Ulimwengu wa Spoti, Jan 9
Mkusanyiko wa matukio muhimu ya michezo ndani ya siku saba zilizopita......
Magongo: Iran yang'ara Kombe la Croatia
Timu ya taifa ya mpira wa magongo ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imetemalaki mashindano ya mchezo huo ya kuwania Kombe la Croatia mwaka huu 2017. Siku ya Jumamosi wachezaji wa Iran waliitandika klabu ya matawi ya juu ya wenyeji Croatia mikwaju 15-3 katika mchezo uliopigwa katika uwanja wa mji wa Sveti Ivan Zelina, ulioko kaskazini mashariki mwa mji mkuu, Zagreb. Kabla ya hapo timu ya taifa ya Iran iliichachawiza Croatia mikwaju 5-2 Ijumaa, siku moja baada ya kuitandika Belarus mikwaju 8-2. Vijana hao wa Iran walianza vyema mashindano hayo baada ya kuwagaragaza vijana wa Slovenia mikwaju 20-0 katika mchuano wa ufunguzi Ijumaa.Mashindano hayo ya mpira wa magongo ya Croatia Indoor Cup 2017 yalianza Januari 6 na kufunga pazia lake siku mbili baadaye. Timu ya taifa ya Iran ya mpira wa magongo imeyatumia mashindano hayo kupasha misuli, kwa ajili ya kushiriki duru ya 7 ya Kombe la Asia katika mchezo huo itakayofanyika Qatar mwezi Mei mwaka huu.
Mwanamieleka wa Iran atawazwa Bingwa wa Mieleka Duniani
Bingwa wa mieleka mtindo wa freestyle wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Yazdani Charati ametawazwa kuwa mwanamieleka bora duniani katika kategoria ya kilo 74 mwaka uliomalizika wa 2016. Shirikisho la Mieleka Duniani limemtangaza bingwa huyo wa Iran mwenye umri wa miaka 22 nafasi ya kwanza kimataifa, kutokana na namna alivyong'ara katika Michezo ya Olimpiki ya Rio nchini Brazil Agosti mwaka jana.
Raia wa Russia Aniuar Geduev ameibuka wa pili katika orodha hiyo ya Shirikisho la Mieleka Duniani. Wanamieleka wa mtindo wa freestyle Yabrail Hasanov wa Azerbaijan, Soner Demirtas wa Uturuki, raia wa Uzbekistan Bekzod Abdurakhmanov pamoja na Galimzhan Usserbaev wa Kazakhstan wameibuka katika nafasi tatu hadi 6 kwa usanjari huo. Itakumbukwa kuwa, Agosti 19 mwaka 2016, Yazdani Charati alimcharaza Aniuar Geduev wa Russia katika mieleka mtindo wa freestyle kategoria ya kilo 74, katika ukumbi wa Carioca Arena 2 mjini Rio de Janairo nchini Brazil na kutwaa medali ya dhahabu baada ya kujizolea jumla ya pointi 6-2. Hii ilikua dhahabu ya kwanza kutwaliwa na Iran katika mashindano ya olimpiki katika mielekea mtindo wa freestyle, tangu Olimpiki ya Sydney mwaka 2000. Wakati huo huo, Ghasem Rezaei wa Iran ameibuka wa tatu katika mtindo wa Greco-Roman kategoria ya kilo 98. Mwanamieleka huyo wa Iran ametunukiwa medali ya shaba baada ya kulemewa na Yasmany Lugo Cabrera wa Cuba katika Michezo ya Rio 2016. Raia wa Armenia Artur Aleksanyan ameibuka kidedea katika kategoria hiyo.
…………………………….......…XXXXXXXXXXX.............................................
Mshindi wa Tuzo ya Mchezaji Bora Afrika 2016
Kiungo nyota wa timu ya taifa ya Algeria ambaye pia anakipiga katika klabu ya Leicester City ya Uingereza, Riyadh Mahrez ametangazwa mshindi wa tuzo ya mchezaji bora Afrika mwaka 2016. Tuzo hizi huandaliwa na Shirikisho la Soka barani Africa CAF. Mahrez alishinda tuzo hiyo kwa kujizolea kura 361, huku Mgabon Pierre-Emerick Aubameyang anayechezea klabu ya Borussia Dortmund akishika nafasi ya pili kwa kupata kura 313 wakati ambapo Sadio Mane anayekipiga Liverpool raia wa Senegal akimaliza nafasi ya tatu kwa kupata kura 186.
Tuzo ya mchezaji bora wa Afrika kwa wachezaji wa ndani ambayo alishinda Mtanzania Mbwana Samatta mwaka 2015, mara hii imerudi tena Afrika Mashariki, baada ya kwa golikipa wa Mamelodi Sundowns na timu ya taifa ya Uganda, Denis Onyango kushinda tuzo hiyo.
Soka: Simba na Yanga kuvaana nusu fainali Kombe la Mapinduzi
Klabu za Yanga na Simba za Tanzania zinatazamiwa kushuku dimbani Jumanne hii kutoana jasho katika mchuano wa nusu fainali ya Kombe la Mapinduzi. Yanga imejikatia tiketi ya nusu fainali licha ya kuchabangwa na Azam katika mchuano wake wa mwisho. Katika kipute hicho cha Januari 7, vijana wa Young Africans almaarufu Yanga walikubali kulishwa kichapo cha mbwa na Azam FC cha magoli 4-0 na kumaliza Kundi B wakiwa katika nafasi ya pili; wakati ambapo Simba walikuwa wanaguruma kwa na kuwameza mzima mzima vijana wa Jang’ombe Boys kwa kuwacharaza mabao 2-0 na kuifanya imalize Kundi A ikiwa katika nafasi ya kwanza. Ushindi wa magoli 2-0 dhidi ya Jang’ombe Boys yaliyofungwa na Laudit Mavugo dakika ya 12 na 54, umeifanya Simba kumaliza nafasi ya kwanza katika msimamo wa Kundi A wakiwa na point 10. Ieleweke kuwa, kwa mujibu wa kanuni za mashindano hayo, mshindi wa kwanza wa Kundi A (Simba) atacheza na mshindi wa pili wa Kundi B (Yanga). Kindumbwendumbwe hicho cha nusu fainali kinatazamiwa kupigwa Jumanne hii ya January 10 saa mbili na robo usiku katika uwanja wa Amman visiwani Zanzibar. Azam FC waliyokuwa vinara wa Kundi B kwa jumla ya point saba wanausubiri mchezo wa mwisho wa Kundi A kati ya URA ya Uganda ambao ni Mabingwa watetezi dhidi ya Taifa Jang’ombe ili kuweza kufahamu atacheza na nani katika hatua ya nusu fainali ya Mapinduzi Cup mwaka huu 2017.
Riadha: Wakenya waliobadili uraia wawika Uingereza
Raia wa Kenya ambao walibadilisha uraia Leonard Korir na Yasemin Can ndiyo mabingwa wapya wa mbio za nyika za Great Edinburgh XCountry zilizofanyika nchini Uingereza, siku ya Jumamosi. Kwa mujibu wa wavuti wa swahilihub wa Shirika la Habari la Nation la Kenya, Korir alinyakua taji la mbio za kilomita nane kwa upande wa wanaume ikiwa ni pamoja na kumbwaga nyota wa riadha Mo Farah na bingwa wa mwaka 2016 Garett Heath. Korir, mwenye umri wa miaka 30, ambaye alichukua uraia wa Marekani mnamo Mei mwaka 2016, alishinda taji hilo kwa kutumia dakika 24:03, akimlemea aliyekuwa nyuma yake Callum Hawkins kwa sekunde moja tu. Hawkins aliongoza mbio hizi ikisalia mzunguko wa mwisho akifuata unyo unyo na Korir na mzawa mwingine wa Kenya, Aras Kaya, lakini Korir akampiku Hawkins utepeni. Can, ambaye alibadili uraia kutoka Kenya hadi Uturuki mnamo Machi 13 mwaka 2016, alizidi kutesa. Mkimbiaji huyu mwenye umri wa miaka 20, ambaye alifahamika kama Vivian Jemutai, alishinda mbio za mita 5,000 na 10,000 katika Riadha za Ulaya na Mbio za Nyika za Ulaya mwaka 2016. Akda, ambaye alifahamika kama Mirriam Jepchirchir Maiyo akiwa Mkenya kabla ya kubadili uraia Machi 13 mwaka 2016 na kuwa Mturuki, alimaliza katika nafasi ya tatu jijini Edinburgh.
…………………………….......…..XXXXXXXXXXXX…….....…………………….
Ligi ya Premier
Kiungo Dele Alli, aliifungia Tottenham mabao mawili wakati timu hiyo ilipokutana na vinara wa Ligi Kuu ya Soka ya Uingereza, Chelsea, na kuvunja msururu wa timu kutoshindwa. Chelsea ilikuwa ikijaribu kuwa klabu ya kwanza kupata ushindi katika michezo 14 mfululizo na kusalia kileleni mwa ligi, lakini mabao ya Dele Alli yaliyopachikwa wavuni baada ya kuandaliwa pasi nzuri na mchezaji Christian Eriksen yalitosha kuzamisha jahazi la kocha Antonio Conte.Eden Hazard alikuwa na nafasi mbili za kuiokoa Chelsea lakini Spurs waliweza kufanikiwa kupata alama tatu muhimu na kuwaondoa majirani zao Arsenal katika nafasi ya nne. Licha ya kichapo hicho,
The Blues wanasalia kileleni mwa msimamo wa ligi ya Premier wakiwa na alama 49. Liverpool ambayo ililazimishwa sare ya mabao 2-2 na Sunderland, ipo katika nafasi ya pili ikiwa na alama 44 huku wabeba bunduki wa Arsenali ambao pia walilazimishwa sare ya mabao Bournemouth wakibaduliwa kutoka nafasi ya tatu ya hivi karibuni hadi nafasi ya tano, wakiwa na alama 41. Manchester City ambayo iliibamiza Burnley mabao 2-1, hawana budi kuridhika na nafasi ya tano kwenye jedwali la Ligi ya Premier kwa sasa, wakiwa na pointi 42, sawa na vijana wa Spurs walioko katika nafasi ya tatu, ingawaje wanatofautiana kwa mabao.
…………………………...............…….TAMATI…...................………………………