Dec 04, 2016 08:22 UTC
  • Jumamosi, 03 Disemba, 2016

Leo ni Jumamosi tarehe 3 Mfunguo Sita Rabiul Awwal 1438 Hijria sawa na tarehe 3 Disemba mwaka 2016.

Miaka 132 iliyopita katika siku kama ya leo, alizaliwa Dakta Rajendra Prasad, mwanasiasa na mwanafalsafa wa India huko katika mojawapo ya vijiji vya jimbo la Bihar. Rajenda Prasad aliweza kuendelea na masomo na kufikia daraja ya udaktari, licha ya hali duni ya kifedha ya familia yake. Aidha alishiriki na wananchi wa India katika mapambano ya kupigania uhuru wa nchi yao. Prasad vilevile alishirikiana bega kwa bega na Mahatma Gandhi katika mapambano ya kisiasa dhidi ya wakoloni wa Kiingereza na kwa mara kadhaa aliteuliwa kuongoza chama cha Congress ya Kitaifa ya India. Rajendra Prasad aliteuliwa kuwa Rais wa kwanza wa India baada ya uhuru wa nchi hiyo na kuasisiwa mfumo wa jamhuri nchini humo mwaka 1950. ***

Siku kama ya leo miaka 97 iliyopita, Auguste Renoir mchoraji mkubwa wa Kifaransa aliaga dunia akiwa na umri wa miaka 78. Renoir alizaliwa tarehe 7 Machi 1841 na kwa haraka mno aliweza kuonyesha dhuku na mapenzi yake kwa taaluma ya uchoraji. Akiwa na umri wa miaka 19 tayari Auguste Renoir alikuwa ameshaondokea kuwa mchoraji mahiri na mashuhuri mjini Paris. ***

Katika siku kama ya leo miaka 32 iliyopita, kulitokea janga kubwa la kuvuja gesi ya kemikali katika kiwanda kimoja cha Marekani katika mji wa Bhopal huko katikati mwa India. Kiwanda hicho kilikuwa kikimilikiwa na kampuni ya Kimarekani iliyokuwa ikijulikana kwa jina la Union Carbide. Uzembe wa maafisa wa kiwanda hicho na kutozingatiwa viwango vya usalama ulipelekea kuvuja kwa gesi ya sumu ya sianidi (cyanide) kutoka katika kiwanda hicho na kuenea katika hewa. Maelfu ya wakazi mji wa Bhopal walipoteza maisha na mamia ya wengine kujeruhiwa katika janga hilo ambalo lilitambuliwa kuwa janga kubwa zaidi la viwandani duniani. ***

Miaka 26 iliyopita katika siku kama ya leo, mkutano wa kwanza wa Kiislamu wa Palestina ulifanyika mjini Tehran. Mkutano huo ulianza mjini Tehran ukiwa na ajenda ya mfungano wa ulimwengu na harakati ya Intifadha ya Palestina na kuendelea Mayahudi kuhamia Palestina. Wanamapambano na wanafikra wa Kiislamu wa Palestina, Iran na nchi nyingine walishiriki katika mkutano huo. ***

Na miaka 5 iliyopita, maafisa wa kijeshi wa Iran walitangaza kwamba wamefanikiwa kuidhibiti ndege ya kijasusi isiyokuwa na rubani (drone) ya Marekani aina ya RQ-170. Ndege hiyo iliyoingia katika anga ya mashariki mwa Iran kutokea Afghanistan, ilitumbukia katika mtego wa kikosi cha vita vya electroniki cha Iran na kushushwa chini ikiwa nzima. Ndege hiyo ya RQ-170 ni miongoni mwa drone za kisasa kabisa za jeshi la Marekani na inatumiwa na shirika la ujasusi la nchi hiyo CIA kutokana na uwezo wake mkubwa wa kufanya ujasusi.