Nov 24, 2016 02:33 UTC
  • Alkhamisi, 24 Novemba, 2016

Leo ni Alkhamisi tarehe 24 Safar 1438 Hijria sawa na Novemba 24, 2016.

Siku kama ya leo miaka 384 iliyopita alizaliwa mwanafalsafa na mtaalamu wa masuala ya jamii wa Uholanzi, Baruch de Spinoza. Spinoza alivutiwa sana na falsafa ya Descartes sambamba na kipindi cha kutafuta elimu ya juu. Ukosoaji mkubwa wa mwanafalsafa huyo dhidi ya itikadi za dini ya Kiyahudi ulizusha uhasama mkubwa wa viongozi wa dini hiyo na kuanzisha kampeni za kumtenga katika jamii yao. Fikra za kifalsafa za Spinoza zinakaribiana sana na itikadi za kisufi.

Miongoni mwa vitabu vya mwanafalsafa huyo ni 'Sayansi ya Maadili', 'Siasa' na 'Marekebisho ya Akili'.

Baruch de Spinoza

Siku kama ya leo miaka 152 iliyopita alizaliwa mchoraji na msanii mkubwa wa Ufaransa, Henri Toulouse Lautrec. Familia ya Lautrec ilikuwa ya kipato cha wastani na licha ya kukabiliwa na matatizo mengi ya kimaisha, Lautrec alitokea kuwa miongoni mwa wasanii mashuhuri na hodari wa Ufaransa kutokana na kipawa chake kikubwa. Msanii huyo alifariki dunia mwaka 1901.

Henri Toulouse Lautrec

Tarehe 24 Novemba miaka 185 iliyopita, Michael Faraday mwanafizikia stadi wa Kiingereza alifanikiwa kugundua chombo cha mkondo wa umeme kinachojulikana kwa jina la ''Electric Current''. Ugunduzi huo ulimuwezesha Faraday kupiga hatua kubwa katika elimu ya fizikia. Faraday alizaliwa mwaka 1791 na awali alikuwa akifanya kazi katika duka la kuuza vitabu. Ni kipindi hicho ndipo taratibu alipoanza kusoma vitabu mbalimbali na kugundua vifaa vingi vya umeme.

Michael Faraday

Siku kama ya leo miaka 50 iliyopita Ustadh Jabbar Baghcheban alifariki dunia baada ya miaka mingi ya kutoa huduma kubwa kwa viziwi hapa nchini. Ustadh Baghcheban alizaliwa mwaka 1261 Hijria Shamsia na mwaka 1303 aliasisi shule ya kwanza ya watoto katika mji wa Tabriz magharibi mwa Iran. Shule hiyo ilianza kutoa mafunzo kwa watoto watatu viziwi. Ustadh Jabbar Baghcheban alivumbua mbinu mpya na ya kisasa ya kutoa mafunzo ya kusoma na kuandika kwa watoto viziwi ambayo ingali inatumika hadi hii leo hapa nchini.

Ustadh Jabbar Baghcheban

Tarehe 24 Novemba miaka 3 iliyopita Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na nchi tano wanachama wa kudumu Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa pamoja na Ujerumani zilitia saini makubaliano ya muda kuhusu miradi ya kuzalisha nishati ya nyuklia ya Iran katika mji wa Geneva. Kutiwa saini makubakliano hayo kulifungua njia ya mazungumzo kati ya Iran na nchi hizo sita kwa ajili ya kufikia mapatano kamili na kuondoa suutafahamu iliyokuwepo juu ya miradi ya kuzalisha nishati ya nyuklia ya Iran na hatimaye kufutwa vikwazo vya kidhalimu vya nchi za Magharibi. Sifa muhimu zaidi ya makubaliano ya muda ya Geneva ni hatua ya nchi za Magharibi ya kukiri na kukubali haki ya Iran ya kuwa na nishati ya nyuklia kwa malengo ya amani na kurutubisha madini ya urani. Makubaliano kamili ya na mwisho kati ya Iran na kundi la 5+1 yalitiwa saini Julai 2015.    

Na siku kama ya leo miaka 1054 iliyopita Sahib bin Ubbad, mwanafasihi maarufu na msomi wa Kiislamu wa kizazi cha Dailami alifariki dunia. Sahib alikuwa mwandishi hodari na mtu mwenye hadhi na mashuhuri sana katika zama zake. Licha ya kwamba alikuwa waziri katika serikali ya kizazi cha Dailami, lakini alikuwa mtu mnyenyekevu na mwema kwa watu wa chini yake. Sahib bin Ubbad ameandika vitabu vingi, na maarufu zaidi ni kile cha "al Muhiit" chenye juzuu saba.

Mahala lilipo kaburi la Sahib bin Ubbad, Isfahan-Iran 

Miaka 66 iliyopita na katika siku kama ya leo yaani tarehe 4 Azar mwaka 1329 Hijiria Shamsia, Tume ya Mafuta ya Bunge la Taifa la Iran, ilipinga mkataba ziada wa mafuta kati ya Iran na Uingereza. Mkataba huo ulikuwa na lengo la kuimarisha nafasi ya Uingereza na kuzidisha uwezo wa nchi hiyo kuchimba mafuta huko kusini mwa Iran. Vilevile mkataba huo uliotayarishwa katika kilele cha ushindani wa Marekani na Uingereza wa kupora utajiri wa mafuta wa Iran, ulitambuliwa kuwa ni tishio kwa maslahi ya taifa.

Kutaifishwa kwa sekta ya mafuta ya Iran