Ni dalili inayoongoza kwenye njia iliyo bora zaidi na ni kitabu ambacho  ndani yake mna ufafauzi na ubainishaji…… Kina dhahiri na batini na dhahiri yake ni hukumu na batini yake ni elimu. Dhahiri yake ni ya kuvutia na batini yake ni ya kina. Kina nyota, na juu ya nyota hizo kuna nyota nyingine. Maajabu yake hayahesabiki wala mageni (mambo yasiyojulikana) yake kukatika. Ndani yake mna taa za mwongozo, minara ya taa za hekima na dalili za maarifa kwa watu wanaofahamu sifa….’

Kwenye hadithi hii muhimu na kamili ya Mtume Mtukufu (saw) kuna maelezo kuhusiana na jinsi ya kuifahamu Qur’ani Tukufu na kuepuka fitina ambapo tutaashiria baadhi yake kuhusiana na swali la kipidi hiki baada ya muda usio mrefu, hivyo basi endeleeni kuwa pamoja nasi.

 

Mtume Mtukufu (sw) anaashiria kweye hadithi hii kwamba dhahiri ya Qur’ani Tukufu ina hekima ambapo kwenye hekima na batini yake mna elimu kwa maana kwamba dhahihiri yake ina viwango vya maarifa ambayo yana maarifa mengine ya kina zaidi ambayo kuyafahamu kunahitajia nyota ambazo ziko juu ya Qur’ani yenyewe, yaani zina ujuzi wa kutosha na yaliyomo kweye kitabu hicho. Hii ina maana kwamba ni watu watoharifu na walio na elimu ya kina kuhusiana na mambo yaliyofichika na kuhifadhiwa kweye Qur’ani na hivyo kuwafanya kuwa nyota zinazoagaza na kutoa nuru inayoelekeza kwenye hakika za kitabu hicho tu ndio wanaofaa na walio na uwezo wa kujua kina cha maarifa ya kitabu hicho cha mbinguni.

Jambo la pili ni kuwa uwezo wa kufikia maarifa ya Qur’ani na hata yale ya dhahiri, umepewa watu ambao wanafahamu vyema sifa, yaani sifa za Qur’ani na njia za kufikia sifa hizo mbali na upotovu wa kimaanawi na sio wa kilafudhi katika kukielewa kitabu hiki kitukufu. Kwa msigi huo usomaji wa kitabu hicho utaandamana na uzingatiaji na usomaji wake kupewa haki inayostahiki kama anavyobainisha hilo Maulana al-Basit al-Muhammadi al-Akbari kama ilivyopokelewa katika kitabu cha Tuhuf al-Uqul kwamba amesema: ‘…..Fahamuni kwamba hamtawajua walio na takwa hadi mfahamu sifa ya uongofu… na hamtasoma Kitabu kama inavyotakiwa hadi mtakapomjua aliyeyasema maneneo yaliyomo. Mtakapoyajua hayo matapata kujua bidaa (uzushi) na ulaghai na kuona udanganyifu ukifanywa dhidi ya Mwenyezi Mugu, na wala wasikudanganyeni wasiojua. Na yajueni hayo kutoka kwa watu wanaofaa (walio na elimu) kwa sababu wao ni watu maalumu ambao wanaongozwa kwa nuru yao na ni Maimamu wanaofuatwa.’

 

Na natija tunayoipata kutokana na somo la leo wapenzi wasikilizaji ni kwamba kufahamu hatua za dhahihiri za Qur’ani Tukufu ni jambo rahisi na linalowezekana kwa yule mtu aliyefungulia akili yake jambo hilo na kujiweka mbali na matamanio na upotoshaji wa kimaanawi kwa misingi ya fikra iliyo salama. Hii ni katika hali ambayo kufikiwa kwa marifa na hakika ambazo zimehifadhiwa ambazo hazifahamiki ila na baathi wa watu wema waliotakaswa na kutohorishwa na hivyo kuepuka kila aina ya fitina ikiwemo ya ufahamu mbaya na usio sahihi wa aya takatifu, kunahitajia mwongozo wa nuru, wajuzi na walimu wa Qur’ani Tukufu na ambao ni wataalamu na warithi maasumu wa elimu ya Mtume Mtukufu (saw).

Na kufikia hapa wapenzi wasikilizaji ndio tunafikia mwisho wa kipindi chetu cha juma hili cha Maswali Yetu na Majibu ya Thaqalain ambacho kimekujieni kupitia Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inayokutangazieni kutoka hapa mjini Tehran. Ni matumaini yetu kuwa mtajiunga nasi tena juma lijalo ili mpate kunufaika na yale tutakayokuwa tumekutayarishieni katika kipindi hicho. Basi hadi kufikia wakati huo, tunakuageni nyote wapenzi wasikilizaji kwa kusema, Wassalaam Aleikum Warahmatullahi Wabarakatuh.