Jumapili Januari 22, 2017
Leo ni Jumapili tarehe 23 Rabiul th-Thani 1438 Hijria sawa na tarehe 22 Januari, 2017 Miladia.
Siku kama ya leo miaka 839 iliyopita, alizaliwa Shihabud-Din Abdul-Rahman Dimashqi Muqaddasi, maarufu kwa jina la Abu Shamah, mmoja wa walimu wenye itibari katika vyuo vya mjini Damascus, Syria ya leo. Baada ya kuhitimu masomo yake ya msingi Shihabud-Din Abdul-Rahman Dimashqi, alielekea mjini Alexandria nchini Misri na akiwa hapo akajifunza elimu za hadithi, fiqhi na elimu nyingine za zama hizo. Baada ya hapo msomi huyo alisimamia chuo cha hadithi cha Darul-Hadith Ashrafiyyah. Kadhalika Abu Shamah aliandika vitambu mbalimbali vya historia na baadhi vikiwa vinahusiana na lugha ya Kiarabu.
Siku kama ya leo miaka 456 iliyopita alizaliwa mwanafalsafa na mtaalamu wa hesabati wa Uingereza Francis Bacon. Awali Bacon alijishughulisha na masuala ya kisiasa na baadaye akafungwa jela kwa tuhuma ya kula rushwa. Kipindi cha kufungwa jela kilikuwa fursa mwafaka kwa Francis Bacon kudhihirisha kipawa chake. Mwanafalsafa huyo alitoa mchango mkubwa katika kueneza Sayansi jarabati nchini Uingereza na kuhuisha sayansi na falsafa barani Ulaya. Bacon ameandika vitabu kadhaa kikiwemo kile cha New Atlantis.
Siku kama ya leo miaka 242 iliyopita, alizaliwa Andre Marie Ampere, mtaalamu wa hisabati na fizikia wa Ufaransa. Akiwa kijana mdogo alipendelea sana fani ya hesabati. Akiwa Chuo Kikuu cha Polytechnique cha mjini Paris, aligundua mambo kadhaa katika uga wa fizikia. Moja ya mambo aliyoyagundua Andre Marie Ampere ni pamoja na simu ya upepo "Telegrafu." Mtaalamu huyo alifariki dunia mwaka 1836.
Siku kama ya leo miaka 229 iliyopita, alizaliwa George Gordon Byron, malenga mashuhuri wa nchini Uingereza. Maisha ya Byron yalijawa na milima na mabonde kutokana na kujikita sana katika ukosoaji. Alianza shughuli ya kusoma mshairi akiwa kijana mdogo na kutokea kuwa maarufu katika uga huo. Shairi lake la kwanza lilikuwa lile lililoitwa 'Saa ya Wazi.' Alifariki dunia mwaka 1824 kwa kuuawa wakati wa vita baina ya utawala wa Othmania na Ugiriki, ambapo alikuwa upande wa jeshi la Ugiriki.
Siku kama ya leo miaka 193 iliyopita, alifariki dunia, Allamah Ahmad Naraqi, mtaalamu wa sheria za Kiislamu (fiqhi), hadithi na malenga mkubwa wa Iran. Alizaliwa mwaka 1185 Hijiria na akiwa kijana mdogo alisoma elimu ya dini kwa wasomi wakubwa wa mji wa Kashan, moja ya miji ya katikati mwa Iran na kufikia daraja ya ijtihadi. Aidha alisafiri mjini Najaf, Iraq kwa ajili ya kuujiendeleza kielimu. Baada ya kufariki dunia baba yake mzazi, Allamah Ahmad Naraqi alirejea mjini Kashan na kujishughulisha na kazi ya ukufunzi na malezi ya vijana wa mji huo. Moja ya athari muhimu za msomi huyo ni pamoja na kitabu cha 'Mi'rajus-S'adah' na Asraarul-Hajj'
Siku kama ya leo miaka 116 iliyopita, alifariki dunia Alexandrina Victoria, malikia maarufu wa Uingereza akiwa na umri wa miaka 82. Victoria alizaliwa mjini London mwaka 1819 Miladia, huku akichukua nafasi ya William IV kiutawala ambapo alisalia katika madaraka kwa kipindi cha miaka 64. Katika utawala wa Alexandrina Victoria, kulishtadi ukandamizaji dhidi ya raia wa nchi hiyo. Kufariki dunia malikia huyo ilikuwa mwanzo wa kudhoofika utawala wa kifalme ambapo baada yake aliingia madarakani Edward VII.
Siku kama ya leo miaka 45 iliyopita, alifariki dunia Lyndon B. Johnson, rais wa Marekani wa 36. Johnson aliingia madarakani tarehe 22 Novemba mwaka 1963 akiwa na umri wa miaka 55, baada ya kuuawa John F. Kennedy nchini humo. Mwaka mmoja baadaye, yaani sawa na tarehe 3 Novemba mwaka 1964, Johnson alikuwa rais mpya wa Marekani baada ya kushinda katika uchaguzi. Moja ya matukio makubwa yaliyojiri katika kipindi cha miaka mitano ya uongozi wake ni kuingia katika vita vya wazi na nchi ya Vietnam, kwa kisingizio cha kushambuliwa meli ya Marekani na meli ya kijeshi ya Vietnam. Katika vita hivyo serikali ya Marekani ilipata hasara kubwa ya mabilioni ya Dola, huku vikisababisha maelfu ya raia wasio na hatia wa Vietnam kuuawa. Kutokana na kuchukiwa na wananchi wa Marekani hasa baada ya kuiingiza nchi hiyo vitani, Lyndon B. Johnson aliamua kutoshiriki katika uchaguzi wa rais uliofuatia yaani mwaka 1968, huku Richard Nixon akichaguliwa baada ya kuahidi kuhitimisha vita hivyo.
Siku kama ya leo miaka 38 iliyopita, inayosadifiana na tarehe Pili Bahman 1357 Hijria Shamsia, watu kadhaa waliuawa na wengine kujeruhiwa, baada ya kujitokeza mapigano ya barabarani kati ya wananchi wa Iran na vikosi vya utawala wa Kifalme hapa nchini. Wananchi Waislamu wa Iran walikuwa kwenye maandalizi ya kumpokea Imam Khomeini. Wananchi wa matabaka mbalimbali kutoka mijini na vijijini walikuja mjini Tehran kwa shabaha ya kumlaki Imam Khomeini akitokea uhamishoni nchini Ufaransa. Wakati harakati hiyo ya wananchi ikiendelea, maafisa wasiopungua elfu nne wa jeshi la anga, walionyesha uungaji mkono wao kwa wananchi, na kutangaza mgomo wa kula chakula, sanjari na kutaka washauri wa Kimarekani waliokuwepo hapa nchini waondoke mara moja.