Jan 24, 2017 02:53 UTC
  • Jumanne, 24 Januari, 2017

Leo ni Jumanne tarehe 25 Rabiuthani 1438 Hijria sawa na Januari 24, 2017.

Mwaka 288 Hijria katika siku kama ya leo, alifariki dunia Thabit bin Qurrah Swabi, mtaalamu wa hesabati, nyota na tabibu katika kipindi cha utawala wa Bani Abbas. Alizaliwa mwaka 221 Hijria mjini Harran uliopo eneo la Mesopotamia nchini Iraq. Thabit bin Qurrah Swabi alikuwa akizungumza lugha za Kigiriki, Kiasyria na Kiarabu. Alisafiri kwenda mjini Baghdad, Iraq kwa lengo la kusoma na kwa usimamizi wa Muhammad bin Musa aliyekuwa mtaalamu mkubwa Mwislamu wa hesabati na nyota kipindi hicho, Thabit bin Qurrah Swabi akaingia katika uwanja wa elimu hizo. Alibuni nadharia mpya katika uwanja wa hesabati. Aidha katika utaalamu wa nyota yeye ni katika watu wa kwanza kurekebisha chombo cha Ptolemaic. Thabit bin Qurrah Swabi aliandika vitabu vingi katika uwanja wa tiba, hesabati na nyota, vilivyofasiriwa kutoka lugha ya Kigiriki kwenda Kiarabu. Miongoni mwa vitabu hivyo ni pamoja na kile kiitwacho "Adh Dhakhiratu fii Ilmi al Twib" na "Kitabul Mafrudhaat."

Thabit bin Qurrah Swabi

Miaka 1070 iliyopita mwaka 368 Hijiria, alizaliwa mjini (Corduba, Qurtuba) Uhispania, faqih, mtaalamu wa hadithi, fasihi na mwanahistoria Abu Omar Yusuf bin Abdallah mashuhuri kwa jina la Abdul Birr. Alipata masomo ya msingi kutoka kwa baba yake na walimu wengine wakubwa wa kipindi hicho. Ibnu Abdul Birr aliupa umuhimu mkubwa utafiti, ambapo kwa kipindi cha muda mfupi alikuwa mmoja wa wasomi wakubwa wa mjini Andalusia. Kufuatia kukosekana amani na usalama katika mji wa Corduba, Ibn Abdul Birr alilazimika kuhamia mji mwingine wa Daynah ambao kipindi hicho ulikuwa moja ya vituo muhimu vya elimu vya Andalusia, na huko alifanikiwa kuandika vitabu vyake. Miongoni mwa athari za msomi huyu mashuhuri ni kitabu cha "al Istiiab" ambacho kinahusu maisha ya masahaba wa Mtukufu Mtume Muhammad (saw).

ابن عبدالبر

Siku kama ya leo miaka 350 iliyopita, mkataba wa Breda ulitiwa saini kati ya Uingereza na Uholanzi. Kwa mujibu wa mkataba huo, Uholanzi ambayo haikuwa na uwezo wa kulinda makoloni yake katika bara lililokuwa ndio kwanza limegunduliwa la Amerika, iliyakabidhi makoaloni yake hayo kwa Uingereza. Eneo muhimu ambalo Uingereza ilikabidhiwa ni New York, ambalo leo kijiografia linapatikana mashariki mwa Marekani.

Mkataba wa Breda ulitiwa saini kati ya Uingereza na Uholanzi

Katika siku kama ya leo miaka 158 iliyopita, kisima cha kwanza cha mafuta kilichimbwa na mada hiyo muhimu ikatolewa chini ya ardhi kwa mara ya kwanza katika historia katika jimbo la Pennsylvania nchini Marekani. Kisima hicho kilichimbwa na Edwin Laurentine Drake kikiwa na kina cha urefu wa mita 230. Uchimbaji wa kisima hicho uliendelea kwa kipindi cha mwaka mmoja. Vifaa vilivyotumika kuchimbia kisima hicho vimehifadhiwa hadi leo katika jumba moja la makumbusho nchini Marekani.

Kisima cha kwanza cha mafuta duniani

Miaka 52 iliyopita katika siku kama ya leo, aliaga dunia Winston Churchill, mwanasiasa maarufu wa Kiingereza akiwa na umri wa miaka 91. Churchill alizaliwa mwaka 1874 na mwaka 1895 alijiunga na jeshi la Uingereza na kushiriki katika vita vya kikoloni. Mwaka 1900 Winston Churchil aliingia katika bunge la Uingereza akikiwakilisha chama cha Kihafidhina na mara kadhaa aliongoza wizara mbalimbali na kwa vipindi viwili alikuwa Waziri Mkuu wa Uingereza.

Winston Churchill

 

 

Tags