Sayansi na Teknolojia Mpya (3)
Karibuni katika mjumuiko huu wa vipindi ambavyo huangazia maendeleo mapya katika sekta za sayansi, teknolojia na tiba duniani na hasa nchini Iran. Leo tutaangazia mafanikio ya wanasayansi wa Iran katika kutengeneza chombo cha kusafisha maji machafu kati ya mambo mengine.
Iran imekuwa nchi ya tatu duniani kumiliki teknolojia ya hali ya juu ya nano yenye uwezo wa kuyasafisha maji yenye kiwango cha juu cha madini ya nitrate. Mwanzoni mwa mwezi Novemba 2016, Iran ilizindua mashine ya kusafisha maji inayojulikana kama electrodialysis. Kabla ya Iran kufanikiwa kumiliki teknoljia ya utengenezjai mashine hiyo, ni Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel tu ndizo zilizokuwa zikimiliki teknolojia hiyo duniani.
Kuwepo maji safi na salama ya kunywa ni kati ya masuala muhimu na ya kimsingi katika maisha ya mwanadamu. Moja ya matatizo makubwa katika nchi za ulimwengu wa tatu na hasa barani Afrika na Mashariki ya Kati ni upatikanaji wa maji safi ya kunywa. Karibu asilimia 71 ya eneo lote la sayari ya dunia limefunikwa kwa maji lakini asilimi 97 ya maji hayo ni ya chumvi na hayafai kwa ajili ya kunywa. Ni asilimia moja tu ya maji ya kunywa duniani ndiyo yanyopatikana kwa urahisi.
Kwa hivyo kuhakikisha kuwa kunapatikana maji safi na salama ya kunywa kote duniani ni jambo muhimu sana na kwa msingi huo kunafanyika jitihada za kuhakikisha maji hayo yanapatikana kwa njia za utumizi wa teknolojia mpya.
Moja ya teknolojia hizo mpya ni ile ya kusafisha maji kwa mbinu ya Electrodialysis ambayo kwa kifupi inajulikana kama EDR. Kimsingi ni kuwa EDR ni mchakato wa kutumia umeme kuyeyusha madini kama vile chumvi, floridi, nitrati na sulphate katika maji
Mapema mwezi Novemba mwaka 2016, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilifanikiwa kuunda chombo hicho cha Electrodialysis na hivyo kuhakikisha kuwa teknolojia hiyo haihodhiwi tena na Marekani na Utawala wa Kizayuni wa Israel.
Kabla ya Iran kumiliki teknolojia hii, visima vya maji ambavyo vilikuwa na kiwango cha juu cha madini ya nitrate vilifungwa au maji katika visima hivyo kuchanganywa na yale yenye kiwango kidogo cha nitrate. Lakini hivi sasa Iran inatumia teknolojia hiyo ya Eelectrodialysis kusafisha maji na kuondoa mada haribifu pasina kudhuru mada zenye manufaa katika maji. Majaribio yaliyofanywa katika maabara kuhusu teknolojia hii yanaonyesha maji yaliyosafishwa kwa kutumia chombo hicho cha Electrodialysis ni ya kiwango cha juu sana. Kwa kutumia chombo hicho, Iran sasa inaweza kudhamini maji salama safi kwa gharama za chini.
Tunaendelea na kipindi chetu kwa habari ya mafanikio ya watafiti Wairani katika Chuo Kikuu cha Teknolojia cha Amir Kabir mjini Tehran ambao kwa mara ya kwanza wamefanikiwa kuunda mashine ya inkubeta ambayo inatumiwa chini ya mikroskopu ili kuweza kukuza seluli au mikrobu za utafiti au zinazofanyiwa uchunguzi. Kwa kutumia inkubeta hii maalumu, watafiti wanaweza kufanya majaribio ya elektromagnetiki katika seli. Ili kuzihifadhi seli katika mazingira yaliyo nje ya mazingira ya kumaumbile, kunahitajika mazingira maalumu kwani seli ambazo ziko katika mazingira yasiyo ya kimaumbile huwa na umri mfupi.
Kwa hivyo kwa kutumia mashine ya inkubeta hiyo wataalamu wanaweza kuchukua sampuli za seli za mwili wa mwanadamu na kuziweka katika miale na kuchunguza athari za miale hiyo katika seli.
Nukta maalumu ya inkubeta hii ni kuwa, kwa kuilinganisha na inkubeta kama hizo ambazo Iran imekuwa ikiziagiza kutoka nje ya nchi, inkubeta hii iliyotengenezwa na wataalamu Wairani imetumia gharama ndogo.
Kwingineko, Chuo Kikuu cha Teknolojia cha Amir Kabir mjini Tehran kimefanikiwa kuunda mfumo bora zaidi wa kulinda maelezo na faili binafsi za watumizi wa kompyuta. Mfumo huo unatumia ile mbinu ya kuhifadhi mafaili hewani ama kwenye 'mawingu' kwa Kiingereza 'Cloud'.
Katika kuhifadhi mafaili hewani ama kwenye 'mawingu' huwa kunakuwepo na uwezekano wa mafaili kuharibiwa kupitia baadhi ya aplikesheni au baadhi ya watumizi walio na idhini ya kuingia katika mfumo huo. Watafiti wa Chuo Kikuu cha Teknolojia cha Amir Kabir kwa kutumia mbinu ya K-Annonymity wameweza kutumia mbinu yenye kasi na usalama wa mtumizi wa mfumo wa kuhifadhi mafaili katika 'mawingu'.
Hali kadhalika, watafiti wa Chuo Kikuu cha Teknolojia cha Amir Kabir wamefanikiwa kuunda ngozi ambayo inaweza kutumiwa kufunika kidonda na baada ya siku saba kidonda kitakuwa kimepona. Mbinu hii ni bora zaidi kuliko ile inayotumika hivi sasa inayojulikana kama skin tissue repair. Aidha mwezi Novemba mwaka jana wataalamu wa Chuo Kikuu cha Teknolojia cha Shariff mjini Tehran nao pia walitangaza kufanikiwa kuunda ngozi ya kutibu vidonda sugu kama vile vya watu wenye kisukari na vya watu waliochomeka pasina kuwepo na madhara.