Jan 21, 2017 04:39 UTC
  • Jumamosi, 21 Januari, 2017

Leo ni Jumamosi tarehe 22 Mfunguo Saba Rabiu Thani 1438 Hijria sawa na tarehe 21 Januari 2017 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 1142 iliyopita, Musa al-Mubarraqa mtoto wa Imam Muhammad Taqi al-Jawad na ndugu wa Imam Hadi as aliaga dunia katika mji mtakatifu wa Qum Iran. Alizaliwa mjini Madina mwaka 214 Hijria na mpaka anafikisha umri wa miaka 6 ambapo baba yake aliuawa shahidi, alikuwa chini ya malezi na usimamizi wa baba yake huyo. Baadaye alijifunza elimu kutoka kwa kaka yake yaani Imam Jawad as. Musa al-Mubarraqa kipindi fulani aliishi mjini Kufa katika Iraq ya leo na alipokuwa na umri wa miaka 42 alisafiri na kuelekea katika mji wa Qum Iran. Aliishi mjini Qum akijishughulisha na uenezaji Uislamu hadi alipofariki dunia katika siku kama ya leo. Musa al-Mubarraqa ana daraja ya juu ya kielimu na alikuwa mpokezi wa hadithi. Aidha alisifika mno kwa taqwa na uchaji Mungu***

Miaka 280 iliyopita yaani tarehe 21 Januari 1723, tufani kubwa ililikumba eneo la Ghuba ya Bengali mashariki mwa India na kuua watu laki tatu. Tufani hiyo ilitambuliwa kuwa kimbunga kilichosababisha maafa makubwa zaidi katika eneo hilo. Ghuba ya Bengali iko kaskazini mashariki mwa Bahari ya Hindi na ni miongoni mwa maeneo ambayo hukumbwa na mafuriko na vimbunga vya mara kwa mara vinavyosababisha maafa makubwa ya nafsi na mali za watu. ***

Katika siku kama ya leo miaka 224 iliyopita, Mfalme Louis XVI wa Ufaransa anayejulikana pia kama Louis Capet. alinyongwa. Alichukua hatamu za uongozi nchini Ufaransa mwaka 1774 na kuathiriwa mno na mkewe yaani Malkia Marie-Antoinette. Mwaka 1789 wananchi wa Ufaransa walianzisha mapambano dhidi ya Mfalme Louis XVI kutokana na hali mbaya ya kiuchumi na kijamii na miaka mitatu baadaye serikali ya kifalme ilifutwa rasmi nchini Ufaransa. Hata hivyo kutokana na kuwa Mfalme Louis alikuwa ameomba msaada wa nchi za kigeni kwa siri alituhumiwa kuwa amefanya uhaini na kuhukumiwa kifo. Watu kadhaa wa familia ya Mfalme Louis XVI akiwemo mkewe Marie-Antoinette nao pia walitiwa kitanzi.***

Mfalme Louis XVI wa Ufaransa

Siku kama ya leo miaka 176 iliyopita, Sheikh Muhammad Taqi Razi, mashuhuri kwa jina la Agha Najafi, msomi mkubwa wa Kiislamu alizaliwa katika mji wa Isfahan Iran. Alisoma masomo ya utangulizi kwa baba yake na kisha baadaye akaelekea Najaf Iraq kwa lengo la kujiendeleza zaidi kielimu. Akiwa katika mji mtakatifu wa Najaf Muhammad Taqi Razi alihudhuria darsa na masomo ya wanazuoni wakubwa katika zama hizo kama Muhammad Hassan Shirazi na Sheikh Muhammad Kashif al-Ghitaa. Baada ya kurejea mjini Isfahan, Agha Najafi alifanikiwa kufikia daraja ya Ijtihad na kuwa na ushawishi mkubwa miongoni mwa wananchi. Mwanazuoni huyo hakuwa nyuma pia katika utunzi na uandishi wa vitabu ambapo al-Ijtihad wat-Taqlid, Asrar al-Ayaat na An-war al-Arifin ni baadhi tu ya vitabu mashuhuri vya alimu huyo.***

Sheikh Muhammad Taqi Razi (Agha Najafi)

Katika siku kama ya leo miaka 93 iliyopita, Vladimir Ilyich Lenin, kiongozi wa mapinduzi ya kikomonisti ya Umoja wa Kisovietu alifariki dunia. Lenin alizaliwa mwaka 1870. Alianza harakati za mapambano dhidi ya utawala wa kifalme wa Russia tangu akiwa Chuo Kikuu. Kutokana na harakati zake hizo, mara kadhaa Lenin alifungwa jela na kubaidishwa. Katika kipindi cha kuwa kwake jela, Lenin aliandika vitabu kadhaa.***

Vladimir Ilyich Lenin

Na miaka 38 iliyopita katika siku kama hii ya leo, kufuatia kuendelea upinzani wa wananchi Waislamu wa Iran dhidi ya utawala wa mfalme Shah, kulitokea mapigano baina ya raia na wanajeshi na kupelekea wananchi wengi kuuawa na kujeruhiwa. Wakati huo huo, wananchi Waislamu wa Iran walikuwa wakisubiri kwa hamu na shauku kubwa kurejea nchini Imam Khomeini kutoka uhamishoni na walikuwa wamefanya maandalizi ya kutosha kwa ajili ya mapokezi makubwa ya kihistoria ya kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu. Kamati maalumu iliyokuwa ikijumuisha viongozi wa kidini na wawakilishi wa matabaka mbalimbali ya wananchi iliundwa mjini Tehran, ili kutekeleza shughuli ya mapokezi ya Imam Khomeini  kwa hamasa kubwa kadiri inavyowezekana. Wakati huo huo, wananchi kutoka mikoa mbalimbali hpa Iran walikuwa wakimimika mjini Tehran kwa ajili ya kushiriki katika mapokezi ya Imam Khomeini. Aidha baada ya maandamano makubwa ya wananchi, askari 4,000 wa jeshi la anga wakiwaunga mkono wananchi wanamapambano wa Irn walifanya mgomo wa chakula wakitaka kutimuliwa nchini Iran washauri wa Kimarekani.***